Ahadi ya Kindiki yakosa kurudisha wanafunzi shuleni
HATIMA ya mamia ya wanafunzi kutoka shule zilizoathiriwa na ujangili Pokot Magharibi haijulikani, baada ya kukosa kuripoti shuleni tangu zilipofunguliwa Januari.
Ingawa serikali ilitangaza kukarabati shule hizo pamoja na kuimarisha usalama, sasa imewekwa kwenye darubini kuhusu kujitolea kwake kuimarisha usalama katika eneo hilo.
Karibu shule saba katika maeneo yaliyo na utovu wa usalama kama Chesegon na Turkwel zilifungwa miaka miwili iliyopita.
Serikali ilitoa Sh100 milioni kukarabati miundo mbinu na kununua vifaa vipya kwa shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel na shule za msingi za Samplomoi, Chesegon, Arpollo na KSA, kwenye mpaka wa kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.
Wanafunzi wa shule hizo hawakufanya mtihani wao wa darasa la nane (KCPE) na ule wa gredi ya sita (KPSEA) mwaka jana, kutokana na visa vya utovu wa usalama.
Shule zingine ni za msingi kama Lonyangalem, Kour, Songok, Karon katika kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini na za msingi za Tirap na Cheratat katika kaunti ndogo ya Pokot ya kati.
Wakazi na viongozi wa eneo hilo, sasa wanauliza ikiwa ahadi ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Prof Kithure Kindiki mwaka jana, ilikuwa ya kuwahadaa.
Kulingana na wakazi, wale ambao walikuwa wakikarabati shule hizo, walikuwa hapo kwa siku chache na kuondoka na sasa wanataka kujua ikiwa shughuli hiyo itaendelea ama ilikwama.
Uchunguzi unaonyesha kuwa, ukarabati kwenye shule hizo ulisimama. Sasa wakazi na viongozi wanataka kuambiwa sababu ya ujenzi huo kukwama.
Wanasema kuwa kuna njama fiche wakidai ufisadi na sasa wanataka Prof Kindiki na mwenzake wa Elimu, Bw Ezekiel Machogu, kuingilia kati suala hilo.
Imebainika kuwa wanafunzi wengi hawako kwenye shule ambazo ziliathirika.
Uchunguzi katika shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel eneo la Chesegon, unaonyesha kuwa wanafunzi wa shule hiyo bado wanasomea shule ya msingi ya Surumben, wadi ya Masol,umbali wa kilomita 50.
Mkazi wa eneo la Cheptulel, Bw Kelvin Mweutich, alisema kuwa serikali ilifanya kazi duni isiyofaa kwa kukarabati shule hizo.
“Ujenzi huo haukufanywa vile inafaa. Hakuna vyoo. Chumba cha maankuli na bweni hazikutengenezwa na madirisha ambayo yalipasuliwa na majangili hayakurekebishwa. Walipaka tu rangi mbele ya shule. Tunataka kujua penye fedha hizo za ukarabati zilienda na ni nani alihusika,” alisema.
Alisema kuwa wiki hii mifugo 27 waliibiwa kutoka eneo hilo.
Mwalimu mkuu wa shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel, Bw James Koitilo, alisema hakuna maji kwenye shule hiyo baada ya paipu kuharibiwa, akieleza kuwa sehemu ya jikoni iliangushwa, nyumba za walimu kuharibiwa na mabati kuondolewa na majangili, vyoo vikivamiwa na mchwa.
“Tunapokea wanafunzi na hata tumepata 52 wa kidato cha kwanza. Mwaka jana hatukuwa na wengi sababu tulikuwa nao wanane. Shule ilifunguliwa Machi mwaka jana na tukapata mahali mbadala pa kusomea eneo la Surumben,” alisema.
Viongozi wa eneo hilo ambao walizuru shule ya upili ya wavulana ya Cheptulel, Alhamisi wakiongozwa na Seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Julius Murgor, mbunge wa Sigor, Bw Peter Lochakapong na mwakilishi wakike Pokot Magharibi, Bi Rael Kasiwai, walisema kuwa shule hizo haziko tayari kwa wanafunzi kusomea kwa sasa sababu ukarabati haukumalizika.
Hata hivyo, Kamishna mpya wa kaunti, Bw Khalif Abdullahi, alisema kuwa anafuatilia suala hilo na atahakikisha kuwa hatua kamili zinafuatwa.