Ajabu shule kupokea mgao wa Sh87 kutoka kwa serikali
HASIRA zimezidi miongoni mwa walimu wa shule za umma sio tu kufuatia kucheleweshwa kwa mgao wa muhula wa pili wa mwaka 2025, bali kiasi cha pesa ambazo shule zao zilitumiwa.
Walimu wakuu wengi sasa wanaonya kuwa shughuli za masomo na za ziada zitalemazwa kabisa iwapo hali haitarekebishwa.
Baadhi ya wakuu wa shule walishangazwa na kiasi kidogo cha fedha walizopokea, wengine wakisema ni cha kuchekesha.Kwa mfano, baadhi ya shule zilipokea kati ya Sh87 hadi Sh4,000, kiasi kilichoshangaza walimu na wazazi wa shule hizo.
“Nilipokea taarifa ya benki kwamba Sh87 pekee ndizo zilitumwa kwenye akaunti ya shule. Nilipofuatilia akaunti, nilibaini ni kweli. Hakutakuwa na shughuli shuleni katika muhula wa pili. Tumeonywa tusiombe msaada kutoka kwa wazazi. Naheshimu hilo. Lakini lazima tuseme. Hatupaswi kufa kimya tukijaribu kusimamia shule bila pesa,” alilalamika mkuu mmoja wa shule ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu ya hofu ya kuadhibiwa.
Mwalimu mwingine alitaka Bunge kumhoji Waziri wa Elimu kueleza kwa nini kiasi kidogo cha fedha kilitolewa kwa shule.“Bunge lijue. Wizara itolewe jasho. Wanafunzi wetu wana haki. Wazazi wana haki. Sisi pia tuna haki. Bajeti si maneno, ni pesa. Tutafunza bila chochote?” alisema mwalimu huyo.
Kilio hicho kilirudiwa na shule nyingine ndogo ya umma inayoendelea kuangamia kwa kukosa miundombinu, walimu wa kutosha, na fedha muhimu hali inayoathiri ubora wa elimu kwa wanafunzi.
Bw Mark Onyango, mkuu wa shule ya msingi na sekondari ya Ng’op Ngeso katika eneobunge la Seme, Kisumu, alisema shule hiyo inapambana kuendelea kuwepo huku changamoto zikizidi.
Shule hiyo iliyoanzishwa miaka ya 1980, kwa sasa ina wanafunzi 125 katika shule ya msingi na 33 wa sekondari msingi.
Tangu alipoteuliwa Juni 2022, Bw Onyango amekuwa akikabiliana na majengo duni, upungufu wa walimu na ukosefu mkubwa wa vifaa vya kufunza.
“Madarasa yetu mengi ni mabovu, kuna mashimo sakafuni na madirisha yaliyovunjika yenye nyaya hatari. Hatuna madarasa ya kutosha kwa JSS, na wanafunzi wa darasa la saba hawana sehemu nzuri ya kusomea,” alisema.
Shule ina walimu sita tu wa shule ya msingi na mmoja wa JSS licha ya kuwa na madarasa mawili, la saba na la nane.
Hali hiyo imesababisha walimu wa shule ya msingi kufundisha pia JSS, hali inayowalemaza na kuathiri ubora wa elimu.
Licha ya changamoto hizi, fedha zilizotumiwa shule zimeshangaza zaidi.
“Tulipokea Sh4,155 pekee kwenye akaunti ya shule. Sasa tunatarajiwa kutumia pesa hizo kwa shughuli zote ikiwemo kuimarisha miundomisingi. Sijui kwa nini Wizara inatutesa namna hii,” alisema.
Mgao wa shule hugawanywa katika sehemu mbili: ada za masomo na matumizi ya kawaida ya shule.
“Akaunti ya matumizi ya kawaida huendesha mishahara ya wafanyakazi wa mkataba, ukarabati, kulipia umeme, shughuli za ziada, usafiri wa ndani, miongoni mwa mahitaji mengine.
Hatujui tuanzie wapi,” aliongeza.Katika muhula wa pili mwaka 2024, shule ilipokea Sh14,808 kwa matumizi ya kawaida na Sh11,520 kwa ada ya masomo ya shule ya msingi.
Kwa upande wa JSS, shule ilipokea Sh302,108 kwa matumizi ya kawaida na Sh24,449 kwa ada ya masomo muhula wa pili wa 2024.
Kulingana na Bw Onyango, bajeti ya mwaka huu inaonyesha tofauti kubwa kati ya mahitaji halisi na fedha walizopokea.
Kwa mfano, shule inahitaji Sh1,048,543 kwa mwaka, lakini katika muhula wa kwanza ilipokea Sh147,340 pekee na kulazimika kukopa au kutegemea wahisani.
“Tulilazimika kuajiri mwalimu mmoja wa JSS kwa fedha zetu, tukimlipa Sh10,000 kwa mwezi. Mlinzi wa usiku analipwa Sh6,000. Bajeti yetu inakuwa ngumu mno,” alisema.
Mnamo Mei 20 2025 Wizara ya Elimu ilitoa Sh22.03 bilioni kama mgao wa muhula wa pili baada ya kuchelewa kwa wiki tatu.
Waziri wa Elimu Julius Ogamba alisema kuwa fedha hizo zilitolewa kusaidia shughuli za masomo na kupunguza matatizo ya kifedha yanayokumba shule nyingi tangu mwanzo wa muhula.
Hata hivyo, hakufafanua kiwango kilichotengwa kwa kila mwanafunzi au kama kiasi hicho kinajumuisha fedha ambazo hazikutolewa katika muhula wa kwanza. Pia hakuelezwa wazi iwapo fedha hizo ni sehemu ya asilimia 30 ya mgao inayopaswa kutolewa kwa muhula wa pili.