Ajabu ya Wakenya kukopa Sh15 bilioni kwenye Apu za simu kununua chakula – Ripoti
KATIKA hali ya kusikitisha inayoakisi hali ngumu ya maisha nchini, Wakenya wengi sasa wanalazimika kukopa pesa kupitia Apu za mikopo ya dijitali ikiwemo Fuliza, Tala, Branch na Zenka, ili kupata chakula cha kila siku.
Kwa mujibu wa ripoti mpya, zaidi ya Sh15 bilioni hukopwa kila mwezi kupitia majukwaa haya – pesa ambazo nyingi hutumika kwa chakula, kodi, na mahitaji ya msingi.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Chama cha kampuni za kutoa Mikopo Kidijitali nchini (DFSAK) inaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 8 wanategemea mikopo ya kidijitali kila mwezi.
Hii inaashiria ongezeko kubwa la kutegemea mikopo kwa maisha ya kila siku, badala ya uwekezaji au shughuli za maendeleo. Hii ikiwa ishara ya umasikini.
Mwenyekiti wa DFSAK, Kevin Mutiso, asema kuwa idadi inaongezeka.
“Tangu 2010, kampuni wanachama wetu wamekopesha zaidi ya Sh15 bilioni kila mwezi kwa Wakenya zaidi ya milioni nane. Hii imeonyesha jinsi sekta hii imekuwa tegemeo kwa wananchi,” alisema.
“Kama raia anakopa ili ale leo, basi hiyo ni ishara ya hatari ya kiuchumi. Mikopo ya chakula haina faida ya muda mrefu, bali huzidisha kuitegemea,” asema mchambuzi wa sera za kiuchumi, Dkt Humphrey Kimani.
Kwa upande mwingine, mikopo hiyo hutozwa riba na ada za juu, hali inayowaacha wengi wakihangaika kulipa madeni badala ya kujiendeleza.
Kukopa Sh500 kunaweza kumgharimu mkopaji zaidi ya Sh600 baada ya siku chache hali inayozidisha madeni.
Serikali inapaswa kuchukua hatua za dharura kudhibiti gharama ya maisha, kuongeza ajira na kuweka sheria bora za kudhibiti mikopo ya dijitali, ili kuzuia raia kuzama zaidi katika mikopo kwa kulemewa na hali ya uchumi.