Afueni benki ikiongeza kiasi mteja anaweza kutuma kidijitali kwa siku
BENKI zimeanza kuongeza kiasi cha pesa ambazo mteja anaweza kutuma kupitia apu za simu.
Hii ni baada ya benki ya Co-operative Kenya kuongeza kiasi hicho hadi Sh2 milioni kwa siku.Wataalamu wanasema hatua hii itawafaa wateja kwa kuwa watu wengi wanatumia dijitali kwa shughuli zao za kifedha.
Kiasi hicho ni ongezeko mara nne kutoka Sh500,000 ambazo Benki ya Co-operative imekuwa ikiruhusu wateja kutuma kupitia apu yake ya MCoopCash.
Benki hiyo ilifahamisha wateja kuhusu hatua hiyo kwa kusema Sh2 milioni zinaweza kutumwa kwa awamu mbili kumaanisha mtu atakuwa akituma Sh1 milioni mara mbili kufikisha kiasi cha juu ambacho benki imeruhusu kwa siku.
‘Mpendwa mteja, kwa kutumia MCoopCash, sasa unaweza kutuma hadi Sh2 milioni kwa siku kutoka akaunti moja ya Benki ya Co-op hadi nyingine, kwa awamu mbili za hadi Sh1 milioni kila moja,’ benki ilisema katika ujumbe kwa wateja.
Kiasi hicho pia ni zaidi ya Sh500,000 ambazo Co-op Bank inaruhusu wateja kutuma kupitia PesaLink.
Kiasi hicho kipya kinajiri huku benki ikiongeza kiasi ambacho wateja wanaweza kutoa katika ATM kwa kila siku hadi Sh60,000.
Kabla ya Januari mwaka huu, mteja angeweza kutoa Sh40,000 kwa ATM. Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema hii itawapa wateja nafasi ya kufanya shughuli zao hasa katika maeneo ambayo usalama unaweza kuwa changamoto.
Utafiti kuhusu hisia za wateja wa Chama cha Mabenki cha Kenya uliotolewa katikati ya Machi ulionyesha asilimia 45.7 ya wateja walipendelea majukwaa ya dijitali ikiwa ni pamoja na simu za mkononi, Intaneti, na chatbots, kwa huduma zao za benki.
Hii ni tofauti na asilimia 16.5 wanaopendelea huduma zinazosaidiwa na binadamu ikiwa ni pamoja na maajenti na matawi ya benki.
Washiriki wa utafiti waliorodhesha Benki ya Co-op kama benki bora zaidi kwa ujumla katika uzoefu wa wateja kwa mwaka wa pili, ikifuatiwa na Benki ya NCBA na Family Bank mtawalia.