Ajichumia riziki kutokana na ufugaji kuku wa aina tofauti
JOGOO mweupe wa kilo 5.5 ndiye alikuwa kivutio kikuu katika maonyesho ya mwaka huu ya kibiashara na kilimo Kaunti ya Nairobi, yanayoandaliwa na Baraza la Kilimo Kenya (ASK) kila mwaka, baada ya kutangazwa kuwa bora zaidi kitengo cha kuku.
Jogoo huyo wa aina ya Brahma, ni kati ya kuku wanaofugwa na Fredrick Omondi, mfugaji na mwanzilishi wa Kimalat Holdings Ltd, kampuni iliyoko Kimalat, Kitengela, Kaunti ya Kajiado.

Omondi ni mfanyabiashara anayefanya ufugaji mseto wa ndege, ambapo kwa sasa ana zaidi ya kuku 300 wa Brahma.
Aliingilia ufugaji miaka mitatu iliyopita, na leo hii jogoo wake maridadi mwenye manyoya marefu, meupe yanayofika hadi miguuni, kifua kipana na umbo la kuvutia, amemletea heshima kubwa.
Kulingana na Omondi, majaji wa maonyesho ya ASK ambayo yalifanyika kati ya Septemba 29 na Oktoba 5, 2025, walizingatia ukubwa, afya, umri na jinsi kuku huyo alivyotunzwa.

Jogoo wake huyo wa miezi tisa pekee, aliongoza kwa uzito wa kilo 5.5, wakati kuku wa kawaida huwa na kati ya kilo 2.5 hadi 3.
“Jogoo huyu ni mpole, jasiri na wa kupendeza. Wengine humfuga kama ndege wa mapambo kutokana na urembo wake,” Omondi anasema.
Brahma ni kuku mwenye asili ya Amerika Kusini, na anajulikana kwa mwili mkubwa wenye nyama nyingi na manyoya mazito.
Omondi anasema jogoo huyo bora ni kizazi cha pili baada ya wa kwanza aliyekuwa na kilo 7 kufariki mwaka jana, 2024.
Mwonekano wa jogoo wake wa kifahari wakati wa ASK ulimfanya kuwa kivutio kikuu, huku watoto na wageni walioshiriki wakiomba kupiga picha naye.
“Ni matokeo ya kazi ya mikono yangu, uvumilivu na kujifunza kila siku,” mfugaji huyo akaambia Akilimali kupitia mahojiano ya kipekee.
Siri ya kufuga
Siri ya kuku wake wenye uzito mkubwa, alifichua, ni kwa ajili ya kukumbatia ufugaji wa kiasili.
Aidha, alidokeza kwamba anatumia mfumo wa kuachilia kuku na ndege wake kujitafutia malisho, ambapo kuku hutembea wakiwa huru mchana kwenye kichaka kilichoko karibu na mradi wake Kitengela, wakila vyakula vyenye protini nyingi kama panzi, siafu na mabaki ya mboga.

“Protini ndiyo nguzo kuu ya ukuaji. Nawapa wadudu, majani, mabaki ya chakula cha jikoni, na matokeo yake ni kuku wenye afya na uzito wa kustaajabisha,” anaeleza.
Kupitia mfumo huo, anakiri kupunguza gharama ya ufugaji kwa karibu asilimia 70.
Alipoulizwa ofa ambayo anaweza kuchukua kwa jogoo huyo kidedea anayesisitiza ni nyota wake, alijibu, “Usipokuwa na zaidi ya Sh10, 000 kamwe siwezi nikakuuzia.”
Kando na kufuga Brahma, Omondi pia ana kuku aina ya Kenbro wapatao 400, ndege wa mapambo kama vile Japanese Silkie na Polish Bantams, na kanga wasiopungua 800. Kwa mwezi, anakadiria kuuza Brahma 100 na vifaranga wa Kenbro 800.

Anajivunia mradi wake wa ufugaji, anaosema alianza na Brahma watatu pekee, ambao sasa umekuwa kivutio cha mashabiki wa kuku na ndege.
Kutoka kwa mtaji wa Sh50, 000, hii leo unamuingizia maelfu ya pesa akisema hivi karibuni anapania kupanua biashara yake huku akiwekeza kwa utumiaji sola kufanikisha uanguaji wa vifaranga.