Akili Mali

Aliacha kazi ya benki akaanza ufugaji wa nguruwe na kufurahia mapato

October 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

TAKRIBAN miaka 10 iliyopita, Jassan Mureithi alikuwa benkini katika wadhifa wa afisa wa mikopo.

Kazi yake ilikuwa aghalabu ni kutathmini ufaafu wa wateja kupata viwango mbalimbali vya mikopo.

Sehemu kubwa ya wateja hao ilikuwa inajishughulisha na kilimo biashara na hakuwa na hofu kuwa walikuwa wanastawi.

Baada ya kudadisidadisi, akagundua waliokuwa wanafuga nguruwe walitabasamu kupata utamu wa pesa walipofika kuweka akiba na kulipa mikopo.

“Asilimia 70 ya wateja niliowashughulikia walikuwa wanajihusisha na ufugaji wa nguruwe,” alifichua.

Hapo ndipo safari ya shamba la kufugia nguruwe la Goldmine ilianzia.

Jassan Mureithi akiwa katika shamba la mihindi inayotumiwa kulisha nguruwe Kiambu. Picha|Labaan Shabaan

Akizungumza na jarida la Akilimali shambani mwake Ndumberi, kaunti ya Kiambu, Jassan alisema anamiliki takriban nguruwe 300.

Mashamba yake mawili – moja Kiambu na jingine Muranga – yamekuwa tegemeo kubwa maishani mwake tangu kazi ya benki imwone paa.

Katika kipindi ambacho Kuna changamoto ya gharamba ghali ya malisho ya mifugo, Jassan ameondokea kujikuzia malisho.

Ana mashamba ya mahindi na mimea mingine ya kulishia nguruwe wake.

Isitoshe, mfugaji huyu hununua vyakula kutoka kampuni ya Farmers Choice kukidhi nakisi ya virutubisho katika malisho anayolima.

Wakulima wengine pia hufululiza humu kununua malisho ya mifugo yao kama vile ng’ombe, mbuzi na nguruwe.

Kupitia njia hii, Jassan huongeza viwango vya faida katika anazopata kutoka kwa mauzo ya nguruwe.

Jassan Mureithi akiwa katika shamba la mihindi inayotumiwa kulisha nguruwe Kiambu. Picha|Labaan Shabaan

Haya yote yametokana na hatua yake ya ujasiri kujasiria kupiga teke kazi ya kuajiriwa na kuamua kujiajiri.

Anakumbuka alivyoanza na nguruwe wake wawili waliokuwa karibu kuzaa na sasa nguruwe hawa wamemzalia maelfu ya nguruwe.

Gold Mine Pig Farm haijampa Jassan pekee nafasi ya ajira. Kuna wafanyakazi 7 wanaochapa kazi mbalimbali shambani kama vile kulisha nguruwe, kukuza malisho, kutoa matibabu na kadhalika.

Mmoja wa walionufaika ni mkurugenzi wa shamba, Maureen Wanjiru ambaye ana tajiriba pana ya ufugaji.

Maureen hutumika sana kutoa mafunzo ya njia bora za ufugaji nguruwe kwa wateja wanaozuru shamba lao.

Anawashauri wakulima wasifuge nguruwe wa aina moja shambani kwa sababu spishi tofauti huwa na manufaa tofauti maalum.

“Tuna aina ya Landrace, Large white, Duroc na Maxgro ambao tunawafanya kuzaliana ili kupata aina nyingine yenye ubora,” alisema Wanjiru.

Shamba hili la nguruwe kadhalika huwafugia nguruwe wachanga wakulima wanaoanza kukumbatia ufugaji huu.

“Tunauza nguruwe Farmers Choice na wengine tunawachinja na kuuza kwenye bucha maeneo ya Kiambu, Muranga na Nairobi,” alieleza Mureithi ambaye huchinja angalau nguruwe watano kila siku.

Kuhakikisha yuko sokoni kila siku, Mureithi ana nguruwe katika viwango mbalimbali vya ukuaji na hakuna shaka kwamba anafurahia kilimo hiki.