Akili Mali

Amejiinua kimapato kupitia ufugaji wa samaki

Na PETER CHANGTOEK December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MICHELLE Mbeo alijitosa katika ufugaji wa samaki aina ya tilapia miaka kumi na miwili iliyopita, katika eneo la Mfangano Island.

Ni mwasisi wa kampuni ya Lake View Fisheries (LVF) inayohusika na uzalishaji wa samaki.

Anasema kuwa, alijitosa katika shughuli hiyo kwa lengo la kahakikisha kuwa kuna samaki wa kutosha wanaofugwa kwa kutumia teknolojia za kisasa za ufugaji, na kuimarisha uchumi kwa wafugaji na watu wengine husika katika sekta hiyo.

“Pia, kulikuwa na haja ya kubuni nafasi za kazi kwa jamii katika kisiwa kilichotengwa cha Mfangano,” asema Michelle, ambaye alisomea taaluma ya teknolojia ya habari.

Vidimbwi vya samaki vinavyotumika kwa uzalishaji wa samaki wadogo katika shamba la Lake View Fisheries. PICHA|PETER CHANGTOEK

Mfugaji huyo ambaye amewahi kuhudumu katika mashirika ya kimataifa kama vile Accenture and GE Healthcare, anasema kuwa, ana vizimba 14 aina ya HDPE, vinavyotumika kwa ufugaji. Aidha, ana vidimbwi 18 vilivyotengenezwa kwa karatasi za sandarusi.

Anaongeza kuwa, wana eneo la kuzalisha samaki wadogo, ambapo wana uwezo wa kuzalisha samaki wadogo milioni moja, wenye ubora wa kiwango cha juu. “Tunatumia vizimba vinavyozalisha hadi tani 1,000 za samaki kwa mwaka mmoja,” asema mfugaji huyo.

Hata hivyo, anasema kuwa, licha ya kwamba Lake View Fisheries imepiga hatua ya kuzalisha tani 1,000 kwa mwaka, uzalishaji huo hauwezi kutosheleza hitaji kubwa la samaki nchini, ambayo ni tani 450,000 kwa mwaka.

Kwa hivyo, anasema kuwa, wanapania kuagiza vizimba vingine 20, ili kuzidisha idadi ya samaki wanaozalishwa nao.

“Hatua hii itatusaidia kutimiza azimio letu la 2030, la kuzalisha samaki tani 5,000 za samaki waliokomaa kwa mwaka,” afichua Michelle.

Anasema kuwa, Lake View Fisheries ina wafanyakazi wa kudumu 18, na wengine 33, ambao ni wasaidizi.

Anaongeza kuwa, asilimia 66 ya wafanyakazi hao ni wanawake.

Wafanyakazi wakilisha samaki. PICHA|PETER CHANGTOEK

Anadokeza kuwa, teknolojia wanayoitumia inawapa fursa ya kuwasilisha samaki sokoni kwa muda wa miezi sita hadi minane, ikilinganishwa na miezi kumi au kumi na miwili ambayo samaki hao wangechukua, endapo teknolojia hiyo isingetumika.

Kuanzia mwaka 2021-2022, Lake View Fisheries iliwekeza kwa teknolojia ya RAS, inayorahisisha shughuli ya uzalishaji wa samaki, kwa kuwa halijoto hudhibitiwa teknoloji hiyo inapotumika.

Michelle anasema kuwa, wana wafugaji 1,200 wanaonufaika kwa mafunzo wanayotoa kwao.

Pia, wafugaji hao huunganishwa na wauzaji pembejeo, na kuunganishwa pia na wateja.

Mfugaji huyo anasema kuwa, kuna baadhi ya changamoto katika shughuli ya ufugaji wa samaki, kama vile gharama ya juu ya mafuta ya majenereta.

Aidha, shughuli hiyo inahitaji vifaa vya bei ghali vinavyotumika kuhifadhi samaki ili wasiharibika; kama vile majakofu maalumu.

Vizimba vinavyotumiwa na Lake View Fisheries kuwafuga samaki. PICHA|PETER CHANGTOEK.

“Samaki wadogo huwekwa kwa vizimba vyao, na wanaobaki huuzwa kwa wakulima wafugaji wadogowadogo,” aongeza.

Samaki waliokomaa na kuvuliwa huuzwa kwa maduka manane ya Lake View Fisheries, yaliyoko katika sehemu tofauti tofauti. “Baadhi ya samaki hupelekwa kwa shule na katika hafla mbalimbali za kijamii,” aongeza mfugaji huyo.

Mfugaji huyo anafichua kwamba, asilimia 65 ya vitu vinavyohitajika katika ufugaji wa samaki ni lishe, na ni muhimu kununua lishe zilizo na kiwango cha juu cha ubora.

Lake View Fisheries hununua lishe kutoka kwa kampuni ya Tunga Feeds. Aidha, hununua neti kutoka kwa kampuni ya Monasa Nets, na karatasi za sandarasi kutoka kwa kampuni ya East Africa PVC.

“Miaka mitano ijayo, Lake View Fisheries inapania kuuza samaki aina ya tilapia kwa wanunuzi wa kimataifa,” anasema Michelle.