Akili Mali

Ameona faida kuu kwa kuunda bidhaa kutokana na nazi

Na SAMMY WAWERU October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

AKIWA na umri wa miaka 66, ambapo wengi wangeamua kupumzika na kufurahia maisha ya uzeeni, Bw Hamisi Mwakumanya kutoka kijiji cha Mwabuga, Kaunti ya Kwale, amegeuza nazi kuwa dhahabu.

Anatumia zao hili linalokuzwa kwa wingi eneo la Pwani, kuunda bidhaa zinazovuma sokoni kama mafuta asilia ya nazi, losheni, dawa za nywele, makaa, mazulia na bidhaa nyingine nyingi ambazo sasa zimegeuka kuwa alama ya ubunifu na ujasiriamali wa Pwani.
Akilimali ilikutana naye katika ukumbi wa kijamii wa Tononoka, Mombasa, wakati wa mdahalo kati sekta ya umma na binafsi kuhusu biashara ndogondogo.

Bw Mwakumanya alikuwa akihudumia wateja kwa tabasamu, huku akifuta jasho usoni mwake.
Meza yake ilikuwa imepangwa kwa ustadi na chupa za mafuta, losheni zilizochanganywa na aloe vera (shubiri) na mwani (seaweed.
“Kama una ngozi kavu, nataka utumie mchanganyiko wa nazi na aloe vera. Huponya haraka,” alisema huku akimpa mteja wake maelekezo kwa upole.
Kwa Bw Mwakumanya, biashara hii si ya kutafuta riziki tu, bali ni uthibitisho kuwa rasilimali za kiasili zikitumika kwa akili, zinaweza kugeuzwa kuwa utajiri wa kisasa na chanzo cha ajira.
Kutoka ajira rasmi hadi ubunifu wa nyumbani
Awali Bw Mwakumanya alifanya kazi serikalini na pia katika sekta binafsi, akiwa na kipato cha kutosha kumudu mahitaji ya familia yake. Hata hivyo, alipokaribia kustaafu miaka ya 2000, alianza kujiuliza kwa kina, “Baada ya ajira ni nini?”
Mwaka 2007, alijiunga na kikundi cha wakulima wa mazingira na miti kilicholenga kuhifadhi misitu katika kaunti hiyo.
Kupitia udhamini wa miradi ya kijamii, walipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia (JKUAT) kuhusu thamani ya nazi na mbinu za kuongeza bidhaa zake sokoni.
“Mafunzo yale yalifumbua macho yangu. Nikatambua nazi si tunda tu la chakula, bali ni rasilimali, biashara na riziki ya kweli,” akasema kwa tabasamu.
Bw Mwakumanya alisema nazi ikiuzwa sokoni kama tunda haina thamani sana ukilinganisha na kuuza bidhaa zake kama vile mafuta.
“Nazi sokoni inazwa Sh50 lakini chupa ndogo ya gramu 500 nauza kwa Sh1,000 napata faida maradufu,”anasema.
Akiwa na maarifa mapya, alianza majaribio nyumbani kwake kwa kutumia vifaa vya kawaida vya jikoni. Akaanza kutengeneza mafuta asilia, mkaa wa kijani, mazulia, mikeka, sabuni na bidhaa nyinginezo.
“Kila sehemu ya nazi ikawa bidhaa. Chicha hukamuliwa kuwa mafuta, makumbi na vifuvu hutumika kutengeneza mkaa, nyuzi kuwa mikeka na kamba, huku maji yake yakitumika katika vipodozi,” anaeleza.
“Niliamua hakuna kinachopotea. Kila kipande cha nazi kina thamani,” anasema.
Alianza kwa kuuza kwa majirani na jamaa wa karibu, lakini umaarufu ukasambaa polepole. Bidhaa zake zilipata soko katika masoko ya Likoni, Ukunda na Mombasa mjini, kabla ya kupenya hadi masoko ya Nairobi na Kisumu.
“Sasa ninapokea oda kutoka Kenya nzima na hata Uganda na Tanzania kupitia maonyesho. Wakati mwingine mahitaji huzidi uwezo wangu wa kuzalisha,” asema huku akicheka.
Biashara yake imeajiri vijana na kina mama zaidi ya kumi kutoka vijiji jirani, akiwapa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa na mbinu za masoko. Wengi wao, hasa wanawake, sasa wanauza bidhaa ndogo ndogo na kusaidia familia zao.
“Hawa vijana walikuwa hawana kazi. Niliona heri tushirikiane badala ya kila mtu kulalamika,” akasema.
Kwa wakazi wa Mwabuga, Bw Mwakumanya ni zaidi ya mjasiriamali,ni mwalimu, mlezi na mfano wa matumaini kwamba hata baada ya kustaafu, maisha yanaweza kuanza upya.
Mafanikio yake yalipata msukumo mkubwa baada ya kupata cheti cha viwango vya ubora kutoka Shirika la Kudhibiti Ubora Nchini (KEBS), jambo lililopanua soko na kuongeza imani ya wateja.
“Haikuwa rahisi,” alikiri. “Lakini baada ya kupata cheti hicho, bidhaa zangu zilianza kuaminiwa zaidi. Nilijua sasa niko katika biashara ya kweli.”
Hata hivyo, safari yake haijakosa changamoto. Upungufu wa nazi wakati wa kiangazi, gharama kubwa za vifungashio na uchapishaji wa bidhaa, pamoja na ukosefu mtaji, vimekuwa kizingiti kikubwa. “Wateja wanataka vifungashio vya kisasa na nembo nzuri. Kama ningepata mitambo bora na mtaji wa kutosha, ningetimiza oda kubwa zaidi,” akasema kwa matumaini.
Licha ya changamoto hizo, ndoto zake bado ni kuu. Anapanga kusafirisha bidhaa zake hadi Ulaya, Bara Hindi na Mashariki ya Kati.
Pia anapanga kuanzisha kiwanda kidogo cha kusindika nazi huko Kwale, kitakachohusisha vijana na wanawake kutoka maeneo ya Ukunda, Matuga na Lunga Lunga.

“Nataka Kwale ijulikane kwa bidhaa za ubora wa kimataifa. Vijana wasione ajira kama ndoto isiyowezekana,” akasema.
Anasema ujasiriamali wa aina hii ungetatua changamoto nyingi za ukosefu wa kazi Pwani ikiwa serikali na mashirika yangewekeza katika mafunzo na mitaji midogo kwa wajasiriamali wadogo. Mlezi wa kizazi kipya cha wabunifu. Mbali na biashara, Bw Mwakumanya sasa anahusishwa kama mlezi wa wajasiriamali wachanga.
Mara kwa mara hualikwa kutoa mafunzo katika maonyesho ya kilimo, semina za vijana na mikutano ya biashara. “Hii elimu lazima igawanywe. Vijana wetu wasikae wakisubiri ajira za ofisini. Asili imetupa rasilimali tayari,” akasisitiza.
Anawaelekeza vijana jinsi ya kutumia rasilimali zilizopo kijijini kama nazi, mwani na mikoko kutengeneza bidhaa zenye thamani kubwa.
“Ninaamini suluhu za ajira zipo mikononi mwetu. Tunachohitaji ni ubunifu na imani kuwa tunaweza,” Bw Mwakumanya akaeleza.
Anapoitazama safari yake, Bw Mwakumanya hana majuto ya kuondoka kwenye ajira rasmi. Kinyume chake, anasema maisha yake ya sasa yana furaha, uhuru na mafanikio zaidi.
“Kama kuna majuto, ni kupoteza muda mwingi kwa ajira. Yale niliyopata tangu 2007 yananipa furaha zaidi,” akasema. Kwa sasa, kila kipande cha nazi kimekuwa riziki kwake, akithibitisha methali ya Kiswahili: “Akili ni mali.”

Kwa wakazi wa Kwale, simulizi ya Bw Hamisi Mwakumanya ni ushuhuda kuwa ubunifu na bidii vinaweza kubadilisha maisha hata katika uzee.