Akili Mali

Anakuza mimea ya viungo na kuuza ughaibuni

Na PETER CHANGTOEK December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MIMEA ya viungo huhitajika mno katika maeneo mengi kote ulimwenguni, kwa ajili ya matumizi tofauti tofauti.

Viungo hutumika kuongeza ladha katika chakula, na pia hutumika katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

Baadhi ya wakulima nchini huikuza mimea ya viungo ili kuuza katika nchi za nje.

Judy Musisia, 30, ni mmojawapo wa wakulima wanaoikuza mimea ya viungo na kuuza ughaibuni. Alijitosa katika ukuzaji wa mmea wa thyme na viungo vingine miaka minne iliyopita katika eneo la Kantafu, Kaunti ya Machakos.

Mkulima huyo alifanya utafiti kwa kuzuru mashamba kadhaa yanayoendeleza ukuzaji wa mmea huo, katika eneo la Athi River, Nyahururu na Murang’a, ambapo alifahamu mengi kuhusu zaatari.

“Kukaa bila kazi ni jambo ambalo liliniathiri akili sana. Ni wakati ambapo nililazimika kufikiria kuhusu jinsi ya kupata pesa. Nilihitaji shughuli ambayo ingenipa fedha, kwa sababu kazi zetu zilisimama ghafla,” asema Musisia, ambaye alisomea shahada ya Ujenzi katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT), na kuhitimu mwaka 2017.

“Wazazi wangu wana shamba ekari kumi. Nilizungumza nao na wakiniruhusu nitumie sehemu ya shamba kuikuza mimea ya viungo,” asema Musisia, anayetumia shamba zaidi ya ekari moja.

Anasema kuwa, ili kufanikisha ukuzaji wa mimea ya viungo kama vile zaatari, jambo ambalo mkulima anafaa kuwa nalo akilini ni kuhusu maji. Kwake, maji hayakuwa tatizo, maadamu walikuwa nayo shambani.

Judy Musisia, mkulima wa mimea ya viungo akionyesha mimea yake katika Kaunti ya Machakos. PICHA|PETER CHANGTOEK

“Niliamua kutumia mbinu ya unyunyiziaji maji ya drip irrigation kwa sababu ni rahisi na maji mengi hayatumiki vibaya,” adokeza, akiongeza kuwa shughuli hiyo, pamoja na kununua tangi, kulimgharimu Sh250,000.

Musisia, anayetumia mbolea za kuku na ng’ombe kuikuza mimea, anasema kuwa nguvukazi ilimgharimu Sh100,000. “Nilitaka kukuza aina mbili za viungo; rosemary na zaatari. Mbegu za rosemary zikanigharimu Sh50,000 na zaatari gramu 500 zikanigharimu Sh17,600,” afichua.

“Mimi hufungulia maji kwa mimea mara mbili kwa wiki kwa muda wa dakika 30. Mimea inapoendelea kukua, hunyunyizia mbolea ya foliar au mkojo wa sungura. Huchanganya lita moja ya mkojo wa sungura na lita 20 za maji,” aeleza, akiongeza kuwa, mkojo wa sungura una kiwango kikubwa cha naitrojeni.

“Mmea huo huchukua muda wa miezi mitatu ili ianze kuchumwa, na huchukua muda wa miaka mitano,” aongeza mkulima huyo.

Hata hivyo, anasema kuwa kuna changamoto kadhaa katika kilimo hicho.

Miongoni mwa changamoto ambazo amepitia ni soko. Mmea huo aghalabu huuzwa ughaibuni, na ubora wa hali ya juu unahitajika.

“Mimi humtegemea mwuzaji anayeuza ughaibuni ili kuuza mazao yangu, na kufanya hivyo si jambo la kutegemewa,” asema, akiongeza kuwa, usafirishaji pia, hususan wakati wa mvua kubwa, huwa changamoto.

Anasema bei huathirika kuambatana na masoko ya ulimwengu.

Kwa wakati huu, huuza gramu 100 kwa Sh35.

“Kwa sasa, ninatafuta soko nchini kwa wauzaji viungo, hoteli na wakulima wengine ambao wanataka kununua,” aongeza.

Anawashauri wale ambao wananuia kujitosa katika ukuzaji wa mimea ya viungo kutafuta soko la mazao kwanza, kabla hawajaanza kuchuma. “Hilo litasaidia kunyoosha mchakato wako kwa kuzuia kuharibika kwa viungo na kufa moyo kwa kutokuwa na wateja,” asema.

Anafichua kuwa, ana mipango ya kuongeza kiasi cha shamba analotumia kwa ukuzaji.

“Nilianza kwa shamba ekari moja na nimejifunza kutoka kwa makosa yangu. Ningependa kuongeza, hasa kwa kuzingatia mafunzo niliyojifunza,” asema Musisia, akiongeza kwamba, anapania kuvijenga vivungulio atakavyovitumia kwa ukuzaji.

Aidha, anasema kuwa ananuia kulitafuta soko la mazao yake ughaibuni, na kupata kibali cha kuuza bidhaa zake kule.

Isitoshe, anadokeza kwamba ananuia kuwahamasisha wakulima wengine wakuze viungo vinavyokua vizuriP katika mazingira yao. Isitoshe, anasema kuwa, ananuia kuvitumia viungo anavyovikuza kutengeneza bidhaa kama vile sabuni, mafuta, n.k.