• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 1:16 PM
Corona ilimfungua macho kuanzisha kampuni ya huduma za kidijitali

Corona ilimfungua macho kuanzisha kampuni ya huduma za kidijitali

NA PETER CHANGTOEK

JANGA la ugonjwa wa Covid-19 lilipoanza na kisha kusambaa katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya, biashara na shughuli nyingine za watu kujitafutia riziki ziliathirika mno.

Watu wengi walifutwa kazi katika kampuni tofauti, huku wengine wakilazimika kufanyia kazi nyumbani kwao.

Miongoni mwa wale walioathirika ni George Rotich,30.

Hata hivyo, ujio wa ugonjwa huo ulimfaidi kwa njia nyingine, kwa sababu alilazimika kufikiria zaidi kuhusu jinsi ambavyo angefaidi katika wakati huo uliokuwa mgumu kwa watu wengi.

Aliianzisha kampuni yake mwaka 2021, ambayo inajulikana kama Jewel Films Digital yenye ofisi yake kuu Westlands, Nairobi.

Kampuni hiyo hushughulika na uundaji wavuti kwa wateja, upigaji picha na usanifishaji wa michoro, miongoni mwa huduma nyinginezo.

“Mimi ni mbunifu wa michoro na mpigapicha. Nina shahada ya diploma katika usanifu wa picha na upigaji picha kutoka Shaw Academy, Ireland. Kampuni yangu inashughulikia mahitaji maalum ya ubunifu kwa biashara ndogondogo na za kiwango cha kati,” Bw Rotich anasema.

Anaambia Akilimali kwamba haikuwa rahisi kwani alikabiliana na changamoto ya ugumu wa kupata mtaji wa kutosha.

Lakini anasema alilazimika kutumia rasilimali alizokuwa nazo kipindi hicho na kubana matumizi hapa na pale.

“Nilinunua kompyuta yenye uwezo wa kufanya kazi haraka upesi na kamera ya ubora wa hali ya juu ili kuanzisha biashara yangu,” anasema.

Kabla ya kujitosa katika biashara hiyo, kwanza alifanya utafiti kuhusu mianya au fursa za kibiashara sokoni.

Alitazamia kampuni ambayo ingeziba pengo kati ya biashara ndogondogo na za kiwango cha kati, na watoaji huduma kama zake.

Anaongeza kuwa, pia hupenda kufanya kazi na wanaoanzisha biashara. Hata hivyo, Rotich anasema kuwa, kupata wateja wapya kunaweza kuwa changamoto ya mara kwa mara katika soko lenye ushindani mkubwa.

Anasema kuwa, huwapata wateja wake mara nyingi wanaotumwa na wale wa awali, ambao wameshughulikiwa naye.

Aidha, huwapata wateja kutoka kwa marafiki.

Pia, huwapata wateja kutoka kwa majukwaa yao ya mitandao ya kijamii na tovuti.

“Facebook ni jukwaa linalotumika sana ambalo huturuhusu kufikia hadhira pana na kushirikiana na wateja watarajiwa. Kwa msisitizo wake katika usimulizi wa hadithi unaoonekana, Instagram ni jukwaa jingine muhimu la kuonyesha bidhaa za kampuni yetu kupitia picha za kuvutia na urembo ulioratibiwa,” asema, akiongeza kuwa, LinkedIn ni jukwaa jingine muhimu, ambalo huwezesha kampuni yake kufikia hadhira kubwa.

Bw Rotich anadokeza kwamba, ada zao ni nafuu, na wateja ambao wanajitosa katika biashara ndogo wanaweza kumudu.

Bw George Rotich,30, ni mwasisi wa kampuni ya Jewels Films Digital yenye makao makuu Westlands, Nairobi. PICHA | PETER CHANGTOEK

Anafichua kuwa, ana uzoefu wa zaidi ya miaka saba katika uwanja huo.

“Nina ujuzi na maarifa ya kusaidia kuinua chapa yako na kuwasilisha ujumbe wako kwa ufanisi. Kama mbunifu mwenye ushirikiano wa hali ya juu, ninaamini kuwa, matokeo bora zaidi yanatokana na kufanya kazi kwa karibu na wateja wangu ili kuelewa mahitaji na malengo yao. Huchukua muda kutafiti kikamilifu na kuelewa biashara yako, hadhira lengwa, na washindani, na kutumia habari hii kufanya maamuzi yangu ya muundo,” asema.

“Ili kuwapa wateja wangu wazo la mtindo na uwezo wangu, wanaweza kutembelea wavuti wangu katika www.jewelfilms.co.ke. Iwe unahitaji muundo mpya wa nembo, uonyeshaji upya chapa, nyenzo za uuzaji, au wavuti za kuvutia, nina uhakika kwamba, ninaweza kutoa miundo ya hali ya juu na yenye ufanisi ambayo itasaidia biashara yako kuwa bora na kufanikiwa,” aongeza.

  • Tags

You can share this post!

Je, wafahamu kwamba mikoko ina matunda? Ila si mikoko yote!

Taka zafunga barabara Murang’a, panya wakionekana waziwazi

T L