• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Hapa kupunjwa tu: Wakulima wanavyolazimishwa kurefusha magunia ya viazi

Hapa kupunjwa tu: Wakulima wanavyolazimishwa kurefusha magunia ya viazi

NA LABAAN SHABAAN

KILIMO Biashara cha viazi kimenoga Kaunti ya Narok hasa eneo la Olorropil sehemu za kaskazini ya kaunti.

Katika msimu wa mavuno, malori mengi yanaonekana kutoka maeneo tofauti nchini kuelekea mashambani kusafirisha viazi masokoni.

Meneja wa shamba moja la ekari 50, Clinton Naranke, anaeleza kuwa katika nyakati za mvua, kila mwezi ni mwezi wa mavuno.

Mpango wa kupanda viazi ulaya katika hatua tofauti za makuzi umekuwa mwokozi kwa wakulima kujihakikishia mavuno tele.

Lakini kuna tatizo kubwa linalowakosesha wakulima usingizi.

Mabroka wanaendelea kukiuka kanuni za vipimo vya ukubwa wa gunia kama ilivyowekwa na serikali.

Magunia ya viazi yanayopakiwa kwenye malori ni makubwa kuliko kiasi.

Utayaona yamechongoka na kuwa marefu.

Hali hii imewapunguzia wakulima faida zao.

Magunia makubwa yaliyopakiwa viazi kinyume cha sheria shambani Narok. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kwa lugha ya soko, wanaita magunia haya ‘bullets’ sababu yalivyo na ncha kama risasi.

“Japo tunafurahia mauzo, haya magunia makubwa yanatuumiza sana,” alisema Naranke.

Anaeleza kuwa ekari moja ya viazi hutoa angalau magunia 90 shamba likisimamiwa vizuri.

Shamba lao la ekari 50 limegawanywa kwa vipande vitatu.

“Kuna wakati bei ya viazi iko chini katika sehemu ya msimu. Hali hii huokolewa na shamba jingine lililo na mavuno wakati bei iko juu,” alikiri Naranke.

Naranke alieleza masaibu wanayopitia mikononi mwa madalali wanaoamua bei ya viazi hadi kufika Sh3,000 kwa gunia.

“Magunia haya yanafaa kuuzwa kwa kati ya Sh6,000 na Sh10,000 ili kurejesha mtaji uliotumika. Lakini mabroka hufyonza sana pesa zetu,” alilalama.

Naranke anafichua kuwa wameajiri makumi ya vibarua katika shughuli za upanzi, upaliliaji na mavuno.

Vile vile tingatinga hutumika kulima na kuandaa shamba.

Clinton Naranke, meneja wa shamba la viazi Olorropil Narok. PICHA | LABAAN SHABAAN

Aghalabu huwa na gharama kubwa nyakati za hali ngumu ya kiuchumi Kenya.

Kwa hivyo madalali kuvimbisha magunia na kununua kwa bei ya chini ni upunjaji mkubwa.

Haya yanafanyika wakati wakulima wanazongwa na gharama ghali ya maisha.

“Ukubwa wa magunia ya viazi tunayouza hutunyima hadi asilimia 30 ya pesa tunayofaa kupokea kwa gunia moja,” alieleza Naranke.

Kwa mujibu wa Huduma ya Utathmini wa Afya ya Mimea nchini (KEPHIS), wakulima hupoteza kati ya asilimia 40 – 30 ya mbegu wanazopanda shambani.

Naranke anataka wizara ya kilimo kusaidia wakulima ili kuhakikisha kanuni za vipimo halisi vya gunia vinafuatwa pamoja na uratibu wa bei sokoni.

  • Tags

You can share this post!

Samidoh: Hizi drama zangu nazipenda sana, zinanipa hamu ya...

Polisi shujaa aliyesombwa na mafuriko akiokoa raia Muthurwa...

T L