Akili Mali

Hili jembe la kisasa ‘Power Tiller’ linarahisisha kazi ya kulima

Na RICHARD MAOSI October 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JEMBE la mpini ndicho kifaa tegemeo kwa maelfu ya wakulima wadogo vijijini katika shughuli za kuandaa mashamba kwa upanzi au kupalilia mimea yao.

Ian Yosi kutoka AgroPro 365 Kubota Power Tiller chini ya mwavuli wa Green Africa Group anasema jembe la kitamaduni linazidi kuwekwa kando kwa sababu ya mabadiliko ya teknolojia na kupisha majembe ya kisasa.

“Power Tiller ni kifaa bunifu cha kilimo kinacholenga wakulima ambao hawana mtaji mkubwa wa kununua au kukodisha matrekta ya kulima au kupalilia mashamba,” anatanguliza afisa huyo.

Jembe hili lilivumbuliwa mahususi kuwafaa wakulima kwa kuwarahisishia kazi ya kulima na kuimarisha hali ya udongo wakati wa utayarishaji mashamba ama upaliliaji mimea.

Aidha, humpunguzia mkulima gharama nyingi ya kuajiri vibarua msimu wa upanzi na kupalilia.

Fauka ya hayo mtambo huu unaweza kuburuta vifaa vingine ambavyo hutumika shambani kama vile kifaa cha kupulizia dawa, kupalilia, kupanda na kuvuna.

Yosi aliambia Akilimali kuwa tofauti na trekta Kubota Power Tiller unaweza kuendeshwa na mtu mmoja ilmradi ana ujuzi wa namna ya kutumia.

Pili, hutumia kiwango kidogo cha mafuta kulima sehemu kubwa ya ardhi, hivyo inawezesha mkulima kuokoa gharama na kuzidisha pato lake.

Mtambo wa power tiller kutoka AgroPro 365 -Kubota Power Tiller chini ya mwavuli wa Green Africa kwenye maonyesho ya Kilimo jijini Nairobi. PICHA|RICHARD MAOSI

Tatu, kifaa hiki kinazuia kwa kiasi mmomonyoko kinyume na jembe la kitamaduni ambalo huchimba kina kirefu na hivyo kulegeza udongo ambao huwa rahisi kubebwa na upepo au maji.

Matokeo yake ni kuhifadhi wadudu muhimu wanaoishi ardhini.

Yosi anasema kwamba ikilinganishwa na gharama ya kumiliki trekta, jembe la Power Tiller mtambo huu ni bei nafuu.

“Iwapo trekta kubwa itatumia lita mbili ya mafuta kulima shamba kwa saa mbili, hii trekta ya mkononi itatumia lita moja kumaliza kazi katika muda sawia,” aeleza.

Isitoshe, matumizi yake yana manufaa ya kiafya kwani humwezesha mkulima kufanyisha viungo vyake vya mwili mazoezi anaposukuma na kuelekeza kutoka sehemu moja ya shamba hadi lingine.

Kifaa hiki kimeundwa kwa namna ya kipekee kuhimilli mazingira magumu , ina uwezo wa kuvunja udongo ili kutengeneza matuta sahihi kwa ajili ya kupanda, kupalilia na hata kurutubisha shamba.

Hutumika kwa urahisi sio tu katika maeneo tambarare bali pia kuliko na miinuko na vilima, kinyume na trekta za kawaida ambazo hutatizika kufanya kazi maeneo ya bonde na milima.

Mwisho, jembe hili linahitaji gharama ndogo ya utunzi kwa sababu mahitaji yake sio mengi.