Jamii yahifadhi Msitu wa Eburu kupitia ufugaji wa nyuki
MSITU wa Eburu, unaojumuisha mfumo mkuu wa Misitu wa Mau katika eneo la kati mwa Bonde la Ufa nchini, ni sehemu muhimu ya kiikolojia.
Msitu huu ambao mwanzoni ulijulikana kama mojawapo ya “minara ya maji” ya Kenya, huchangia pakubwa katika maeneo yanayokusanya maji ya Maziwa Naivasha na Elementaita.
Hata hivyo, katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, mfumo huu wa ikolojia umekuwa ukiharibika kwa kasi.
Ukataji haramu wa miti, uchomaji mkaa na kilimo haribifu vimesababisha mmomonyoko wa udongo na kupungua kwa BIOANUWAI, hali ambayo ilisababisha mazao kupungua mashambani mwa jamii zinazoishi hapa.
Lakini katika kipindi cha hivi majuzi, kumekuwa na mabadiliko ambayo yamekuwa yakishuhudiwa hapa, yakiongozwa na jamii ya wenyeji wa kijiji cha Ndabibi. Siri yao ni nini? Nyuki.
Bi Magdalene Wanjiku, ambaye kwa muda mrefu amekuwa mkulima katika eneo hili, anakumbuka changamoto za zamani:
“Nilikuwa nalima mahindi na maharagwe, lakini ilifika wakati ambapo shamba langu halikuwa na tija tena. Nilikuwa napata mavuno kidogo sana,” asema.
Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika baada ya kuanzishwa mradi wa ufugaji wa nyuki.
“Sasa tuna nyuki, wanazunguka katika mashamba na miti ya matunda, na tunapata mavuno mazuri tena,” anaongeza.
Katika sehemu hii, nyuki hawazalishi tu asali; wao ni wachavushaji wa kutegemewa. Wameongeza uzalishaji wa mazao na kusaidia kurudisha uhai katika mifumo ya ikolojia ya eneo hilo.
Mabadiliko ya uhusiano kati ya wanakijiji wa Ndabibi na Msitu wa Eburu yanahusishwa pakubwa na chama cha ushirika cha Hifadhi Farmers Cooperative, kilichoanzishwa mwaka wa 2014 chini ya uongozi wa Bw Francis Njogu Mbutu.

Kabla ya kuanzishwa, juhudi za jamii hii katika masuala ya kilimo, zilikuwa zinagonga mwamba, huku shughuli za ukataji haramu wa miti na uchomaji mkaa zikiwa zimekithiri.
“Msitu wetu ulikuwa umeharibiwa sana,” anakumbuka Bw Mbutu.
“Watu walikuwa wanatoka hata katika sehemu za mbali kama vile Kinangop kuja kuchoma mkaa. Hakukuwa na hisia ya umiliki.”
Kuundwa kwa chama cha kijamii cha msitu (CFA) mwaka 2012, kuambatana na Sheria ya Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu ya Kenya, ilikuwa hatua ya kwanza.
“Ni hatua iliyotuletea muundo na kutupa motisha wa kujiendeleza kiuchumi,”aeleza Bw Mbutu.
Walipoanza walikuwa na mizinga 50 ya muundo wa kale, lakini kwa sasa, chama hicho kinasimamia zaidi ya mizinga ya kisasa 700.
Kupitia ushirikiano na mashirika kama vile Kituo cha FAO cha misitu na kilimo (FFF), wakulima wanachama walipokea mafunzo ya ufugaji wa nyuki, usimamizi bora wa rasilimali, na uongezeaji thamani.
Mbali na kuvuna asali, pia wakulima wa kijiji hiki walifundishwa jinsi ya kutengeneza mafuta kutokana na nta ya nyuki.
“Sasa mimi huuza mafuta hayo katika soko la karibu kwa bei ya kati ya Sh50 hadi Sh150, na hivyo kuongeza kipato changu,” aeleza Bi Wanjiku.
“Hapo awali, mkulima angelima ekari tano za mahindi kwa faida ndogo. Kwa upande wangu sasa kwa mizinga mitano tu, naweza kupata zaidi ya Sh100,000 kwa mwaka. Siwezi kamwe kulinganisha na pesa ambazo nilikuwa napata kutokana na kilimo cha mahindi, ambapo ningeweza kupata labda Sh30,000 kwa ekari moja—na kwa kazi nyingi zaidi.”
Kutokana na kuwa ufugaji nyuki ni rahisi na hauhitaji kazi nyingi, wakulima wengi kijijini humu wamevutiwa na shughuli, na faida ambazo wamekuwa wakishuhudia, zimebadilisha mtazamo wao kuhusiana na uhifadhi wa msitu huu.
“Tumejifunza kuwa msitu ni rafiki yetu. Tunauhifadhi kwa sababu nyuki wanategemea msitu huu,” aeleza Bw Mbutu.
Chama hiki pia kimeanza kuhusisha kizazi kipya katika shughuli hii, na hivyo kusaidia kuziba mapengo yanayotokana na ukosefu wa ajira.
Kwa mujibu mhasibu wa chama hiki, Bw Stephen Kamau, Hifadhi Cooperative sasa ina wanachama 561, wakiwemo vijana 144.
“Tumehakikisha kuwa vijana wanachukua kati ya asilimia 25 na 30 za nafasi za mafunzo. Hii ni kwa sababu kikundi hiki kinaongoza katika masuala ya masoko, matumizi ya mitandao ya kijamii, na hata matangazo yanayotumia akili unde (AI),” asema.
Mabadiliko ya kidijitali yamewezesha wanakijiji hawa kufikia masoko mapana. Mwaka wa 2024 pekee, kikundi hiki kilivuna tani 2.3 za asali, na kupata mapato ya jumla ya takriban Sh1.9 milioni.
“Asilimia 30 ya pesa hizo, husalia kwenye ushirika ambapo hutumika katika uendeshaji wa shughuli zake, huku kiasi kilichobaki kikielekezewa wakulima,” aeleza Bw Kamau.
Lakini kando na faida za bidhaa zinazotokana na ufugaji nyuki, manufaa mengi yameshuhudiwa katika mazingira ya msitu huu.
Msitu huu unarejelea hali yake ya awali kwani wanakijiji sasa wamekomesha tabia ya ukataji miti na shughuli zingine zinazosababisha uharibifu wa misitu.
“Shughuli za uchomaji makaa sasa hazikubaliki, ukataji miti haramu umepungua kwa kiasi kikubwa, na miti ya asili inarejea polepole,” asema Bw Mbutu.
Ili kuimarisha urejesho huo, ushirika huu umeanzisha mpango wa upandaji miti, ikiwa ni pamoja na kuanzisha kitalu cha miche ya miti ya asili na ya matunda.

Kwa mujibu wa Bw Philip Kisoyan, mtaalamu wa ikolojia ya mandhari na mkuu wa mradi wa usimamizi wa rasilimali asilia katika shirika la FAO, ufugaji wa nyuki ni muhimu sana katika uhifadhi wa mazingira.
“Uzuri wa ufugaji nyuki katika uhifadhi wa misitu ni kuwa huleta ulinzi wa mfumo mzima wa ikolojia, na wala sio katika spishi moja au mti mmoja tu. Nyuki ni kiungo muhimu katika shughuli za uchavushaji, na hivyo wanasaidia kuendeleza uzazi wa spishi nyingi za mimea, zikiwemo zile muhimu kwa afya ya misitu.”
Bw Kisoyan aongeza kuwa uchavushaji ni muhimu sio tu kwa kuongeza mavuno ya kilimo, bali pia kwa kudumisha misitu yenye afya, kuhifadhi bioanuwai, na kuhakikisha uendelevu wa mifumo ya ikolojia kwa ujumla.
Anatoa wito kwa ufugaji wa nyuki kuunganishwa na sera za uhifadhi wa misitu, kama mbinu ya kuimarisha maisha endelevu.
Kwa upande mwingine, mafanikio ya kijiji cha Ndabibi yamevutia mashirika ya kimataifa.
Kupitia mpango wa FFF-DBG (Direct Beneficiary Grant) kutoka kwa FAO, ushirika huu ulipokea msaada wa kifedha kwa mafunzo na maendeleo ya miundombinu.
Mwaka wa 2024 na 2025, ushirika ulitumia ruzuku hizo kutekeleza miradi mipya, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vitalu vya miti, na kupanga ziara za mafunzo katika mashirika mengine ya ufugaji wa nyuki nchini.
“Ziara hizi zililenga kubadilishana maarifa, kujifunza kuhusu mbinu bunifu za usindikaji, na kupanua masoko ya ushirika,” aeleza Bw Mbutu.
Sasa kuna mipango ya kupanua masoko kwa kuanzisha maduka ya asali yenye chapa maalum katika miji kama Nairobi, na kutengeneza bidhaa zingine kama mishumaa ya nta na marashi.
Ushirika huu pia unalenga kuwa kituo cha mafunzo kwa jamii zingine zinazozunguka misitu kote nchini Kenya na hata mbali.