Akili Mali

Jinsi biashara ya kuongeza thamani nazi inavyomfaidi

Na PETER CHANGTOEK December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kupoteza kazi wakati wa vurugu vya baada ya uchaguzi 2007/2008, Cosmas Mole aliwaza na kuwazua kuhusu jinsi ya kujiruzuku, na akaamua kujitosa katika shughuli ya kuongeza thamani kwa nazi. 
Mole alianzisha shughuli hiyo baada ya kupata mafunzo kutoka kwa asasi mbalimbali za mafunzo. Aliutumia mtaji wa Sh4,500 alizokopa kutoka kwa chama ambacho mkewe alikuwa mwanachama.
Yeye huendesha kampuni yake inayojulikana kama Cocoa Poa Ventures, inayotengeneza bidhaa za nazi katika eneo la Makomboani, Kaloleni, Kaunti ya Kilifi.
“Wazo la kuanzisha shughuli hii lilinijia akilini baada ya kufutwa kazi baada ya vita vya 2007/2008, ambapo nilikuwa nikihudumu katika hoteli,” aeleza.
Kampuni hiyo huajiri watu zaidi ya 35 wa kike na vijana 17 kuanzia shambani hadi wakati ambapo bidhaa zinauzwa sokoni.
“Safari yangu katika kampuni ya Coco Poa Ventures ilianza mwaka 2013, chini ya mti. Nimekuwa na ushirikiano mwema na asasi ya Nuts and Oil Crops Directorate (NOCD),” asema Mole, akiongeza kwamba asasi ya NOCD ilimsaidia kupata mafunzo ya ziada katika asasi nyinginezo za mafunzo.
Mfanyakazi akuna nazi katika eneo la Kaloleni, Kilifi. PICHA|PETER CHANGTOEK
Anafichua kuwa, alianza kwa  kutengeneza bidhaa zilizoidhinishwa na Shirika la Kukagua Ubora wa Bidhaa, Kenya (KEBS), Aprili 2013, kupitia usaidizi wa Kenya Coconut Development Authority (KCDA).
Bidhaa hizo zilikuwa zikijulikana kwa jina Uzima, kwa wakati huo.
“Mnamo Agosti na Septemba 2013, KCDA walinialika kwa mara ya kwanza kuonesha bidhaa zangu katika maonyesho ya kilimo ya Mombasa na Nairobi.
Katika maonyesho hayo, bidhaa zangu zilipata fursa ya kujulikana kwa wateja wa hapa nchini na nje ya nchi,” asimulia, akiongeza kuwa, bidhaa zake zilianza kuhitajika mno, kiasi kwamba alishindwa kuwatosheleza wateja wake sokoni.
“Biashara hiyo ilianza kujisimamia hadi 2015, ambapo KCDA  iliniunganisha na wawekezaji nchini ili wanisaidie kuikuza biashara hiyo. Tulianzisha ushirikiano wa biashara, lakini ushirikiano huo haukudumu kwa muda mrefu,” asema.
Nazi iliyokunwa katika eneo la Kaloleni, Kilifi. PICHA|PETER CHANGTOEK
Mjasiriamali huyo anadokeza kwamba, wanalenga kuibuka bora katika shughuli ya utengenezaji wa mafuta ya nazi, kwa kuelewa matakwa ya wateja na kutengeneza bidhaa zenye thamani.
Anaongeza kuwa, azma yao ni kuhakikisha kwamba wanajitolea kuboresha maisha ya jamii zinazojishughulisha na ukuzaji wa minazi, kwa kupunguza gharama ya uzalishaji, kupunguza hasara inayotokea baada ya kuvunwa kwa mavuno kwa kutoa soko la nazi, na hivyo kutoa ajira kwa vijana.
Mjasiriamali huyo anasema kuwa, uongezaji thamani kwa nazi una faida ikilinganishwa na uuzaji wa mazao ya nazi ambayo hayajachakatwa. Anaongeza kwamba, amewahamasisha wakulima zaidi ya 500 ili wawe wakimwuzia mazao yao ya nazi, ambayo huchakata ili kupata mafuta.