Jinsi utumiaji wa teknolojia umesaidia kuletea Kenchic ufanisi
SEKTA ya kuku nchini Kenya inaendelea kupitia mageuzi makubwa kutokana na uwekezaji katika teknolojia za kisasa zinazoboresha utoshelevu wa chakula, ustawi wa wanyama na ufanisi wa uzalishaji.
Hii inatokana na ari ya Wakenya kwa nyama nyeupe na bidhaa zake, wakiwa makini kwa maradhi yanayosababishwa na lishe.
Wazalishaji wa kuku na bidhaa zake kama vile Kenchic, wamegeukia mifumo ya kiotomatiki ili kukidhi mahitaji yanayozidi kuongezeka, na wakati huohuo kudumisha viwango vya kimataifa vya usalama wa chakula.
Utafiti wa 2022 wa Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo (FAO), unaonyesha kuwa asilimia 92.6 ya Wakenya hupendelea kula nyama ya kuku mara kwa mara.
Miongo ijayo, shirika hilo aidha linahoji matumizi ya nyama na mayai ya kuku yanatarajiwa kuongezeka maradufu – hilo likichochewa na ukuaji wa mijini, mapato ya juu na mabadiliko ya lishe.
FAO inakadiria ongezeko la asilimia 289 kwa ulaji wa nyama ya kuku na asilimia 211 mayai, ifikapo mwaka 2050.
Kwa kampuni za uchakataji, changamoto kuu si tu uzalishaji, bali kutekeleza hilo kwa kudumisha usafi, ufuatiliaji wa bidhaa na ustawi wa wanyama.
Kenchic Ltd, inayochakata kuku na bidhaa zake kwa minajili ya soko la Kenya na Afrika Mashariki, teknolojia imekuwa nguzo ya shughuli zote—kuanzia ufugaji hadi uchinjaji, uongezaji thamani na upakiaji.
Kwenye kiwanda chake cha kisasa kilichoko pembezoni mwa barabara ya Kilimambogo, Thika, Kaunti ya Kiambu kila hatua ya uchakataji inafanywa kwa usahihi wa kisayansi.
Kulingana na Alun Maskell Mkuu wa Oparesheni za Kiwanda na Uchinjaji, hatua ya kuhamia teknolojia za kisasa na kidijitali kuendesha huduma, umewezesha kampuni hiyo ya kuku kutimiza viwango vya usalama wa chakula vya kitaifa na kimataifa.
Anasema Kenchic inajikakamua kuboresha utendakazi wake, huku Sheria ya Udhibiti wa Usalama wa Chakula na Lishe ya Kenya 2023 ikiwa katika hatua za lala salama kuidhinishwa.
“Tunashirikiana na wakulima – wafugaji ambao wanatilia mkazo kanuni za ufugaji, usalama na ufuatiliaji wa bidhaa kuanzia yai hadi kuku wanapotua kwenye sahani,” Maskell, mwenye shahada ya Sayansi ya Nyama na utaalamu wa juu katika teknolojia za uchakataji wa kuku anasema.
Kampuni hiyo, kando na kuwekeza pakubwa kwenye usindikaji, inaangua mayai kuwa vifaranga na kulea kuku.
Husambaza vifaranga waliochanjwa kwa wakulima nchini.
Maskell anaeleza kuwa ubora huanza mashambani, ambako wakulima walioandikisha kandarasi na Kenchic hufuata sheria kali za usalama wa kuku na ufuatiliaji.
Aidha, kuku husafirishwa mapema asubuhi kwenye kreti zinazoingiza hewa na udhibiti wa joto.
Hupitia viwango kadhaa; kuchinja, utoaji wa viungo vya ndani – tumboni, bidhaa za kuku kuwekwa kwenye vyumba vyenye baridi na barafu, uchakataji na upakiaji.
Katika kichinjio cha Kenchic cha Halal, kituo cha uchinjaji ni ya kiotomatiki chenye mwangaza wa buluu unaotuliza kuku na kupunguza msongo wa mawazo.
“Mwanga wa buluu, kuku wanapotulia unasaidia kuboresha rangi ya nyama, muonekano na thamani yake,” Maskell akaambia Akilimali wakati wa mahojiano kwenye kiwanda cha Kenchic.
Mashine za kutoa manyoya hufanya kazi kwa kasi ya kuku 78 kwa kila dakika. Baadaye, kinachofuata ni kuondoa viungo vya ndani kupitia mfumo maalum.
Aidha, vinatenganishwa kati ya vinavyotumika na visivyotumika, Maskell akisisitiza kuwa asilimia kubwa inaongezwa thamani.
Kisha nyama husafishwa na kupelekwa kwa mitambo ya kushusha joto hadi chini ya nyuzi 5°C ili kuzuia ukuaji wa bakteria.
“Baadaye, nyama huwekwa usiku kucha kwenye vyumba maalum vya baridi kabla ya kuingia kwenye sehemu ya kukata na kuondoa mifupa,” Maskell anaelezea. Ipo mashine ya kiotomatiki kuondoa mifupa.
Vipande kama mabawa, mapaja na sehemu zisizo na mifupa ndio viungo vinavyoingizia Kenchic hela, huku mabaki yake yakitumika kuunda sausage na nuggets.
Bidhaa zingine za kuku hugandishwa hadi nyuzi joto –18°C ili kudumisha ubora, kisha zinahifadhiwa kwenye vyumba vya nyuzi joto –12°C kabla ya kusambazwa sokoni.
Maskell anasisitiza kwamba suala la nyuzi joto kwenye uhifadhi ni muhimu.
“Bidhaa hairuhusiwi kukaa nje ya baridi kwa zaidi ya dakika 20”.
Lori na matrela ya usafirishaji, Kenchic huhakikisha yana nyuzi joto kati ya 2°C na 3°C, lengo, akisema, ni kuhakikisha kila bidhaa ya kuku inafika kwa mlaji ikiwa salama, tamu na yenye ladha bora.
Aidha, anafichua kuwa Kenchic huuza asilimia 95 ya bidhaa zake kwenye masoko ya ndani kwa ndani Kenya.