Akili Mali

Kilimo cha mwani kinavyobadilisha maisha ya wanawake pwani ya Afrika Mashariki

Na PAULINE ONGAJI July 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MITA chache kwenye ufukwe wa eneo la Paje katika kisiwa cha Zanzibar, wanawake kadhaa wamekaa majini wakisuka kamba na kufunga mwani kwenye fimbo zilizozamishwa.

Miongoni mwao ni Bi Pili Halili, ambaye amekuwa akijihusisha na kilimo cha mwani tangu mwaka 2005. Leo, yeye ni mmoja wa wanawake kumi wanaofanya kazi katika kampuni ya Mwani Zanzibar Ltd, inayojihusisha na uzalishaji, uchakataji, na usafirishaji wa mwani.

“Awali kilimo cha mwani hakikuwa na faida,” Pili akumbuka.

“Nililazimika kuacha shughuli hii kwa muda kwa sababu bei ya mazao haya kwa kilo ilikuwa ndogo sana — takriban Sh700 za Tanzania (chini ya Sh30 za Kenya).”

Lakini miaka kadhaa baadaye, alirejea katika shughuli hiyo lakini kupitia mradi wa kikundi cha wanawake wakulima wa mwani walioshirikiana na kuunganisha rasilimali zao.

Mwenyekiti wa Shangani Amani Self Help Group Bakari Ali kutoka Nyumba Sita, Msambweni, Kwale kwenye ‘shamba’ lao la mwani. Anasema wamenufaika na kilimo hicho tangu 2011. Picha|Wachira Mwangi

“Sasa, sijuti kwani kupitia kilimo cha mwani, sasa naweza kusomesha watoto wangu na kutunza familia yangu,” aeleza Bi Pili

Hapa nchini, katika Kaunti ya Kwale, eneo la pwani, wanawake kama Bi Mwanasiti Athumani na Bi Mwanasiti Ali Juba, wamejitosa vilivyo katika shughuli ya kilimo cha mwani.

Wakazi hawa wa eneo la Msambweni, walianza kujihusisha na kilimo hiki mwaka 2011. Kufikia mwaka 2018, kupitia kikundi cha Shangani Amani, waliunda ushirika uliowawezesha kuimarisha shughuli yao, na hivyo, kujiimarisha kibiashara.

“Tulianza kuuza mwani kwa Sh19 kwa kilo,” Bi Athumani anasema. “Sasa tunauza kwa Sh50, ambapo tunaweza kuvuna hadi tani kumi kwa wakati mmoja.”

Kwenye Kongamano la Tatu la Umoja wa Mataifa kuhusu Bahari (UNOC3) liliofanyika jijini Nice, Ufaransa, kilimo cha mwani na mimea mingine ya baharini, kilijadiliwa kama mojawapo ya shughuli za kibiashara ambazo zinaweza kutumika kuimarisha uchumi wa jamii zinazoishi pwani.

Katika jopo la ngazi ya juu lililoongozwa na Waziri wa Uchumi wa Baharini na Uvuvi wa Zanzibar, Bw Shaaban Ali Othman, wataalam walijumuisha kilimo cha mwani, pamoja na uvuvi baharini, kama nguzo kuu ya kupambana na njaa na umaskini.

“Mwani sio tu bidhaa ya kuuza nje. Ni sehemu muhimu ya kuimarisha lishe na kipato, hasa kwa wanawake,” alisema Bi Shakuntala Haraksingh Thilsted kutoka mtandao wa kimataifa wa taasisi za utafiti wa kilimo CGIAR.

Kulingana na Dkt Flower Msuya, mtafiti wa mwani katika mpango wa Zanzibar Seaweed Cluster Initiative, kati ya watu 15,000 na 20,000 — wengi wao wakiwa wanawake — wanajihusisha na kilimo zao hili katika kisiwa hiki.

“Kisiwa cha Unguja huchangia takriban asilimia 25 ya uzalishaji wa mwani, huku kile cha Pemba kikitoa asilimia 75 iliyobaki,” asema Dkt Msuya, huku akiongeza kwamba licha ya haya, sekta hii haipokei msaada wa kutosha.

Katika kongamano la UNOC3 wataalam walisisitiza umuhimu wa mazao na vyakula vya baharini kujumuishwa katika sera zinazoangazia utoshelevu wa vyakula.

“Nchi zinaweza kufaidika pakubwa iwapo mifumo ya vyakula vya baharini itajumuishwa katika ajenda zetu za maendeleo,” alisema Bw Jim Leape kutoka Chuo Kikuu cha Stanford, nchini Amerika.

Lakini sekta hii, hasa katika eneo la Afrika Mashariki, bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Wakulima wa mwani kama Bi Pili Halili na Bi Mwanasiti Athumani, wanaendelea kukumbwa na changamoto kama vile kazi ngumu inayohusika katika ukulima wa zao hili, vile vile mabadiliko ya tabianchi.

“Joto la bahari linapoongezeka na mawimbi kuwa makali zaidi, mwani huchukua muda kukua, na wakati mwingine mashamba yote huoshwa na maji,” asema Bi Norah Magangi kutoka Taasisi ya utafiti wa bahari na uvuvi ya Kenya (KEMFRI)

Nchini Kenya, Bi Magangi, aongeza kuwa matatizo ya kimfumo yameathiri mazingira. Pia, aeleza kuwa hakuna sera za kuwalinda wakulima, miundombinu ni duni, huku madalali wakiendelea kuwakandamiza wakulima.

Kina mama wakichambua mwani (seaweed) katika eneo la Msambweni, Kwale. Picha|Wachira Mwangi

“Hakuna sera za kuwalinda wakulima. Wanunuzi huweka bei, na madalali ndio wanaofaidi zaidi. Hii huwafanya wakulima halisi kuteseka,” asema.

Lakini bado kuna matumaini, huku wataalamu wakisisitiza haja ya sekta hii katika eneo la Afrika Mashariki, kuiga mfano wa nchi za Asia na kuwekeza katika teknolojia, masoko, na mbinu za kilimo zinazokabiliana na hali ya hewa.

“Kwa mfano, nchini Japani, mifumo ya kiotomatiki na mbinu zilizotafitiwa zinahakikisha mavuno thabiti, licha ya changamoto za kimazingira,” asema Bw Mirko Dunner wa UNCTAD. “Afrika Mashariki inaweza kufanya hivyo pia.”

Tayari kuna baadhi ya wakulima ambao wameanza kujaribu. Katika kisiwa cha Zanzibar, Bi Halili na wengine wanaboresha mbinu za kukausha mwani. Nchini Kenya, Bi Athumani na kikundi chake wanafanya jitihada za kupata mashine ya kusaga mwani kuwa unga wa kuunda vipodozi, na kuuza nje.

“Tumeanza kutengeneza losheni na sabuni, na sasa tunalenga kupanua biashara,” asema Bi Athumani.