Akili Mali

Kilimo kinavyobadilisha sifa za Nyalenda iliyofahamika kwa ghasia za maandamano

Na FRIDAH OKACHI September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

HATUA chache kutoka katikati mwa jiji la Kisumu, katika mtaa wa Nyalenda, wenye msongamano na shughuli nyingi, mambo kadha kuhusiana na shughuli za kilimo yanaendelea.

Katika mtaa huo uliojaa vibanda vya kuuza samaki, kundi la vijana linabadili sura ya mabanda ya mjini si kwa maandamano au sera, bali kupitia ufugaji wa kuku, uzalishaji wa mbolea na mboga aina mbalimbali.

Mtaa wa Nyalenda uliokuwa ukitambulika kwa taka zisizokusanywa, ukosefu wa ajira kwa vijana, na tishio linaloongezeka la mabadiliko ya tabianchi, sasa ni nyumbani kwa kizazi kipya cha wajasiriamali wa kilimo.

Kupitia mradi wa Kisumu Young Agropreneurs (KIYA), vijana hawa wanabadilisha taka kuwa mbolea yenye rutuba, kupanda mboga, kufuga wanyama na kuwafundisha wengine kufanya vivyo hivyo.

Dhamira yao ikiwa ni kuthibitisha kwamba hata katikati ya makazi duni ya mabanda, kilimo kinaweza kukuza mustakabali wa maisha.

Badhi ya mboga zinazokuzwa katika shamba la Lilian Chepngetich kwenye kitongoji duni cha Nyalenda, Kisumu. Picha|Fridah Okachi

Bi Lilian Chepng’etich hakuwahi kufikiria maisha yake yangelibadilishwa na shughuli za kufuga kuku na kupanda mboga. Alipoona wenzake wakinufaika kupitia mradi wa KIYA, aliamua kujaribu.

“Niliona marafiki zangu wakinufaika na KIYA, nami nikaamua kujiunga. Nilifundishwa, nikapata mlezi, na sasa mimi ndiye mkufunzi wa wakufunzi , ninafanya kazi na asilimia 70 ya wanawake. KIYA imenifungulia milango,” anasema Chepng’etich.

Leo hii, Bi Chepng’etich si mkulima pekee. Ni kielelezo cha kuigwa, mkufunzi wa jamii, na mtetezi wa kilimo endelevu.

Msaada wake mkubwa ukitokana na Wakfu wa Mastercard, kwa kumjengea banda la kuku linalohifadhi kuku 200.

Shamba lake, ambalo sasa linastawi kwa nyanya, sukuma wiki, mihogo na kuku, linapata soko la moja kwa moja kupitia mtandao wa KIYA.

“Kupata masoko ya mazao yangu kimekuwa rahisi zaidi,” anaongeza.

Amejitosa pia kwenye ufugaji wa nzi wa Black Soldier (BSF), mbinu bunifu na rafiki kwa mazingira ya kilimo endelevu na usimamizi wa taka.

Safari yake inaonyesha mabadiliko ya jamii yake: kutoka ukosefu wa chakula na ajira hadi tija na fahari.

KIYA imewafundisha zaidi ya vijana 3,000 wenye umri kati ya miaka 18–35 katika kilimo na mifumo ya chakula.

Kati ya waliopata mafunzo, vijana 2,600 wameanzisha biashara zao za kilimo kwa mafanikio.

Kiongozi wa kundi la KIYA, Bw Stephen Onyango anaeleza kuwa kabla ya mradi huo kuanza vijana wengi walikuwa wakijihusisha na uhalifu kwenye mtaa huo.

“Kabla ya mradi kuanza, si vijana wengi waliokuwa kwenye kilimo, lakini sasa tumewaona wengi zaidi wakijiunga,” anafafanua Bw Onyango.

“Tumeweza kutoa mafunzo kwa vijana 3,000 na 2,300 wameanzisha biashara zao za kilimo. Asilimia 60 wameongeza kipato chao na wameunda ajira kwa wengine katika jamii,” anaongeza Bw Onyango.

Imebainika kuwa hatua hiyo inachangia kupunguza uagizaji wa chakula katika Kaunti ya Kisumu kutoka maeneoo mengine.

Mabadiliko haya yanahusishwa zaidi na KIYA na mkakati wake unaolenga vijana. Ingawa vijana wengi hawamiliki ardhi, KIYA huwasaidia kukodisha maeneo ya kulima, huwapa mafunzo, ulezi, na upatikanaji wa masoko.

Mradi huo unaelenga kusaidia vijana zaidi kwa uwekezaji wa Sh50 milioni kupitia benki za ndani.

Mradi huu kulingana na vijana walioshirikishwa, umekuwa taa ya matumaini, ukionyesha kwamba wanaweza kuwa nguvu kuu ya kuhakikisha chakula toshelevu na mageuzi ya kiuchumi.

Wakati wengi wakiona maganda yaliyotupwa, mboga zilizooza na kutupwa kwenye mapipa, wanachama wa KIYA huona dhahabu.

Kundi hili hukusanya taka za kikaboni kutoka soko kuu la Kibuye na kugeuza kuwa mbolea.

Kila wiki, hukusanya maganda ya matunda na mboga kisha kuyazika chini ya udongo na majani. Baada ya muda, huyageuza kuwa mbolea yenye virutubisho inayofufua udongo ulioisha virutubishi.

Lakini KIYA hawakuishia hapo. Waligundua nguvu ya nzi wa Black Soldier (BSF), mdudu ambaye viwavi wake hula taka za kikaboni kwa wingi.

BSF hutaga mayai, ambayo hukusanywa na kutunzwa hadi wafikie kuwa viwavi.

Viwavi hula taka, na mabaki wanayoacha huwa mbolea yenye rutuba, huku wao wenyewe wakigeuka chakula chenye protini kwa kuku, samaki na nguruwe.

“Ufugaji wa BSF ni mageuzi makubwa. Sio tu usimamizi wa taka; ni kuunda uchumi unaoendelea kunawiri,” anasema Bw Onyango.

Kulingana na Bw Roy Odawa, mmoja wa washirika kwenye kundi la KIYA, anasema kuziba pengo la elimu ya awali ya kilimo, KIYA imepanua huduma zake hadi kwenye shule za umma.

Januari 2025, mradi huu kwa msaada wa African Population and Health Research Center (APHRC) ulizinduliwa katika shule nane za msingi za umma Nyalenda.

“Tuligundua tuna watoto wengi mabandani ambao hawaelewi kilimo,” anasema Bw Odawa.

“Mashamba haya ya shule yatatumika kama sehemu ya mafunzo na pia chanzo cha chakula,” anadokeza Bw Odawa.

Afisa katika Serikali ya Kaunti ya Kisumu, Bw Daniel Owino anasema kuwa mradi huo unawahusisha walimu ambao pia wanahakikisha wanafunzi wanapata elimu ya kilimo bora.

“Tumewashirikisha walimu. Tumefundisha shule nane za msingi katika zaidi ya masuala matano ya thamani: mboga za kienyeji za Kiafrika, kuku, nyanya, mihogo, ufugaji samaki, na hatua dhidi ya tabianchi kama ufugaji wa BSF,” anaeleza.
Juhudi za KIYA zimefaulishwa na ushirikiano na GIZ ya Ujerumani.