KRA yaongeza siku 5 kwa waliochelewa kuwasilisha ushuru wa 2024
MAMLAKA ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) imewapa afueni walipa ushuru kwa kuongeza muda wa kuwasilisha taarifa za ulipaji ushuru za mwaka jana kwa siku tano.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Julai 1, 2025, KRA ilitangaza msamaha wa adhabu na riba kwa waliochelewa kuwasilisha taarifa za ushuru, na kuongeza muda wa mwisho hadi Julai 5, 2025.
Hatua hii ilijiri baada ya maelfu ya Wakenya kukumbana na matatizo ya kuingia kwenye jukwaa la iTax mnamo Juni 30, 2025, tarehe ya mwisho ya kuwasilisha taarifa zao ushuru.
Jukwaa hilo lilikwama kutokana na ongezeko kubwa la watumiaji, hali iliyopelekea wengi kushindwa kuwasilisha taarifa au kufanya malipo kwa wakati.KRA ilitambua hali hiyo na ikajibu kwa kutumia kifungu cha 89(5A)(b) cha Sheria ya Taratibu za Ushuru ili kutoa afueni.
“Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) inawashukuru kwa dhati walipa ushuru wote kwa kujitokeza kwa wingi kuwasilisha taarifa za ushuru wa mapato kwa kipindi kilichoishia Desemba 31, 2024,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
“Kutokana na idadi kubwa ya walipa ushuru waliokuwa wakijaribu kuwasilisha taarifa zao Juni 30, 2025, mfumo ulipata matatizo ya kiufundi yaliyosababisha hitilafu katika utoaji wa huduma za kuwasilisha taarifa na malipo, hivyo kuzuia baadhi ya walipa ushuru kuwasilisha kwa wakati.”
Ili kuhakikisha haki kwa wote, KRA ilithibitisha kuwa walipa ushuru sasa watakuwa na hadi Ijumaa, Julai 5, 2025, kuwasilisha taarifa na kulipa ushuru wanaodaiwa bila kutozwa faini au riba.
“Kutokana na wingi wa walipa ushuru msamaha wa adhabu na riba umetolewa. Tarehe mpya ya mwisho ya kuwasilisha marejesho na kulipa ushuru wowote unaodaiwa ni Julai 5, 2025,” iliongeza taarifa hiyo.
KRA ilihimiza Wakenya kutumia fursa hiyo ya muda wa ziada na kuhakikisha wanawasilisha taarifa zao za ushuru.
“Wakenya wanashauriwa kuwasilisha taarifa zao zote na kulipa ushuru wowote wanaodaiwa kabla ya tarehe iliyowekwa kumalizika.”