Maparachichi ya Kenya na mafuta yake yanavyoteka soko ng’ambo
MAPARACHICHI ni mojawapo ya jamii za matunda yanayopigiwa upatu kukuzwa kwa sababu ya soko lake lenye ushindani mkuu.
Ni matunda yenye thamani si tu kifedha, bali pia kisiha kutokana na tija zake anuwai kiafya.
Miaka ya nyuma, matunda haya maarufu kama avokado, yalikuwa yakikuzwa na wakulima katika mashamba madogo; soko lake likiwa ni la ndani kwa ndani humu nchini.
Kwa sababu ya faida zake kimapato na kiafya, baadhi ya kampuni na mashirika yanayotoa huduma za kilimo sasa yameingilia ukuzaji wake.
Kampuni nyingine zimeandikisha kandarasi na wakulima ambapo huyakusanya matunda na kuyatafutia masoko ng’ambo.
Avodemia Ltd ni kati ya kampuni na mashirika yanayoshiriki mtandao wa maparachichi. Ikiwa na makao yake makuu katika eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu, inahudumu na wakulima wapatao 4,050.
“Tuna wakulima kutoka Kiambu, Murang’a, Kirinyaga, Embu, Nyeri na baadhi ya kaunti za Bonde la Ufa,” anasema Dennis Wachira, afisa wa mauzo katika kampuni hiyo. Idadi kubwa ya wakulima ni wanaokuza avokado aina ya Hass – spishi iliyoboreshwa. Vilevile, wapo wanaolima Fuerte.
“Hatubagui wakulima; awe ni mwenye kipande kidogo cha shamba au kikubwa, muradi tu wanatusambazia matunda bora nay a hadhi,” Bw Wachira anaelezea.
Kulingana na data za Halmashauri ya Kilimo na Chakula Nchini (AFA), kiwango cha mashamba kinachotumiwa kukuzia maparachichi kimeongezeka kutoka Hekta 26,561 (2021) hadi Hekta 27,807 mwaka wa 2022.
Hali kadhalika, kiwango cha uzalishaji kimepanda kutoka Tani Metri (MT) 432, 969 mwaka 2021 hadi 455,279 MT (2022), hilo likiashiria ongezeko la asilimia 5.2.
Takwimu za AFA pia zinaonyesha kuwa katika mwaka wa 2022, wakulima walitia kibindoni Sh12.6 bilioni, ikilinganishwa na Sh12.4 bilioni mnamo 2021.
Ingawa mataifa ya Bara Ulaya, China, na Milki za Kiarabu (UAE) ndiyo wanunuzi wakuu wa avokado za Kenya, Bw Wachira anasema Avodemia Ltd mwaka huu wa 2024 ilifanikiwa kupenyeza mazao katika soko jipya la India.
“Tunaendelea kunogesha soko la Bara Ulaya na China”. Spishi ya Hass ndiyo inateka soko kama andazi moto, kampuni hiyo ikilipa wakulima kati ya Sh370 hadi Sh400 kwa kila katoni ya kilo nne. Wale wa spishi ya Fuerte nao wanalipwa kati ya Sh250 hadi Sh280 kwa katoni moja ya kilo nne.
Maparachichi yanayokosa kufikia vigezo vya masoko ya ughaibuni, cha kuridhisha ni kwamba yanaongezwa thamani kwa kukama mafuta.
“Yenye muundo usioridhisha na ya hadhi ya chini, nayo tunayakama mafuta ambayo pia yanateka soko lenye ushindani mkubwa Bara Ulaya,” Bw Wachira anafichua.
Kampuni hiyo ilikuwa miongoni mwa washirika waliohudhuria Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024, yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi.
Baadhi ya vigezo inavyoweka kwa wakulima ni matunda yaliyokuzwa kwa kuzingatia taratibu kitaalamu zikijumuisha mbinu faafu kukabiliana na wadudu na magonjwa pamoja na kusambaza maparachichi yaliyokomaa vizuri.
Matunda yenye ngozi ya rangi nyeusi ndiyo huwa yamekomaa vizuri. Isitoshe, huzingatia saizi ya matunda, kiwango cha mafuta, Bw Wachira akiambia Akilimali kwamba kampuni hiyo pia ina programu na mipango ya kuhamasisha wakulima kuhusu ukuzaji bora wa avokado.
Agriculture and Food Authority (AFA) na Horticultural Crops Directorate (HCD), ambayo ni mashirika ya kiserikali, ndiyo hupiga msasa maparachichi yanayouzwa nje ya nchi.