Mbinu ya kudhibiti wadudu waharibifu bila kutumia kemikali shambani
JINSI mimea ya mkulima inavyoendelea kunawiri shambani ndivyo huwa katika hatari ya kushambuliwa na wadudu waharibifu.
Utafiti umegundua msambao wa maradhi mengi yanayokumba mimea husababishwa na wadudu mbali na changamoto za mabadiliko ya hali ya anga.
Kisayansi baadhi ya wataalam huwashauri wakulima kupanda mimea ambayo haiwezi kuvutia wadudu karibu na mimea yao ya mazao.
Kwa mfano, mkulima anaweza kukuza pilipili au vitunguu pembezoni mwa shamba lake ili kudhibiti wadudu.
Baadhi ya wakulima vilevile wamekuwa wakiandaa mchanganyiko wa kitunguu saumu ikiwa ni mojawapo ya mbinu za kale.
Paul Chege ambaye ni Mkurugenzi wa Dynasty Green Farms kutoka Maragua, Kaunti ya Murang’a, aliambia Akilimali kuwa njia bomba ya kuwafukuza wadudu hatari ni pamoja na kudumisha usafi wa shamba.
Anashauri wakulima kuepuka tabia ya kuteketeza shamba wakilenga kuangamiza bakteria na vimelea wanaofanya afya ya shamba kuzorota.
Anasema athari ya wadudu kuvamia mimea ni kubwa kwa sababu wengi hujificha chini ya majani au kutaga mayai juu ya mazao hivyo basi kufanya ubora wa mazao kushuka.
“Ishara mojawapo ni pale ambapo mkulima huanza kuona mistari meupe au makuvu meusi katika sehemu za juu ya mimea yake,” asema.
Hali hii inamhitaji mkulima kuchukua hatua za haraka kwa kupulizia dawa au kupiga doria katika kila sehemu ya shamba lake ili kubaini kiwango cha uharibifu.
Matatizo mengine shambani huwa yanatokana na ukosefu wa madini katika mimea kama vile kalsiamu au uchachu wa udongo.
“Njia ya kuzuia changamoto kama hizi za uhaba wa virutubisho ni kubadilisha mazao kwa mfano baada ya kuvuna zao hili, zao linalofuata lisiwe la jamii moja,” anaeleza.
Utaratibu mwingine wa kukinga shamba ni pale ambapo mkulima huzingatia kilimo kwa kuzingatia mfumo wa kutumia mbegu safi.
“ Mbegu hizo ambazo zimeboreshwa kibayolojia kuendana na mahitaji ya mkulima kwa msimu huo, jambo ambalo humpunguzia hasara ya kuingia gharama ya kununua dawa za wadudu,” anaeleza.
Teknolojia ya FCM
Kwa sababu ya wakulima wengi kutilia maanani mbinu za uzalishaji, Chege anasema pana umuhimu mkubwa pia kukumbatia namna ya kupunguza wadudu shambani mwao bila kemikali.
Hii ni kwa sababu mbali na wadudu kudhoofisha mimea, kunao wadudu muhimu ambao wanaweza kuboresha udongo.
Anasema teknolojia ya FCM hulenga kuwanasa na pia kuwaangamiza wadudu kama vile viwavi na vipepeo ambao huzaana kwa wingi msimu wa mvua.
Anasema hii ni njia mbadala ya kudhibiti wadudu kwa lengo la kuzuia uharibifu wa mazingira na pia kutoa nafasi kwa mkulima kuendeleza kilimo asilia.
Kifaa hiki humsaidia mkulima kutambua mapema endapo mimea yake ipo hatarini kwa kubaini aina ya wadudu ambao huenda wakavamia shamba lake na namna ya kuwakabili.
Isitoshe, anasema mbinu hii ni salama kwa sababu haitumii kemikali na pia mkulima anaweza kuzalisha chakula ambacho ni salama kwa matumizi ya binadamu.
Kifaa hiki huwa kimewekewa aina maalum ya rangi ya manjano, kijani au samawati kuwavutia wadudu.
“Kifaa hiki huwavutia wadudu wanaoruka na wale wanaotambaa na pindi wanapoingia ndani ya kifaa chenyewe hawawezi kutoka. Kisha mkulima anaweza kuwakusanya siku itakayofuata na kuwaangamiza kwa kutumia moto au kemikali mbali na mazingira ya shambani,” anaeleza.
Anaongeza kuwa kifaa hiki ni muhimu sana kwa wakulima wanaokuza matunda kama vile parachichi, maembe, na hata ndizi.
Hususan maeneo ya nyanda za juu zenye baridi shadidi kama vile Nyandarua, Murang’a, Nyeri Kirinyaga na baadhi ya sehemu za Makueni na Machakos ambazo hukuza matunda kwa wingi.