Mkazi wa jiji alivyoasi uhalifu na kujitosa katika ufugaji wa nguruwe
UFUGAJI wa nguruwe katika kitongoji cha Madoya wadi ya Huruma, Kaunti ya Nairobi, umebadilisha maisha ya Vincent Asena, 23, ambaye awali alifahamika kuwa na sifa mbaya ya wizi.
Alianza kufuga nguruwe ikiwa ni njia ya kuchochea wenzake kufuata mkondo huo, kinyume na awali alipotuhumiwa kuwa mhalifu.
Aliamua kubadilisha maisha yake miaka mitatu iliyopita na kuwa miongoni mwa vijana ambao waliokota takataka katika jaa la taka la Dandora na kisha kuwauzia wafugaji wa nguruwe.
“Nilifanya kazi kwa kipindi kirefu kuwauzia chakula hicho na nikawa ni kama nimeajiriwa. Kadri nilipokuwa nikiendelea kufanya kazi, niliona silipiwi vizuri haswa kwa kuwalisha nguruwe na kuwadunga sindano,” anaeleza.
Asena ambaye sasa anamiliki zaidi ya nguruwe 20, kutokana na juhudi zake za kufanikiwa kununua mmoja na wengine akiwachiwa na rafiki yake aliyepata kazi Amerika.
“Nina sehemu mbili ambazo natumia kufuga nguruwe wangu. Sehemu ya kwanza ipo huko chini karibu na Mto Nairobi. Hii sehemu ya pili ni kwa swahiba wangu. Mamake aliona nafanya kazi nzuri na kuniachia hii sehemu,” anaeleza Asena.
“Hii nafasi ukiangalia ni nyumba kama nne ambazo zilibomolewa na kugeuzwa makazi ya nguruwe wangu.”
Kazi hiyo imenipa amani, mizozo kati ya jamii na idara za usalama ikipungua. Anasema kuwa wakati wake mwingi hutumia kufanya usafi katika vyumba vya wanyama hao.
“Hata kuwe na maandamano ambayo nilikuwa nikijihusisha, sina wakati wa kwenda. Siwezi kujiingiza katika visa vya kupotosha. Kila wakati nalazimika kujihusisha kujua watakula nini? Watalala sehemu gani? licha ya kuwa na vijana wawili ambao hunisaidia.”
Asena anasema kuwa ufugaji wa nguruwe umemwezesha kuwaajiiri vijana watano ambao hushughulikia maslahi ya wanyama hao kwa kuhakikisha wanaishi sehemu safi na salama.
Kilichomchochea zaidi ni kufahamu kuwa kila mwaka nguruwe hao hujifungua mara mbili kwa mwaka. Huwauza nguruwe hao kila mwezi na kupata mapato ya kuwalipa vijana wenzake.
“Kila mmoja hapa hujifungua kati ya watoto wa nguruwe) 14 hadi 18.”
Tofauti na wafugaji wengine, Asena amelazimika kuwafungia ili kuepuka mzozo kati yake na majirani.
“Hapa ndani wana amani. Ukisafisha hutasikia wakisumbua. Ukiwaacha watembee watashinda kwenye mitaro iliyo na uchafu,” anasema.
Pia, huhakikisha kuwa nguruwe wake wanapata dawa za kupunguza minyoo na kuwapatia madini ya kuongeza hamu ya kula na kuzuia magonjwa.
Asena anaeleza kuwa baada ya wiki mbili huuza kivinimbi mmoja kati ya Sh3,000 – Sh5,000 kulingana na miezi yake baada ya kuzaliwa. Wale wakubwa wakiuzwa kati ya Sh10,000 – Sh15,000.
“Wakulima wa viwango vya chini kama mimi utapata wengi huzuruza kwenye mapipa ya taka kuokota chakula kile ili kuwapa. Wangu, iwapo nitaokota, huwa nalazimika kupika tena ili kuondoa viini vinavyoweza sababishia nguruwe wangu kuwa wagonjwa,” anaongoza.
Nyakati za mchana nguruwe hao hulishwa mboga ambazo huwa zimepikwa na kiporo kilichochemshwa. Majira ya jioni nguruwe hao wakilishwa viazi vitamu ambazo vimepikwa na chakula kinachouzwa madukani.