Akili Mali

Mkenya ashinda Sh8.3 milioni kwa kuvumbua kifaa cha kutambua wadudu shambani

June 15th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MVUMBUZI Esther Kimani, aliyeshinda Sh8.3 milioni kutokana na tuzo ya ubunifu wa Uhandisi barani Afrika iliyoandaliwa na Royal Academy of Engineering, ameahidi kuboresha kifaa kinachotumia kamera na miale ya jua kutambua wadudu na ugonjwa unaoangamiza vyakula shambani.

Binti huyo mwenye umri wa miaka 32 aliunda kifaa hicho kwa kutumia teknolojia ya AI. Bi Kimani ni mwanamke wa tatu barani Afrika na wa pili nchini kushinda tuzo hiyo ya kifahari baada ya Edmund Wessels pamoja na Anatoli Kirigwajjo kutoka Afrika Kusini kutajwa washindi pamoja wa 2023.

Bi Kimani alipokea Sh8.3 milioni (£50,000), kiasi kikubwa zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya Tuzo ya Afrika.

 “Lengo langu ni kuongeza Ubunifu wangu ili uweze kufaidi wakulima milioni moja nchini Kenya katika miaka mitano ijayo,” alisema Bi Kimani baada ya tuzo.

Sola inayotumia miale ya jua kutambua wadudu na ugonjwa unaovamia mimea shambani. Picha|Fridah Okachi

Binti huyo alisomea Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Eldoret (hapo awali ilijulikana Chepkoilel tawi la Chuo Kikuu cha Moi) 2015-2019, alianza uvumbuzi wake wa kutumia nishati ya jua akiwa chuoni.

Aliongeza kuwa ubunifu huo ulichochewa baada ya wazazi wake kupoteza asilimi 40 ya mazao ya kila, jambo ambalo liliathiri hali yao ya maisha.

“Tunawawezesha wakulima wadogo, ambao wengi wao ni wanawake, ili kuongeza mapato yao,” alikiri Bi Kimani.

Ubunifu wa Kimani unaonekana kuwa na uwezo wa kupunguza kupotea kwa mazao kwa wakulima wadogo hadi asilimia 30, wakati uo huo ukiongeza mavuno kwa asilimia 40.

Alisema teknolojia hiyo inafanya kazi kwa saa 24 kwa siku saba na kutoa matokea mazuri yenye kiwango cha asilimi 97.

Hata hivyo, uvumbuzi huo unasaidia wakulima walio na nusu au ekari moja, kwa kuona kwa umbali wa kilomita 600.

“Hii inamaanisha kuwa kamera moja inaweza kutoa matokeo kwa wakulima watatu kwa kuwa kwetu wengi wa wakulima wana ardhi ya ekari 3. Kila mkulima atahitaji kugharamia kwa Sh386 (£3) pekee kwa mwezi,” alibainisha.

Kwa sasa kifaa hicho kinatumiwa na wakulima 5,000, Bi Kimani akiwa na ari ya kuongeza wateja na kufikia idadi ya wakulima 10,000.

Jinsi kifaa hicho kinafanya kazi

Kifaa hicho kilichotumia teknolojia ya AI huunganishwa na kompyuta ili kutambua wadudu, magonjwa ambayo huharibu mazao, pamoja na asili mahususi ya maambukizi au uvamizi.

Baada ya kutambua, kifaa hicho hutuma arafa chini ya sekunde tano kwa mkulima. Kisha kutoa mapendekezo. Pia, hufahamisha maafisa wa kilimo wa serikali kuhusu uwepo wa magonjwa au wadudu, na kusaidia katika juhudi pana za usimamizi wa kilimo.

Wakati wa tuzo hiyo, Balozi Philip Thigo alibainisha kuwepo haja ya ubunifu nchini, hii ikiwa ni njia moja ya kukabiliana na upungufu wa chakula nchini.

“Nikiwa mshauri wa AI, tungependa kuonyesha jinsi ya kutatua shida ya chakula na kuhakikisha tunaimarisha hali ya wakulima wadogo kote dunia,” alisema Balozi Thigo.