Mkulima aliyechanganya maparachichi ndani ya shamba la chai na matokeo ni tabasamu tu!
NA LABAAN SHABAAN
WAKULIMA wengi wakiganda na majani chai eneobunge la Konoin Kaunti ya Bomet, Moses Limo ni mmoja wa wakulima waliokumbatia miparachichi na tangu aanze kulima, mapato yanazidi kuongezeka wakulima wengine wakifuata nyayo zake.
Katika shamba lake la ekari 6, Limo hupanda majani chai, karakara, ndizi, nyasi ya boma Rhodes na kufuga ng’ombe wa maziwa.
Mseto huu umemzidishia faida na kuwekea imara mfumo wake wa kutega uchumi.
Mkulima huyu ambaye ni mtaalamu wa kilimo cha chai, anafunua kumbukumbu yake kueleza Akilimali kichocheo cha kukuza avocado.
Mwaka wa 2015, katika shughuli zake za kuwafunza wakulima wa majani chai mbinu bora za kuyakuza, alikutana na mkulima aliyepanda miparachichi pamoja na chai.
“Kwa desturi, nilizoea kuwazuia kufanya hivi sababu miti hudumaza chai kwa kivuli lakini aliponifichulia kuwa hupata Sh34,000 kutoka kwa mti mmoja kwa mwaka, nikaona hapa kuna kitu,” Limo alisema.
“Limo Farm inajulikana kwa avokado aina ya hass na katika vitalu nina miche takriban 10,000 kila wakati,” akaongeza.
Kuzingatia nafasi kati ya miti ya avokado kulimsaidia sana kukabili athari yake kwa majani chai.
Alianza kwa mamia ya miche na kwa kipindi kimoja aliuza miche 2,000 akidhani ni mauzo makubwa sana sokoni.
“Mteja wangu alinipa changamoto akisema ilikuwa miche michache sana. Hapo ndipo nilijua kuna uhitaji mkubwa sana sokoni na uhaba shambani,” Limo alieleza.
Changamoto zilimkabili akianza kilimo hiki hai sababu hakuwa na uelewa mkubwa lakini baadaye akaimarika.
Mwanzo asilimia ya ukuaji wa miche ilikuwa 30 na kadri miaka ilivyosonga, miche huchipuka kwa zaidi ya asilimia 80.
Shambani mwake mlimo vitalu mmezingirwa na ua huku miche ikifunikwa na neti inayoilinda dhidi ya jua kali na matone mazito ya mvua.
Mkulima Limo ambaye ametambulisha makumi ya wakulima katika kilimo hiki, anaambia Akilimali kuwa lengo lake ni kuhakikisha Bomet inajulikana kwa kilimo cha miparachichi.
“Ninaomba siku moja nikitembea Bomet, nione kila sehemu kuna avokado na magari ya uchukuzi yanasafirisha avokado,” alisema.
Kisha akaongeza: “Bomet inajulikana sana kwa majani chai na ng’ombe wa maziwa lakini tunataka wakulima wakumbatie mitindo mingine ili kuongeza mapato ya mazao.”
Aghalabu Limo Farm hutumika kuwa eneo la mafunzo ya mbinu bora za kilimo.
Kadhalika, Limo huendeleza masomo kwenye majukwaa dijitali.
Limo anatuarifu kuwa wakulima ambao wametamani kukuza avokado huja shambani mwake kupata stadi muhimu za kuchangamkia dhahabu hii inayovutia soko la ulaya.
Mbali na miche takriban 10, 000 shambani, Limo ana miparachichi takriban 250 akipata angalau Sh20,000 kwa mwaka kutoka kwa mti mmoja.
Mtaalamu huyu wa kilimo huuza mazao na miche katika Kaunti za Bomet, Kericho, Nakuru, Kisii, Nandi na Nyamira.
Limo Farm huuza angalau 6,000 kwa mwaka kwa Sh150 kila mche na wakati kuna mvua nyingi, idadi ya miche inayouzwa hupanda.
Mkulima huyu anashukuru Wizara ya Kilimo ya Kaunti ya Bomet kwa kuwapa shime na usaidizi wa kukuza miparachichi kuwa ziada ya mazao yaliyozoeleka.