Mkulima asema siri ya mafanikio iko kwa waru aina ya shangi
NA BENSON MATHEKA
KATIKA kijiji cha Magutu, lokesheni ya Ngimini, Kaunti ya Nyandarua, Bw John Ndurere na familia yake wanashughulika katika shamba lao la viazi.
Wao hawaonekani kuchoka.
“Hatuwezi kuchoka kwa sababu wateja watawasili wakati wowote kuchukua viazi na tunataka wapate vikiwa tayari,” asema Bw Ndurere.
Mkulima huyu anakuza viazi aina ya shangi anavyosema vimebadilisha maisha yake.
“Viazi hivi vinasaidia mkulima kwa kuwa vina soko kubwa nchini. Vinatumiwa kupika chipsi katika mikahawa mikubwa na midogo nchini mbali na matumizi mengine ya upishi,” asema Bw Ndurere ambaye amekuwa akishughulika na kilimo kwa miaka mingi.
“Nimeshughulika na ukulima wa mimea tofauti kama kitunguu, kabeji na mahindi lakini viazi vimenipa faida zaidi,” asema mkulima huyo.
Mara nyingi yeye huuza mazao yake papo hapo shambani.
“Wakulima huja kuvichukua hapa shambani. Kama hakungekuwa na soko lake, hatungewaona na vingeharibikia shambani,” asema.
Licha ya viazi hivyo kuwa na soko, Wizara ya Kilimo inasema uzalishaji hautoshelezi mahitaji nchini jambo ambalo wataalamu wanahusisha na matumizi ya mbegu mbaya.
Kwa wakati huu, Kenya hutegemea mbegu za viazi kutoka nchini Uholanzi.
Wataalamu wanasema kwamba mahitaji ya viazi nchini Kenya ni tani 30,000 kwa mwaka lakini kwa wakati huu inatoa tani 6,700.
Hii ndio siri ambayo Bw Ndurere aligundua alipoamua kuzamia kilimo cha viazi aina ya shangi.
Mkulima huyo anakiri kwamba kuna uhaba wa mbegu bora za viazi.
“Huwa tunategemea mbegu tunazotoa wenyewe na kusema ukweli, matokeo yake sio ya kuridhisha,” asema.
Kulingana na wataalamu wa kilimo, ekari moja ya viazi aina ya shangi inaweza kutoa kati ya tani 12 na 15 za zao hilo mkulima akitumia mbegu nzuri na mbinu za kisasa cha kilimo.
“Kukosa kutumia mbegu nzuri kunasababishia wakulima wa viazi hasara lakini mkulima akitumia mbegu nzuri, anaweza kuvuna kati ya tani 12 na 15 za viazi aina ya shangi katika ekari moja,” asema mtaalamu wa kilimo cha viazi, Silas Wachira.
Mtaalamu huyu anaeleza kwamba aina hiyo ya viazi huchukua kati ya miezi mitatu na minne kukoma.
Viazi aina ya shangi, hukuzwa kaunti za Kiambu, Nyandarua, Meru, Nakuru, Nyeri na Bomet.
“Pia aina hii inafanya vyema katika maeneo ya Tigoni, Narok, Nandi na Kericho,” asema.
Bw Ndurere anayekuza viazi katika ekari nne za shamba lake kila msimu anasema kwamba huwa anauza gunia moja la kilo 50 kwa Sh1,200 bei ikiwa ya chini kabisa. Akiuza magunia 200 kwa msimu moja huwa anapata Sh240,000 sawa na Sh720,000 kwa mwaka.
Ndurere anasema kwamba changamoto kuu katika ukulima wa viazi aina ya shangi, ni kuhakikisha kuwa mumea hauathiriwi na magonjwa.
“Tunatumia dawa kukinga mumea na maradhi hasa baridi inayoweza kusababisha hasara kubwa,” asema akionyesha Taifa Jumapili wafanyakazi wake watatu wakinyunyuzia dawa mmea huo shambani.
Changamoto nyingine ambayo hukabili wakulima wa viazi kwa jumula ni kupunjwa na wafanyabiashara laghai wanaonunua zao lao kwa bei ya chini.
“Hata wakati ambao serikali imeweka sheria ya kutulinda kwa kuhakikisha viazi vinapakiwa na gunia la kilo 50 pekee, kuna wanaotaka tupakie kwa magunia ya kilo zaidi hasa wakati zao hilo linapatikana kwa wiki,” alisema.
Takwimu zinaonyesha kuwa ukulima wa viazi umeongezeka nchini kufuatia ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ya mimea (Kephis) kwa wakulima kutumia mbegu zilizoidhinishwa na shirika la utafiti wa kilimo la Kenya (Kalro).
Kulingana na wizara ya kilimo, Kenya inaweka mikakati ya kukuza mbegu bora ili ikome kutegemea za kutoka ng’ambo.
Ukosefu wa mbegu nzuri ni changamoto ambayo taasisi za utafiti kama Kalro na wawekezaji wengine zinaweza kutumia kuleta suluhu.