Akili Mali

Mkwanja Mrefu: Thamani ya Microsoft yagonga Sh516 trilioni, yadhihirisha nguvu za AI

Na BENSON MATHEKA August 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HISA za kampuni ya Microsoft zilipanda kwa kasi wiki jana baada ya kutangaza matokeo bora ya kifedha.

Hatua hiyo sasa imeifanya kampuni hiyo kuingia rasmi katika klabu ya matajiri wa teknolojia wenye thamani ya zaidi ya dola 4 trilioni (Sh516 trilioni) pamoja na kampuni ya Nvidia, ambayo pia inaongoza katika teknolojia ya Akili Unde (AI).

Wataalamu wa biashara wanasema kuwa thamani hii ya kihistoria ni ishara ya kuongezeka kwa matumaini ya wawekezaji kuhusu ukuaji wa uwekezaji katika AI.

Hata hivyo, ni hatua ambayo wachambuzi wa soko wanaamini bado iko katika hatua za awali – licha ya kampuni kama Microsoft kupanga kutumia mabilioni kila mwaka kuongeza uwezo wa teknolojia.

Katika robo ya nne ya mwaka wa kifedha, Microsoft ilitangaza faida nono ikihitimisha mwaka mwingine wa ukuaji mkubwa kutokana na ongezeko la wateja wanaovutiwa na uwezo wa AI wa kampuni hiyo.

Mnamo Alhamisi mchana, hisa za Microsoft zilikuwa zimepanda kwa asilimia 4.3, na kuiwezesha kampuni hiyo kufikia thamani ya soko ya karibu Sh516 trilioni baada ya muda mfupi.

“Teknolojia ya Cloud na AI ndizo zinazoendesha mageuzi ya kibiashara katika kila sekta na tasnia,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa Microsoft, Satya Nadella.

“Tunaendeleza ubunifu katika kila ngazi ya teknolojia ili kuwasaidia wateja wetu kukua na kuendana na enzi hii mpya.”

Matokeo hayo yalipongezwa na wachambuzi wa soko la hisa katika mkutano wa matokeo ya kifedha, ambapo Nadella alijivunia kuanzisha vituo vipya vya data katika mabara sita ndani ya mwaka mmoja uliopita, na pia alitaja mikataba mikubwa ya ushirikiano na mashirika ya kimataifa kama Nestle na Barclays.

Microsoft ilikuwa miongoni mwa kampuni za kwanza kuwekeza kikamilifu katika AI baada ya uzinduzi wa ChatGPT mwaka 2022 uliotikisa sekta ya teknolojia.

Tangu 2019, Microsoft imekuwa na ushirikiano wa kimkakati na OpenAI, mtengenezaji wa ChatGPT, ikiwa na haki za mali miliki ya teknolojia hiyo.

Sababu ya matokeo hayo ilikuwa ongezeko la asilimia 39 katika Azure – jukwaa la kompyuta ya Microsof Cloud – ambalo sasa linapewa msukumo mpya kupitia AI, kwa mujibu wa mchambuzi wa teknolojia Angelo Zino kutoka CFRA Research.

Zino alieleza kuwa karibu kila ongezeko la hivi karibuni la thamani ya Microsoft linatokana na uwekezaji wake katika AI.

Ingawa kampuni kama Nvidia zimepata umaarufu kutokana na kuibuka kwa AI katika miaka ya hivi karibuni, Microsoft imekuwa ikiongoza mashirika ya Amerika kwa muda mrefu.

Chanzo kikuu cha mapato ya Microsoft ni bidhaa za kila siku za kazi kama barua pepe ya Outlook na mtandao wa ajira wa LinkedIn.

Pia ina idara kubwa ya michezo ya video kupitia kifaa chake cha Xbox.

Biashara zote hizi zinatarajiwa kufaidika zaidi kutokana na nguvu ya Microsoft katika AI.