Akili Mali

Shughuli ya upanzi imekuwa rahisi tangu agundue mtambo huu

April 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

HUU ni msimu wa kupanda na wakulima wengi kutoka Kaskazini na kusini mwa Bonde la Ufa wameanza kuandaa mashamba yao kwa ajili ya upanzi.

Hii ikiwa ni katika mojawapo ya hatua muhimu kuongeza uzalishaji wa chakula kwa taifa na kipato kwa wakulima.

Wengi wao wanakumbana na changamoto tele kama vile kukodisha mitambo ya planter, tiller na gharama ya juu ya diseli na petroli.

Kwa upande mwingine teknolojia ambazo zinachukua nafasi kubwa msimu huu wa kuandaa mashamba ni kama vile sensa za udongo,ndege za droni zisizokuwa na rubani na taarifa za kimaeneo kwa kutumia mfumo wa GPS.

Katika kijiji cha Bronjo Kaunti ya Uasin Gishu Akilimali inakutana na Timothy Kenyo ambaye ni afisa mstaafu wa Jeshi.

Anaamini kwamba endapo bei ya diseli itateremka siku zijazo bila shaka akiwa miongoni mwa wakulima wengine wengi watakuwa na wakati mzuri wa kuendesha kilimo chenye faida.

Huduma

Ikumbukwe msimu huu wauzaji mbegu, mbolea na mitambo ya kuandaa mashamba wanashuhudia idadi kubwa ya wakulima wanaowatembelea wakisaka huduma , ushauri au pembejeo za upanzi.

Anashauri serikali kuweka mikakati ya kuhakikisha wakulima wadogo wanaweza kutengenezewa maghala au viwanda vya mashine za kuandaa mashamba yao kuwafikia mashinani.

Hii itawasaidia kupunguza safari wanazofunga kila mara inapofika msimu wa upanzi kwa ajili ya kusaka pembejeo muhimu za kilimo.

Anasema hali ya anga inaonekana kuwa nzuri hii ikiashiria kwamba wakulima wanatarajia mavuno mavuri mwisho wa msimu huu.

Awali alikuwa akitegemea kuwaajiri vibarua wa kutosha katika hatua zote za kuandaa shamba, lakini mambo yalibadilika alipojifunza namna ya kutumia planter.

Wafanyakazi watatu tu!

Anasema siku hizi anapotumia mtambo wa planter huwa anahitaji wafanyikazi watatu tu.

Teknolojia imemsaidia kupunguza muda anaotumia wakati wa kuandaa shamba hivyo basi anaweza kuepuka changamoto za tabia nchi ambapo wakati mwingi wakulima wanaotumia jembe hulazimika kusitisha shughuli zao kwa sababu ya hali ya anga isiyoweza kutabirika
Anasema mtambo wa planter kwa mfano hutumika mahususi kupanda mbegu na pia husaidia kutengeneza mikondo ya kuweka mbolea.

Mara nyingi hukokotwa na trekta

Anaeleza kuwa matumizi ya kifaa hiki huwa ni mepesi ambapo kimtazamo huwa kimegawika katika sehemu mbili, sehemu moja huchukua mbegu na ile ya pili ikibeba mbolea.

“Katika sehemu ya juu karibu na anaposhikilia mkulima kuna sehemu wazi ambapo kuna mikondo kama paipu, iliyogawika sehemu mbili. Hapa mbolea na mbegu hujazwa,kisha zikatokea katika sehemu ya chini, dereva wa trekta anaposukuma planter ardhini,” asema, huku pia akielezea kuwa kifaa cha planter kina uwezo wa kufukia mbegu ardhini.

Kulingana naye, kifaa hiki mara nyingi hutumika msimu wa mvua wakati ambapo wakulima wengi huwa wameanzisha shughuli za kutayarisha mashamba.