Starlink ya bilionea Elon Musk yarejesha wateja iliyowapoteza Kenya
KAMPUNI ya kutoa huduma za intaneti kupitia setilaiti ya Starlink, inayomilikiwa na bilionea Elon Musk, hatimaye imerejesha usajili iliyopoteza nchini Kenya, ingawa bado haijarejesha sehemu ya soko iliyopoteza kutokana na ushindani mkali kutoka kwa kampuni za humu nchini.
Katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba, Starlink iliongeza wateja wapya 2,045 na kufikisha jumla ya watumiaji 19,470, ikiwa ni zaidi ya wale wa awali 19,146 iliyokuwa nao Desemba 2024, ambapo ilikuwa ikimiliki asilimia 1.1 ya soko la intaneti nchini.
Hata hivyo, ingawa huu ni ukuaji wa haraka zaidi kurekodiwa na Starlink Kenya tangu Januari, kurejea huko hakukuongeza sehemu yake ya soko ambayo ilishuka hadi asilimia 0.8 Juni baada ya miezi sita mfululizo ya kupungua kwa wateja.
Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Kenya (CA) zinaonyesha kuwa sehemu ya soko ya Starlink imesalia asilimia 0.8 katika robo hadi Septemba, sawa na Vijiji Connect, huku baadhi ya washindani wa ndani wakiongeza uwepo wao sokoni.
Safaricom inayoongoza, ilipata wateja wa intaneti ya nyumbani 79,288 katika kipindi hicho, na kuongeza sehemu yake ya soko hadi asilimia 35.6 kutoka 34.3 Juni.
Kampuni nyingine kama Jamii Telecoms (Faiba), Ahadi Wireless, Vilcom Network na Mawingu pia ziliongeza wateja kwa kiwango kikubwa, zikizidisha ushindani dhidi ya Starlink, ambayo ilivuruga soko ilipoingia.
Kwa jumla, usajili wa intaneti ya nyumbani nchini Kenya uliongezeka kwa 147,150 katika miezi mitatu hadi Septemba, kutoka milioni 2.14 hadi milioni 2.29.
Zaidi ya nusu ya wateja hao wapya walienda Safaricom, huku Starlink ikichangia asilimia 1.4 pekee.
Starlink awali ilishuhudia ukuaji wa kasi ilipoingia nchini, ikitwaa asilimia 0.5 ya soko kufikia Septemba 2024, kisha ikaongeza sehemu hiyo mara mbili ndani ya miezi mitatu.
Hata hivyo, ukuaji huo wa haraka uliathiri uwezo wake, na kuilazimu kusitisha usajili mpya Novemba 2024 si Kenya tu bali pia katika masoko mengine ya Afrika yaliyokuwa yakikua kwa haraka kama Nigeria na Sudan Kusini.