Akili Mali

Sumu ya pareto inavyowapa wakulima utamu wa pesa

April 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA LABAAN SHABAAN

KILIMO cha pareto kimefufuka tena baada ya kutoweka miaka iliyopita Kaunti ya Bomet.

Hitaji la pareto viwandani na duniani limechochea mamia ya wakulima kung’oa mimea mingine shambani na kuanza kukuza maua hayo.

Mercy Chepkemoi, aliyekuwa mkulima wa majanichai, anakuza pareto iliyonawiri katika thuluthi ya ekari eneo la Merigi, Bomet Mashariki.

Bi Chepkemoi aliambia Akilimali kuwa alianza kama majaribio mwaka wa 2018 na tangu hapo hajawahi kuangalia nyuma.

“Bei ya mazao imekuwa ikipanda kila msimu kuanzia Sh200 hadi sasa Sh310. Hii inanipa motisha ya kuendelea,” alifunguka.

Pareto ni kiungo muhimu sana katika utengenezaji wa dawa ya kuua wadudu viwandani.

Chepkemoi anaeleza kuwa bei sokoni hupanda kadri utathmini wa mazao unavyoonyesha kukua kwa thamani ya mavuno endapo kuna utendaji bora shambani.

“Tukivuna pareto iliyonawiri shambani, vipimo huonyesha ubora kwa hivyo bei yake huwa juu kuliko msimu uliotangulia,” alifurahia Chepkemoi.

Kampeni kali ya serikali

Ni mmoja wa wakulima ambao walichangamkia kampeni ya serikali ya kaunti kutaka wakulima kuzamia zaraa hii ili kujaza mapengo katika sekta ya uzalishaji dawa za kuua wadudu.

“Nilisikia matangazo redioni kuhamasisha wakulima wajiunge na kilimo cha pareto ikabidi nijaribu,” Chepkemoi anakumbuka.

Anakiri kuwa ilibidi wang’oe majanichai na viazi shambani ili wakumbatie pareto.

Mkulima mwingine, Stanley Kiplangat, anafichua kuwa aliondoa viazi shambani ili kukuza pareto.

“Tangu mwaka wa 2018, maisha yangu yanategemea kilimo cha pareto sababu nimepokea mafunzo mengi,” anaeleza.

Wataalamu wa kilimo wa Kaunti ya Bomet pamoja na wanachuo wanaosomea kilimo waliwapa maarifa maridhawa kustawisha kilimo biashara hiki.

Baada ya wakulima kuonyesha nia ya kukuza pareto, viwanda vya kuchakata pareto viliingilia kati na kuwasaidia kukita vivungulio kwa malipo ya chini.

Wakulima huanza kuvuna pareto ndani ya miezi miwili baada ya kupanda na inawezekana wakavuna kila siku ili kuuza kila wiki.

Aghalabu hufurahia mavuno sana wakati wa msimu wa jua kwa sababu mvua nyingi ni harabu kwa mazao.

Ekari moja huzaa hadi kilo 600 ya mavuno yakiwa mabichi lakini huuzwa yakiwa yamekauka ambapo uzani hupungua.

Matumaini ya wakulima kufurahia kazi ya mikono yao yalihuishwa na ustawishaji wa Kampuni ya Kiamerika – Kentegra Biotechnology.

Shirika hili la kibinafsi lilipewa idhini ya kuchakata na kuuza bidhaa za pareto baada ya serikali kufungua sekta hiyo ili kusheheni wanabiashara wa kibinafsi miaka minane iliyopita.

Chepkemoi ni mmoja wa wakulima angalau 2000 ambao wana mkataba na Kampuni ya Kentegra.

Kupitia ushirikiano na washikadau mbalimbali, Kaunti ya Bomet inalenga kufufua tena kilimo cha pareto kuwa chanzo endelevu cha fedha kwa wakulima.

Ushirikiano ni msingi mkubwa kustawisha kilimo cha pareto

Kaunti 18 Kenya zinazokuza pareto ziko mbioni kujenga ukanda wa kiuchumi unaojikita katika maua haya.

Maeneo yanayokuza mimea hii ni Nakuru, Narok, Nyandarua, Nyeri, Meru, Laikipia, West Pokot, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nyamira, Kisii, Bomet, Kericho, Kiambu, Trans Nzoia, Murang’a, Kirinyaga na Bungoma.

Afisa wa Kilimo wa Kaunti ya Bomet Joan Cherotich anaamini pareto ni kibadala kizuri cha kutegea wakulima mkate wa kila siku.

“Mmea huu unawavunia pesa nzuri wakulima waliouchangamkia miaka 6 iliyopita. Kinachostawisha kilimo ni ushirikiano wa makundi unaovutia washikadau kuwapa maarifa ya kilimo,” anaeleza.

“Kaunti tofauti Kenya zikishirikiana kuendeleza sekta hii, matokeo yatakuwa makubwa na kufanya Kenya kuwa bora duniani,” anaongeza.

Cherotich anasisitiza umuhimu wa mshikamano uko katika kubadilishana mawazo ya kitaalamu na kubuni vyama vya ushirika.

Shirika la Kentegra ni moja ya kampuni ambazo zinasaidia wakulima kupata soko na maarifa ya kilimo.

Kaunti ya Bomet inaripoti kukua kwa wakulima wanaozamia kilimo cha pareto sababu ya uthabiti wa nguzo za ustawishaji kilimo cha maua haya.