Uchakataji wa vyakula asilia kuangazia utapiamlo
SIRI kuwahi hela katika mtandao wa chakula na kilimo ipo katika uongezaji mazao thamani, na ni kauli anayothamini Andrew Egala.
Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 20 kwenye zaraa, Egala anachakata mazao yanayostahimili athari za tabianchi kama vile viazi vitamu vya rangi ya chungwa, mihogo, mtama, wimbi, na ndengu.
Hali kadhalika, husindika asali, akisisitiza kuwa asali pia ni sehemu ya mtandao wa bidhaa rafiki kwa tabianchi.
Egala ndiye mwanzilishi wa Green Without Borders, chini ya nembo Mugala Naturals, kampuni inayoshughulikia uzalishaji wa mazao yanayohimili mikumbo ya tabianchi, kuyachakata na kuyasambaza sokoni, kwa lengo la kuangazia utapiamlo miongoni mwa Wakenya.

Egala anadokeza kwamba kazi huanza kwa uuzaji wa mbegu, vipandio na pembejeo zingine za kilimo, akisema anatilia mkazo matumizi ya mbolea asilia.
Green Without Borders inashirikisha vijana, wanawake na washirika wote kwenye mtandao pana wa kilimo.
Kufanikisha azma yake, anatoa huduma kuhakikisha nchi inapata chakula salama kwa ushirikiano na wataalamu wa kilimo, ikiwemo, taasisi ya kiserikali ya Utafiti wa Kilimo na Mifugo (KALRO).
“Taasisi hiyo ina teknolojia za kisasa kutoa taarifa za hali ya hewa na anga kuhusu eneo fulani, hivyo basi kurahisisha ajenda yetu,” anasema.
Kwa kuwa msimu wa viazi vitamu huwa mara mbili tu kwa mwaka, hupata mazao kutoka kaunti ya Migori na Busia – kulingana na msimu.
Usafirishaji ni muhimu pia, ambapo wahudumu wa bodaboda husafirisha mazao hadi katika vituo vya usindikaji vinavyoendeshwa na wanawake wanaokausha, kusaga na kuchakata.

Hatua za kwanza za usindikaji hufanyika Migori na Busia, kilele chake kikiwa Ruiru, Kaunti ya Kiambu ambapo hutengeneza cookies, unga na vitafunwa.
Kila bidhaa huzalisha karibu tani moja kwa mwezi.
“Mugala Naturals ina mseto wa bidhaa, kuanzia cookies za mihogo, mtama, wimbi na viazi vitamu, vitafunwa na unga unaochanganywa kuongeza virutubisho,” akaambia Akilimali kwenye mahojiano ya kipekee.
Bei, nayo, anahoji ni ile inayojali Mkenya wa mapato ya chini na ya kadri.
Cookies ni Sh100 gramu 50, Sh200 gramu 100 na Sh400 gramu 200, akaelezea.

“Unga wa mihogo huuza Sh250 kwa kilo, wa ndengu Sh400 na wa viazi vitamu Sh600 – bei hii ikitokana na upotevu mkubwa wakati wa kukaushwa.”
Green Without Borders, kampuni aliyoianzisha miaka mitatu iliyopita, bado anasema haijaanza kupata faida lakini imewekeza sana kwenye uchakataji.
Egala, aliyeshiriki kwenye warsha ya mwaka huu ya Bioeconomy Cluster Development iliyoandaliwa na SEI jijini Nairobi mnamo Novemba 6, anasema changamoto kuu ni kupata mkopo kujiendeleza na kupanua biashara kufuatia masharti magumu yaliyowekwa na mashirika ya kifedha.
“Benki na mashirika yanayotoa mikopo kwa wafanyabiashara yanayohusishwa na serikali, yana masharti magumu sana kutoa fedha,” analalamika.
Hata hivyo, licha ya pandashuka hizo, anasema lengo lake ni kupunguza kero ya utapiamlo haswa kwa watoto na wakazi wa maeneo kame (ASAL) kupitia usambazaji vyakula visivyo na gluteni na vyenye mseto wa virutubisho.
Aidha, mtandao wake wa uchakataji unaegemea sana kwa maharagwe yenye madini na ndengu zenye potasiamu kusaidia kufanikisha ajenda yake.
Biashara yake ikiwa ilimgharimu mtaji wa Sh2 milioni kuwekeza kwenye mashine na mitambo ya kusaga na kuchanganya, pamoja na ya kuoka na kukausha, anasema hutumia mapato yake kupanua mradi.
Anashirikiana na zaidi ya wakulima 100, ingawa anakiri kukabiliwa na changamoto za ubora wa mazao, gharama za usafirishaji, kucheleweshwa kwa malipo haswa maduka ya kijumla, na ushuru mkubwa unaolenga wanaochakata bidhaa.