Ukuzaji mipapai ya ‘Solo F1’ umekuwa baraka kwake
ENEO la Ngwata, Kambu, Kaunti ya Makueni na linafahamika kutokana na mandhari nzuri karibu na Mbuga ya Wanyama ya Chyulu.
Ardhi ina rutuba ya kutosha na wakulima wanaweza kukuza aina mbalimbali za mimea, mboga na matunda.
Hapa tunakumbana na Bw Peter Ndambuki akiendelea kukagua shamba lake la mipapai ya kisasa aina ya Solo F1.
Ndambuki anamiliki zaidi ya miti 400 ya mipapai iliyosheheni afya kutokana na matunzo ya kupigiwa mfano kuhusu udhibiti wa maradhi.
Alifichulia Akilimali kuwa aliamua kukuza spishi hii kwa sababu hustahimili makali ya hali mbaya ya anga vilevile huchukua muda mfupi kabla ya kukomaa.
Anasema baada ya kutambua angekumbana na changamoto ya maji alichimba kisima na hatimaye kutengeneza mikondo ya maji kwa kutumia paipu za unyunyiziaji.
Anasema aliamua kukuza mipapai, zao ambalo sio maarufu sana katika Kaunti ya Makueni, tofauti na wakulima wengi kutoka eneo hili ambao wanapenda kukuza maembe, michungwa na maparachichi.
Isitoshe, kabla ya kuwekeza kwenye mradi huu, alilazimika kutafuta udongo wenye rutuba kutoka kwenye milima ya Chyulu.
“Hii ni kwa sababu eneo la Kambu limejaa mawe makubwa ambayo hufanya ardhi kuwa ngumu kiasi kwamba mizizi ya mimea haiwezi kupenya baina ya udongo,” asema.
Hali hii inamaanisha kuwa mimea haitafikia virutubishi muhimu vinavyopatikana kwenye udongo.
Kabla ya kupanda alianza kwa kufanya uchunguzi na kugundua kwamba mipapai hufanya vyema kwenye udongo mwekundu wenye rutuba na kina kirefu.
Alitafuta mbegu safi spishi ya Solo FI na kuyachimba mashimo kisha kuzifukia mchangani baada ya kuchanganya na mbolea.
Anasema aina hii ya matunda yana ladha nzuri ikilinganishwa na mipapai ya kiasili ambayo wakati mwingine huwa na ladha ya uchachu.
“Sifa nyingine ni kwamba huchukua rangi ya manjano jambo ambalo huwavutia wanunuzi kwa urahisi,”
anaeleza.
Spishi hii huchukua kipindi cha miezi mitano tu kuwa tayari kwa ajili ya uvunaji na mkulima anaweza kuvuna zaidi ya mara mbili kwa mwaka.
Kulingana na Ndambuki hatua ya kwanza ili kuendesha kilimo cha mipapai ni kuandaa shamba ili kuondoa magugu.
Shamba lake hunyunyiziwa maji angalau mara mbili au tatu kila wiki ikifuatiwa na kuwekea mimea dawa ili kuwaangamiza wadudu hatari ambao hujificha chini ya matawi.
Vilevile Ndambuki hupogoa matawi ambayo hulemea miti ili kutoa nafasi kwa mzunguko wa hewa safi na pia miale ya jua kupenya.
Anasema mti mmoja wa mipapai huzalisha matunda 100-150 kila moja ikiwa na uzito wa gramu 500-700.
Ingawaje alianza kilimo hicho kama majaribio, hivi sasa kinamletea hela nzuri na kubadilisha maisha yake.
Pia imeonyesha kwamba aina hii ya matunda yanaweza kustahimili makali ya jua, wadudu hatari na aina mbalimbali ya maradhi.
Mbali na hayo Ndambuki hutumia makundi ya wakulima wa mitandaoni kujiongezea maarifa kwa lengo la kuboresha kilimo na kuyafikia masoko ya nje.
Wanunuzi wake wengi wanatokea kaunti jirani za Machakos, Nairobi, Mombasa Kilifi na Lamu.
Kwa sasa anawarai wakulima kutoka eneo la Ngwata, Kaunti ya Makueni kukumbatia mfumo wa ukuzaji mimea kwa kutumia mbegu za kisasa ikiwa ni njia mojawapo ya kupiga jeki mapato na pia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi.
Changamoto kubwa ambayo anyokumbana nayo ni kwamba hawezi kukidhi mahitaji ya soko kwa sababu ya ongezeko la idadi ya wanunuzi wanaofurika kila mwisho wa msimu katika shamba lake.