Uongezaji thamani kuunda mikate ya viazi vitamu
JITIHADA za kupambana na utapiamlo miongoni mwa watoto Kaunti ya Bomet zilizaa kituo cha kuongeza thamani katika mazao ya shambani.
Mwaka wa 2016, kiwanda cha kusindika viazi vitamu cha Lelaitich, eneo la Sigor, Chepalungu, kaunti ya Bomet kilianza kupitia ushirikiano wa mashirika mbalimbali.
Lelaitich Sweet Potatoes Processing Plant inaendeshwa kwa ushirikiano na Mpango wa Eneo la Bandaptai wa World Vision na serikali ya kaunti ya Bomet.
Mradi wa Kustawisha Uchumi wa Bandaptai (BEEP) ulitekelezwa na Shirika la World Vision ukilenga maeneo ya Chebunyo, Kaboson na Lelaitich.
Lengo la programu hii ni kuwezesha familia maskini kulea watoto kwa njia endelevu za kiuchumi.
Mkate na Krispi kutoka kwa Viazi vitamu
Kiwanda hiki kinazalisha mkate na krispi kutoka kwa viazi vitamu aina ya rangi ya njano.
Kiwanda cha Lelaitich kinachoongeza thamani ya viazi vitamu, kimetoa nafasi za kazi kwa angalau watu 700 kuanzia utoaji pembejeo, shughuli shambani, viwandani n ahata madukani.
Peter Koskei, Meneja wa kiwanda, anaelezea umuhimu wa mradi huu katika kutoa ajira na kuboresha maisha ya watu.
“Kiwanda hiki kimechochea moto wa ajira kwa mamia ya watu wanaojihusisha na kilimobiashara,” alisema Bw Koskei.
Mkate unaozalishwa na kiwanda hiki unajulikana kama LelMatt (Lelaitich Makatiat), na umevutia wateja kutokana na virutubisho vyake.
“Agahalabu bidhaa zetu zinauzwa katika masoko ya Bomet, baadhi zikasambazwa hadi Nairobi. Tunahitaji kuongeza uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko lenye utashi mkubwa,” alieleza Bw Koskei.
Kiwanda hiki huoka zaidi ya mikate 1000 kwa siku.
Kuna soko na kazi
Mikate na bidhaa nyingine kama krispi, unga na malisho ya mifugo aghalabu hununuliwa gatuzini humo.
‘Makatiat’ hutumika kuboresha lishe katika vituHospitali ya Rufaa ya Longisa na taasisi za elimu eneo hilo.
“Kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa zetu kunajenga uhitaji wa kuboresha teknolojia zetu ili kukidhi utashi unaoongezeka,” alifafanua Bw Koskei. “Azimio letu ni kuongeza viwanda vingine sambamba kufikia mwaka 2032, kuwezesha ufugaji wa mifugo wa maziwa na utengenezaji wa chakula cha mifugo.”
Bw Koskei anadokeza kuwa, kila baada ya miezi mine, kuna msimu wa mavuno ya viazi vitamu. Kwa sababu ya mapato ya haraka, anahimiza vijana kujiunga na kilimo hiki ili kukuza uzalishaji na kubuni fursa za ajira.
“Bidhaa zetu zimeidhinishwa na Halmashauri ya Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini Mamlaka KEBS) na Mamlaka ya Kitaifa ya Usimamizi wa Mazingira (NEMA). Kwa hivyo, tunaweza kuziuza katika masoko ya eneo la Afrika Mashariki,” Bw Koskei alijitapa.
Mmoja wa wafanyakazi kiwandani humu Mercy Cherono anafurahia kuwapata fursa ya uokaji mkate ili apate mkate wake wa kila siku.
“Hii ni nafasi kubwa sana kwetu vijana kutumia stadi zetu kujisimamia na kujenga mustakabali wetu,” alisema Bi cherono.
Kupitia mradi huu, kiwanda cha Lelaitich kinaakisi jinsi sekta ya kilimo inaweza kuchangia katika kubuni ajira, kuimarisha afya na kuweka thabiti mfumo wa usalama na utoshelevu wa chakula.