Akili Mali

Utafiti: Ufugaji wa viwandani unatishia maisha ya binadamu

Na SAMMY WAWERU January 19th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

UTAFITI mpya umebaini kuwa ufugaji wa viwandani unapunguza muda wa binadamu kuishi, suala ambalo linapaswa kuangaziwa haraka iwezekanavyo.

Mfumo wa ufugaji wa viwandani, ukitajwa kuchochea msongamano wa wanyama, unaharakisha uharibifu wa mazingira na kusababisha mateso makubwa kwa wanyama, hali inayozua wasiwasi kuhusu kuendelea kutumika kwa mifumo ya kisasa ya uzalishaji wa chakula duniani.

Ufichuzi huo uliotolewa na shirika la kutetea wanyama duniani, ndiyo, World Animal Protection (WAP), unaonyesha kuwa mifumo ya kileo ya ufugaji inaleta madhara makubwa si tu kwa wanyama pekee, bali pia kwa binadamu, wakiwemo wasiotumia bidhaa zinazotokana na ufugaji wa viwandani.

Mfugaji wa kuku kwa kutumia mfumo wa cages – kuku kusongamana kwenye banda. Picha|Sammy Waweru

Ufugaji wa viwandani, ni mfumo wa kufuga wanyama haswa ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, ngamia, na pia ndege kama vile kuku, kwenye eneo moja kiwango cha wanyama kikiwa cha juu na kusongamana bila kuzingatia maslahi yao.

Hatua hiyo, WAP inasema inasababisha wafugaji kutumia vibaya dawa za vimelea na maradhi, hivyo basi kuwa hatari kwa mazingira na binadamu.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya shirika hilo, inayojulikana kama Factory Farming Index (FFI), bado kuna pengo kubwa la maarifa kuhusu athari za sekta ya ufugaji inayokua kwa kasi duniani.

Aidha, utafiti huo unaonyesha kuwa mwaka wa 2020 pekee, uzalishaji wa wanyama wanaofugwa viwandani ulifikia idadi ya kushangaza – ya wanyama bilioni 76 duniani.

Kuku wa kutaga mayai aghalabu ndio huwekwa kwa idadi kubwa kwenye mabanda wafugaji wakilenga kupata faida ya haraka. Picha|Sammy Waweru

“Karibu asilimia 46 ya kuku, nguruwe na ng’ombe wanaofugwa kwa ajili ya chakula walikuwa kwa wingi katika nchi nne pekee: China, Brazil, Amerika na Indonesia. Mataifa yanayoongoza kwa ulaji ni pamoja na Israel, Panama, Belarus na Qatar, ambapo inakadiriwa kuwa wanyama 10 huliwa na mtu mmoja kwa mwaka,” ripoti ya WAP inasema.

Mojawapo ya matokeo yanayotia hofu zaidi ni kwamba ufugaji wa viwandani unagharimu dunia wastani wa mwaka 1.8 ya afya bora ya binadamu, hii ikiashiria kupunguza muda wa kuishi.

Kulingana na WAP, hasara hii inasababishwa na matumizi makubwa ya dawa za antibiotics ambazo zinatumika kiholela na wafugaji, utoaji wa gesi hatari kutoka mashambani (greenhouse gas emission na Carbon), na ulaji wa nyama zilizochakatwa.

Watafiti waligundua kuwa tani 66,000 za antibiotics hutumiwa kila mwaka kwa wanyama wanaofugwa viwandani, kiasi ambacho ni mara mbili ya kinachotumiwa kwa binadamu.

Mkulima akikusanya mayai kutoka kwenye banda la kuku. Picha|Sammy Waweru

Dawa hizi hupewa hata wanyama wenye afya bora ili kuzuia magonjwa kwenye mazingira yenye msongamano na uchafu, hali inayotishia maisha ya binadamu.

Utafiti huo pia unajumuisha magonjwa ya mapafu na hewa chafu kutoka kwa mashamba makubwa, yanayotoa gesi ya Amonia, Nitrous Oxide na chembechembe za uchafu kutoka kwa wanyama.

Ulaji mkubwa wa nyama nyekundu na iliyosindikwa umehusishwa na Saratani ya utumbo mkubwa (colon), magonjwa ya moyo, kisukari, kiharusi, maradhi ya figo na pia shida ya akili.

Ripoti inasisitiza kuwa hata wasiotumia bidhaa za ufugaji wa viwandani bado wako hatarini kupitia dawa za antibiotics na uchafuzi wa hewa.

Mayai kwenye kreti katika mradi wa mfugaji. Picha|Sammy Waweru

Mkurugenzi Mkuu wa WAP, Tricia Croasdell, anazitaka serikali kutathmini upya mifumo ya kulisha wananchi bila kuharibu afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

“Tunapaswa kurejelea chakula cha mimea, na tupunguze msongamano wa wanyama,” Tricia anahimiza.

Utafiti unaonya kuwa mfumo wa uzalishaji chakula duniani unachangia karibu asilimia 29.7 ya gesi chafu, na kutumia asilimia 14 ya maji safi, kusababisha mateso makubwa kwa wanyama, hali inayohitaji mabadiliko ya haraka.

WAP, Kenya imekuwa ikikosoa jinsi haswa kuku na nguruwe wanavyofugwa kwenye mazingira yaliyosongamana na kusafirishwa bila kuzingatia haki za wanyama.

Mfugaji akikagua kuku wake. Wataalamu wanaonya kuhusu mfumo wa ufugaji kuku wenye msongamano, kwa sababu ya uharibifu wa mazingira na kuchangia athari za tabianchi. Picha|Sammy Waweru