Uuzaji wa miche ya miparachichi ng’ambo umewaongezea kipato
NA SAMMY WAWERU
UZALISHAJI avokado ni mojawapo ya shughuli za zaraa ambazo wakulima wanashauriwa kukumbatia.
Kando na serikali ya Rais William Ruto kujitolea kupiga jeki sekta ya kilimo kupitia ruzuku ya mbolea, kiongozi wa nchi amekuwa akihimiza wakulima kukuza mimea yenye thamani, ikiwemo avokado.
Avokado, maarufu kama maparachichi, kilimo chake kinaendelea kukumbatiwa na maeneo kama vile Kaskazini mwa Bonde la Ufa, Nyanza na Magharibi mwa Kenya, ambayo awali hayakuwa yakilima matunda hayo.
Eneo la Kati ndilo ngome la ukuzaji wa matunda haya ambayo sasa yamegeuka kuwa Dhahabu ya Kijani.
Washirika na wadau katika zao hili, nao wamepata mwanya kuvuna hela.
Isinya Avocado Nurseries, ni mojawapo ya washirika wanaohakikisha wakulima wanapata miche bora.
Ikiwa ilianzishwa 2017, kampuni hii yenye makao yake makuu Isinya, Kaunti ya Kajiado imejituma kuzalisha miche iliyoboreshwa kwa kupandikiza aina ya Hass na Fuerte.
Isitoshe, ina tawi jingine Molo, Nakuru.
Ni kutokana na jitihada zake imefanikiwa kuteka mianya ya masoko yenye ushindani mkuu nje ya nchi.
“Tumeidhinishwa na Taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea (Kephis) kuotesha miche ya maparachichi iliyoboreshwa. Tumepanua mbawa na kuiuza nje ya nchi,” anasema Valentine Nyagah, afisa kutoka kitengo cha mauzo.
Aidha, Isinya Avocado Nurseries inauza mazao yake katika nchi za Magharibi mwa Afrika kama vile Ghana, Togo na Nigeria.
Halikadhalika, kampuni hiyo imenogesha soko la miche katika nchi zinazounda Ukanda wa Afrika Mashariki, zikiwemo Tanzania na Uganda.
Valentine anasema walitambua mwanya wa usambazaji miche ya avokado kufuatia kuanza kupata umaarufu kwa matunda hayo.
“Awali, kilimo cha maparachichi hakikutiliwa maanani sana ila kwa sasa wakulima wameanza kuona thamani yake. Wanahitaji miche iliyoafikia ubora, faafu na inayozalisha kwa wingi. Shabaha letu kama washirika ni kuhakikisha tunakata kiu cha wakulima,” anafafanua.
Kinyume na waoteshaji wengine, Isinya Avocado Nurseries huuza miche yenye umri wa mwaka mmoja na yenye kimo cha mita moja, kwa Sh450 kila moja.
“Hatutumii udongo kuotesha. Tumekumbatia matumizi ya malighafi asilia kama vile; vipande vya mbao vilivyosagwa kuwa ungaunga (saw dust), nazi (coco peat), peat moss, pumice, na vermiculite,” aelezea Daniel Wanyama, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kilimo katika kampuni hiyo.
Baadhi ya malighafi hayo huagizwa kutoka Sri Lanka.
Tunzwa vyema
Mparachichi uliotunzwa vyema kitaalamu, wenye umri kati ya miaka mitatu na mitano unazalisha baina ya matunda 350 hadi 500 kwa msimu.
Isinya Avocado Nurseries lilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyohudhuria Maonyesho ya Kimataifa Barani Afrika kuhusu Avokado 2024 yaliyofanyika Sarit Expo Centre, Nairobi majuzi.
Yakiwa ni Makala ya Nne (Mei 7 hadi Mei 10, 2024), yaliandaliwa na Chama cha Ushirika cha Maparachichi Kenya, ndicho Avocado Society of Kenya.
Data kutoka Idara ya Kilimo nchini, inaonyesha mwaka uliopita, 2023, soko la avokado ng’ambo liliimarika – mapato yake yakiwakilisha asilimia 17 ya mazao mabichi.
Kuendelea kuimarika kwa matunda haya kumeiweka Kenya kwenye ramani ya kimataifa, ikitoana kijasho na mataifa kama Amerika, Mexico na Columbia.
Licha ya hatua hiyo, uvunaji wa matunda ambayo hayajakomaa – mabroka na mawakala wakichangia pakubwa, kungali kizingiti.
Hata hivyo, kulingana na Afisa Mkuu Mtendaji wa Avocado Society of Kenya, Ernest Muthomi visa hivyo vinapungua kufuatia mikakati maalum iliyowekwa Horticultural Crops Directorate.