Vijana wajipatia riziki kwa kuunda vesi za maua kutumia taka
WAKULIMA wengi wanapojihusisha na kilimo cha kawaida kama vile ukuzaji mboga na ufugaji, baadhi ya vijana wa Gatina, Dagoretti Kaskazini, jijini Nairobi wameamua kuwa tofauti.
Wao wanachangamkia utumiaji wa taka kuunda vesi za maua pamoja na kukuza maua yenyewe.
Wateja wanaomiminika humu hununua vesi hizi huku wengine wakihitaji pia kukuziwa maua ya urembo na ya kibiashara.
Mazingira yao ya kazi yamerembeka kwa sababu ya maua haya – hii huvutia sana wateja na wapitanjia.
Familia za kurandaranda mitaani huwa kiungo muhimu kwa vijana hawa wa Gatina wenye hitaji kubwa la malighafi.
Pamoja na watu wanaojitolea, vijana hawa hupokea chupa za plastiki, glasi, mavazi na taka nyingine.
“Hatuna shida ya kupata taka hizi za kuundia vesi za maua kwa sababu jiji huchafuliwa sana ovyo ovyo,” Mwenyekiti wa kundi Peter Muisyo aliambia Akilimali.
Muisyo anaamini kuwa desturi ya ukuzaji maua inafaa kukumbatia mitindo ya kisasa kuimarisha kilimo cha maua ili kufanikisha mitindo endelevu na uhifadhi wa mazingira.
“Wakulima wa maua wametuthibitishia kuwa wanaokoa pesa zao kwa kutumia vifaa hivi visivyo ghali. Hii inawaepusha na kununua vesi zenye bei ya juu sokoni,” alieleza akivumisha biashara yake kwa wateja.
Ili kupanua mawanda ya soko, kundi hili limeshirikiana na mashirika mengine.
“Tuna mkataba na Wakfu wa Raising HeARTS Foundation, shirika la hisani linalowawezesha watoto walio katika makao ya watoto,” alifichua Muisyo.
“Huwa tunaendeleza warsha za mafunzo ya kugeuza taka kuwa bidhaa muhimu. Tunaunda vitu mbalimbali kutumia katoni, mavazi mabovu, vyuma, plastiki na glasi mbali na kuendelea na kilimo cha mboga.”
Muisyo anasisitiza kuwa mpango huu huwapa watoto stadi muhimu wanaposhughulishwa katika uundaji wa vesi, kilimo na shughuli nyingine.
Bei ya bidhaa zao hutegemea vigezo tofauti huku vesi zikiuzwa bila maua ama zikiwa zimepandikizwa maua.
Kulingana nao, gharama huanzia mamia hadi maelfu ya pesa ikizingatiwa aina ya maua ama ubora na ukubwa wa vesi.
Uundaji wa vesi na bidhaa nyingine ni chanzo cha hivi punde zaidi ambacho kundi hili limejihusisha nacho.
Mwanachama anayeongoza kitengo cha kugeuza taka kuwa bidhaa muhimu Haman Ndung’u anaarifu kuwa shughuli hii imethibitisha kuwa moja ya njia bora ya kuongeza mapato ya kundi.
“Tulikuwa na lengo la kuzidisha mapato tulipoanza kundi 2019,” Ndung’u anaeleza. “Tulianza tukiwa vijana kumi wenye maono – wanaume watano na wanawake watano – ya kuungana ili kujitegea uchumi.”
Wazo hili liliibuka baada ya waanzilishi kupitia taabu walipokuwa wanatafuta kazi.
Kwa mujibu wa Mwekahazina wa kundi Anne Njoroge, wamefaulu kunasa soko kubwa katika jiji la Nairobi na viunga vyake.
Hii ni baada ya kupata wateja ambao wanawasaidia kuvumisha kazi yao na pia juhudi zao kukumbatia mitandao ya kijamii.