Akili Mali

Vijana waunda pesa kwa kuunda sabuni

Na LABAAN SHABAAN September 26th, 2024 2 min read

IDADI kubwa ya vijana nchini wanahangaika kutafuta ajira ili kujitegemea na kutegemewa katika jamii na kufuta kasumba zinazozingira maisha yao ikiwemo suala la uhalifu. 

Ili kuimarisha kiwango chao cha maisha, baadhi ya vijana wamekumbatia njia bunifu kujitegea uchumi na kujitegemea.

Hii ni simulizi ya kundi la vijana wa eneo la Gatina, Dagoretti Kaskazini, Kaunti ya Nairobi wanaojitengenezea sabuni ya maji yenye ubora wa aina yake.

Sambamba na bidhaa hii, shirika la Gatina Agri-Business Youth Group huuza vifaa vinavyotumiwa kusafisha.

Mwenyekiti wa kundi hilo Peter Muisyo, mwenye umri wa miaka 26, alianzisha kundi hili baada ya mahangaiko ya kutafuta kazi.

 “Haja yetu kuu ilikuwa kupata riziki na kuleta mageuzi ya kimienendo miongoni mwa vijana na jamii kwa ujumla,” alisema. “Niliunganisha wanarika kumi waliokuwa na matatizo sawa n kubuni mradi wa kuunda sabuni.”

Mradi huo kwa jina Super Clean Soap (SCS) Project husambaza sabuni kwa wateja jijini Nairobi hasaa Kawangware, Kangemi, Westlands na maeneo ya Dagoretti.

Mwekahazina wa kundi hili Anne Njoroge, 25 anafichua kuwa wao huuza angalau lita 200 kwa siku wakiwa na lengo la kufikisha lita 10,000 kwa mwezi.

Anne Njoroge aonyesha sabuni wanayotengeneza. PICHA | LABAAN SHABAAN

“Kwa sasa tuna changamoto ya kuongeza viwango kwa sababu pesa nyingi huenda kwa kodi ya nyumba na ada za umeme na maji,” anafunguka.

Muisyo, Mwasisi wa kundi, anaeleza jinsi shirika hili limekumbatia ushirikiano na kampuni nyingine ili kuendeleza ajenda yao ya kuimarisha jamii.

Anaarifu kuwa wateja wameonesha bidhaa hii kidole gumba kwa jinsi wanavyorejea kununua mara kwa mara.

“Kundi letu limesajiliwa na mamlaka ya serikali kama vile idara ya biashara ndogo ndogo na za kadri. Tuko katika hatua ya mwisho ya kupokea idhinisho kutoka kwa halmashauri ya kutathmini ubora wa bidhaa nchini KEBS,” alisema kwa ujasiri.

“Shirika la kijamii la Raising HeARTS limeungana nasi na kutulipia mafunzo ya kuongeza stadi za kuunda sabuni ili tuwasaidie kuwafunza watoto walio katika makao ya kuhifadhi watoto,” akaongeza.

Soko la bidhaa

Vijana hawa wa Gatina hutumia mitandao ya kijamii kunadi sabuni na aghalabu wateja wao wako jijini Nairobi.

Kadhalika, wajasiriamali hawa huhudhuria maonyesho ya biashara ili kuvutia wateja na kutafuta washikadau.

Sabuni hizi za matumizi ya kawaida nyumbani huuzwa kwa vipimo vya lita moja, tano na ishirini.

Sabuni ya maji katika vipimo vya lita moja na ishirini. PICHA | LABAAN SHABAAN

Walianza kwa kupata mafunzo kutumia mtandao wa kupeperusha video maarufu YouTube.

Kisha baadaye wakapokea mafunzo zaidi katika viwanda ili kuboresha thamani ya bidhaa zao.

“Biashara yetu imepanda kutoka mtaji wa Sh1500 hadi zaidi ya Sh100,000 na tunaendelea kukua,” anafafanua.

Muisyo anaorodhesha changamoto ya usafiri, kutokuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa zaidi na upungufu wa malighafi kama baadhi ya matatizo wanayokumbana nayo.