Wataalam waelezea umuhimu wa mazao yaliyoboreshwa
SUALA la vyakula vinavyoboreshwa Kisayansi huibua hisia mseto nchini hasa kuhusiana na ubora wake, huku Wanasayansi wakiendelea kuhakikishia Wakenya kwamba ni vyakula salama.
Wataalam hao sasa wanaonya kuwa Kenya imepoteza karibu Sh20.4 bilioni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa kuchelewa kukumbatia mimea iliyoboreshwa vinasaba maarufu kama GMO.
Ripoti mpya, “Gharama ya Kuchelewa” imeandaliwa kwa ushirikiano kati ya mashirika ya BioTrust Innovation (BTI), Alliance for Science, African Agricultural Technology Foundation (AATF), ISAAA Africenter na International Potato Center (CIP).
Inadokeza kuhusu hasara za kiuchumi na kimazingira, zinazotokana na kuchelewesha kuidhinishwa, kukuza na kuuza mimea ya GMO ambayo tayari imehakikishwa kuwa salama kwa matumizi nchini na Wanasayansi na watafiti.
Kufikia sasa, Kenya imeidhinisha rasmi kilimo na usambazaji kibiashara wa pamba aina ya Bt cotton (mnamo mwaka 2020).
Mahindi aina ya Bt maize, yamekamilisha ukaguzi wa usalama kupitia Mamlaka ya Kitaifa kuangazia Usalama wa Vinasaba (NBA), huku majaribio ya viazi vya late blight-resistant na mihogo, yakiendelea.
Mazao hayo yameboreshwa ili kupambana na magonjwa na wadudu waharibifu, hasa kipindi hiki taifa na ulimwengu unapambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, yanasifiwa kuwa bora kusaidia wakulima kupunguza hasara inayotokana na upuliziaji dawa dhidi ya wadudu na magonjwa ya mimea.
“Kiasi cha pesa ambacho Kenya imepoteza kwa kukawia kukumbatia mimea na mazao ya GMO kingeweza kununua zaidi ya tani 300,000 za mahindi, chakula cha kutosha kwa zaidi ya Wakenya milioni 1.5,” anasema Dkt Daniel Kyalo, Meneja Mkuu wa Sera, Kilimo Biashara na Mauzo AATF. Ripoti hiyo ilizinduliwa majuzi jijini Nairobi.
Utafiti huo wa miaka mitano ulitathmini faida za kiuchumi na kimazingira ambazo Kenya ingeweza kupata iwapo mimea na mazao matatu ya GMO, Bt cotton, Bt maize na viazi vya late blight-resistant, ingekumbatiwa na kukubalika kikamalifu.
Wanasayansi wanasema kukawia huko kumetokana hasa na kesi za mahakamani zinazopinga uamuzi wa serikali kuondoa marufuku ya miaka 10 (2012–2022) kuhusu uagizaji na usambazaji wa bidhaa za GMO. Marufuku hiyo iliondolewa mwaka 2022 na Rais William Ruto.
“Kuna upotoshaji mwingi na dhana potovu kuhusu mazao ya bayoteknolojia. Mazao haya yamefanyiwa tafiti kwa miaka mingi na ni salama,” anasisitiza Dkt Kyalo, akinyooshea kidole cha lawama mashirika ya kigeni kwa kusambaza taarifa anazohoji si sahihi wala za kweli zinazochochea hofu miongoni mwa umma.
Wataalamu wanasema umma kukosa kuhamasishwa kikamilifu kuhusu tija za GMO, kutokuwa na imani, ni changamoto nyingine kubwa, hali ambayo imenyima Kenya kukumbatia mbegu bora zaidi zinazostahimili magonjwa, wadudu na mabadiliko ya tabianchi.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mazao ya GMO yana faida za kimazingira kama vile kupunguza matumizi ya dawa zenye kemikali kuua wadudu na kudhibiti utoaji wa gesi chafu.
Ripoti hiyo inafafanua kuwa, kuchelewa kwa miaka mitano kukubali Bt maize kumegharimu Kenya karibu Sh8.6 bilioni. Sehemu kubwa ya hasara hii imetokana na wakulima kuendelea kutumia dawa ghali za kuua wadudu kwenye mahindi. “Lau nchi ingekubali Bt maize mapema, wakulima wangezalisha tani 194,000 zaidi za mahindi, sawa na asilimia 25 ya mahindi yaliyoagizwa kutoka nje ya nchi mwaka 2022,” inasema ripoti hiyo.
Inakadiria kuwa kufikia mwaka 2030, faida ya kiuchumi ya Bt maize inaweza kufikia Sh28.2 bilioni endapo mahindi hayo yatakumbatiwa na wakulima.
Kukawia kukuza pamba ya kisasa – Bt cotton kumewagharimu wakulima na watumizi karibu Sh155 milioni katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Kwa upande mwingine, kutolewa na kuidhinishwa kwa viazi aina ya 3R-gene Shangi vinavyostahimili ugonjwa wa late blight kunaweza kuleta faida ya Sh21.1 bilioni kwa wakulima, na Sh10.8 bilioni kwa walaji ndani ya miaka 30, kulingana na ripoti hiyo.
Josphat Muchiri, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini, Uhamasishaji na Ushirikiano katika NBA, kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali, alisema ripoti hiyo inaakisi uhalisia uliopo, ingawa Kenya imekuwa makini kuhakikisha usalama kabla ya kuruhusu ukuzaji wa GMO.
“Kenya imezingatia Itifaki ya Cartagena kuhusu Usalama wa GMO,” Bw Muchiri anasisitiza, akiongeza kuwa serikali imewekeza pakubwa katika mifumo ya udhibiti kupitia Sera ya Kitaifa ya bayoteknolojia na Kanuni za Usalama.
Profesa Richard Oduor, mhadhiri mwanabayolojia wa molekuli kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta, kwenye mahojiano alikosoa wanaopinga teknolojia ya GMO, akisema wamepotoshwa.
“Teknolojia hii imetumika kwa zaidi ya miaka 70,” alisema Prof Oduor. “Kinachochekesha zaidi ni kwamba wengi wanaopinga GMO husafiri hadi ng’ambo, mfano, Amerika, moja ya wazalishaji wakubwa wa mazao haya na hula bidhaa za GMO huko bila wasiwasi.”
Wakulima wa Kenya wamekuwa wakikuza Bt cotton tangu mwaka 2021, na imeonyesha udhabiti wake mkubwa dhidi ya mdudu aina ya African bollworm anayeharibu sana pamba. Mahindi ya Bt yamepata idhini zote za usalama na sasa yanangoja kibali cha Baraza la Mawaziri, kabla ya kuanza kukuzwa na kuuzwa.
Baraza la Usalama wa Vinasaba (NBA), Halmashauri ya Mazingira (NEMA), taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea Nchini (KEPHIS), na Wizara ya Kilimo wameshathibitisha kuwa mazao hayo yanaafikiana na viwango vya kitaifa vya usalama na ulinzi wa mazingira
Barani Afrika, matumizi ya bayoteknolojia katika kilimo yanaongezeka. Nchi zinazokuza GMO zimeongezeka kutoka tatu mwaka 2018 hadi nane mwaka 2024. Nchi hizo ni Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Nigeria, Sudan, Eswatini na Afrika Kusini.
Wataalamu wanasema ikiwa Kenya itakubali teknolojia hii kwa wakati na kwa uwajibikaji, inaweza kusaidia pakubwa katika kufanikisha usalama wa chakula, kupunguza gharama za uzalishaji, na kuongeza ustahimilivu wa wakulima dhidi ya changamoto za tabianchi, magonjwa na wadudu.