Wataalamu ni ufunguo wa ufanisi katika ufugaji ng’ombe wa maziwa
BETTY Bett alijitosa katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa bila maarifa na ujuzi unaohitajika aliponunua ng’ombe mmoja miaka minane iliyopita.
Mfugaji huyu anayeishi katika kijiji cha Kapsoyo Wadi ya Silibwet Township, Bomet ya Kati, anafichua kuwa alikabiliwa na changamoto nyingi awali kabla ya kustawi hatimaye.
Japo alikuwa na shauku ya kuwa mzalishaji mahiri wa maziwa shambani, ulimbukeni uliyumbisha azma yake.
Aliona mwanga wa matumaini katika ufugaji baada ya kutangamana na wataalamu wa kilimo wa kaunti ya Bomet kupitia Programu ya Kustawisha Kilimo maarufu (ASDSP).
Bila kukata tamaa kwa kukumbwa na vikwazo mwanzoni, alianza safari ya kujifunza na kukua chini ya ushauri wa ASDSP.
“Safari haikuwa rahisi,” anaeleza Bett. “Lakini kwa mwongozo kutoka kwa ASDSP, nilijifunza mbinu za kilimo bora.”
Aligundua kuwa hakuchagua spishi bora wa ng’ombe wa maziwa alipoanza. Kupata maziwa ya kiwango cha chini nusura kumkatishe tamaa.
Huku akiendelea kupokea mafunzo kutoka kwa wataalamu, Bett alijiunga na kundi la kijamii la Kapsoyo lililojumuisha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Ushirikiano huu wa kujengana ukawa msingi wake wa ustawi.
Zizini mwake ana ng’ombe 15 wa maziwa aina ya Fresian wanaojulikana kwa kutoa maziwa mengi.
“Nikiwa na ng’ombe 15 wa maziwa, ninavuna matunda ya uteuzi makini kulingana na ujuzi niliopata kutoka kwa wataalamu. Ng’ombe wangu hunipa wastani ya lita 28 kila siku,” anaambia Akilimali.
Isitoshe, mafanikio ya Betty hayajikiti tu katika uchaguzi wa aina bora ya ng’ombe. Pia, hatua yake ya kukumbatia teknolojia na uvumbuzi imempiga jeki.
Kupitia mwongozo wa maafisa wa mifugo, alijifunza kuhusu upandishaji mbegu bandia (AI) ili kuimarisha ubora wa kijeni wa mifugo yake.
“Mbinu hii ya kisayansi imeboresha uzalishaji wa maziwa na kuhakikisha kuwa kila kizazi kipya kina afya na tija zaidi kuliko kilichotangulia,” alithibitisha.
Kwa kuimarisha mazingira ya wanyama wake, Betty amewatengea sehemu nzuri ya kulala kwa kuwapa magodoro.
“Ng’ombe wangu ni fahari yangu,” anasema Betty. “Nina bidii ili kuhakikisha wana furaha na afya bora.”
Kilimo Endelevu
Ujuzi alioupata kutoka kwa wataalamu umempa mazoea ya kukumbatia kilimo endelevu.
Betty hutunza mazingira na kuzidisha mapato kwa kutumia teknolojia ya bayogesi kuzalisha nishati safi kutumia uchafu wa shambani na jikoni.
Uchafu wa shambani kutoka kwa shamba lake la mahindi na kinyesi cha ng’ombe vile vile huunda mbolea kwa matumizi ya kilimo.
“Ninatumia taka kutoka shambani kwangu kuzalisha nishati safi inayotumika kupikia,” anaeleza. “Sikuwahi kufikiria ningefika mbali hivi kuhusu kilimo.”
Ajikuzia malisho ya mifugo
Mbali na ufugaji, Betty amebobea katika ukuzaji mimea kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Katika nusu ya ekari ya shamba, amelima mahindi huku nyasi ya Pakchong Napier ikistawi katika nusu ekari iliyobaki.
Hatua hii ya kujikuzia chakula cha ng’ombe husaidia kuafikia utoshelevu wa chakula kwa ajili ya uzalisha wa maziwa mengi.
Kadhalika, Betty hununua chakula kutoka dukani, kusawazisha mlo wa ng’ombe wake.
Changamoto sokoni
Mkulima huyu anaeleza kuwa anakabiliwa na changamoto za umbali wa soko ambayo humega sehemu ya mapato.
Imebidi apendelee mauzo ya moja kwa moja kwa wateja katika shamba lake.
Ili kuzidisha faida, Betty anaomba serikali ya kaunti isaidie uanzishwaji wa chama cha ushirika Silibwet ili wafugaji wafikie upeo wa uwezo wao kibiashara.