Makala

AKILIJIBU: Kuku wangu wananyonyoka ovyo kisha kufa ovyo, tatizo ni nini?

October 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na CHRIS ADUNGO

SWALI: Mimi ni JULIUS MALENYA, mfugaji wa kuku wa kienyeji kutoka eneo la Malaba, Busia. Vifaranga wangu wa mwezi mmoja walianza kunyonyoka na wakaanza kuonekana wanyonge kisha wakaanza kufa ghafla mmoja baada ya mwingine. Je, huu ni ugonjwa gani, na dawa yake ni ipi?

JIBU: Mwanzo, kuna sababu tatu kuu zinazosababisha manyoya kumnyonyoka ndege yeyote yule. Ya kwanza ni ile ya kawaida, hasa katika hatua za mwanzoni za ukuaji. Kunyonyoka huku kwa manyoya ni kwa kifiziolojia na kila ndege hupitia hutua hii.

Hali hii pia huambatana na ukosefu wa mwanga wa jua ambao hudhibiti homoni mwilini mwa ndege. Ndege watapoteza manyoya yao kwa muda fulani kisha yataanza kumea tena baada ya miezi miwili. Ni hali ya kawaida. Lakini ukiwaona vifaranga au kuku wako wakila manyoya yao wenyewe ambayo yashawatoka, hii ni ishara ya ukosefu wa madini muhimu mwilini.

Sababu ya pili ni kuvamiwa na wadudu. Kuna wadudu aina tatu ambao huwasumbua ndege: chawa, siafu na viroboto. Wadudu hawa wanapomvamia ndege, humlazimisha kujikuna kwa mdomo wake mwenyewe na kujipata amejinyonyoa manyoya kutokana na kule kuwashwa wakati wadudu hawa wanawanyonya damu. Wadudu hawa wasipogunduliwa mapema hutaga mayai ndani ya manyoya na kuenea kwa sehemu nyingi za ndege.

Wengine nao hujificha ndani ya magamba kwenye miguu ya ndege. Suluhu ni kusafisha mazingira ya kuku kisha kuwapa maji yenye kitunguu saumu.

Pia washarizie siki ya tufaha (apple vinegar) kwenye manyoya ili kuua chawa na viroboto. Pia unaweza kukausha majani ya mnanaa (mint) na kumwagamwaga kwenye chumba cha kuku.

Ili kutokomeza siafu wanaovamia kuku, changanya vikombe viwili vya maji, kijiko kimoja cha mafuta ya kupikia na kingine cha sabuni ya kuoshea vyombo kisha usharizie chumba cha kuku na kuku wenyewe. Ya tatu ni ukosefu wa lishe ya kutosha mwilini. Kuku na vifaranga wake wanapaswa kulishwa vyakula vyenye protini, wanga (carbohydrates) vitamini na madini muhimu. Manyoya yatanyoyoka kama kuku ana afya duni kutokana na njaa na kiu.

Pia kuku huanza kutoa manyoya iwapo kuna joto na msongamano ndani ya chumba ulimowafuga. Kumbuka mwili wa kifaranga umeundwa kwa asilimia 70 ya maji. Nyuzijoto zikizidi kupanda, maji haya huyeyuka mwilini na kumwacha kifaranga na kiu, hivyo kifo.

Ukosefu wa maji mwilini kwa asilimia 10 utaua vifaranga. Baridi nayo husababisha ugonjwa wa Kichomi (Niumonia) ambao huua vifaranga kwa wingi. Mapafu ya vifaranga waliokufa huwa na rangi isiyokolea ya samawati. Baridi hulazimisha vifaranga kukaribiana ili kupata joto. Msongamano huu huwanyima hewa ya kutosha na baadhi yao hufa.

Unashauriwa kuhakikisha nyuzi joto za chumba unamofugia vifaranga ziko kati ya digrii 29 na 35.3. Vyakula vyenye sumu inayotokana na vimelea (fungi) au vumbi ya mbao, chumvi nyingi ndani ya maji na gesi hatari (Ammonia, Carbon (I) Oxide na Carbon (II) Oxide) huwaua vifaranga papo hapo.

Kwa kawaida, vifaranga hawana uwezo thabiti mwilini wa kukabiliana na magonjwa.

SWALI: Mimi ni SABENSIA GORETTI, mkulima wa mihogo kutoka Kilgoris. Mihogo yangu imebadilika ghafla na kuanza kuwa na michirizi ya rangi ya kahawia. Je, hili ni tatizo gani na suluhu ni ipi?

JIBU: Ugonjwa huu unaitwa batobato na huathiri sana mihogo inayopandwa katika sehemu zenye miinuko iliyo na urefu wa chini ya mita 300 na unapatikana kidogo sana kwenye miinuko ya mita 500. Huenezwa na mdudu mweupe aina ya nzi mwenye mabawa madogo. Ili kubaini dalili za mapema za uvamizi, rangi ya manjano huonekana pembezoni mwa majani. Kisha hutokea mabaka meusi ya mviringo kati ya shina na mizizi ya mmea. Baada ya muda, majani huanza kunyauka na zao la mihogo kuoza.

Njia ya msingi ya kuzuia na kudhibiti ugonjwa huu ni kuchagua mbegu kutoka kwenye mimea isiyo na dalili za kuathiriwa. Mkulima anashauriwa kupanda mbegu bora ambazo zina uwezo wa kustahimili maambukizi. Uonapo hali ya kuoza kwa mizizi ya mihogo wakati wa kuvuna, iteketeze kabisa.