AKILIMALI: Ajali haikuua ari yake, yeye sasa ni mkulima wa kuigwa
Na BENSON MATHEKA
ALIPOHUSIKA katika ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha apoteze mguu wake wa kulia miaka minne iliyopita, wengi walidhani Joseph Mulei angeishi maisha ya omba omba.
Hata hivyo, alivumilia na kuwakosoa wengi kwa kuibuka mkulima stadi na kuwashinda wengi wasio na ulemavu wowote.
Bw Mulei 33, anakiri kwamba alikabiliwa na wakati mgumu kwa kipindi cha miaka miwili alipokuwa akipokea matibabu baada ya kuhusika katika ajali.
“Kabla ya kupata ajali, nilikuwa mfanyabiashara. Nilikuwa nikijitegemea na familia yangu ilikuwa changa,” asema.
Ajali hiyo ilivuruga biashara yake iliyokuwa ikinawiri katika kituo cha biashara cha Nzaikoni, Kathiani, kaunti ya Machakos na akalazimika kuifunga.
“Nilitumia pesa zangu zote kupata matibabu. Nilifanyiwa upasuaji wa kurekebisha mguu wangu mara tatu kwa gharama ya zaidi ya Sh1.5 milioni. Hii ilinifilisisha kabisa. Marafiki na pasta wa kanisa langu walinisaidia sana kupambana na hali ngumu wakati huo,” asema Bw Mulei.
Alikuwa na duka na karakana aliyokuwa akitengeneza pikipiki na kuuza vipuri. Bw Mulei ambaye ni seremala anasema alikuwa akipata zaidi ya Sh80,000 kwa mwezi kutokana na biashara hiyo.
“Japo ajali ilinirudisha nyuma. Niliomba Mungu aliyeninusuru kutoka ajalini anifungulie njia,” asema.
Baada ya kupona, aliamua kuhama eneo alikozaliwa, kijiji cha Kalunga, Kathiani na kutafuta eneo tulivu ambalo angeanza upya maisha yake na familia yake.
“Nilihisi kwamba kuishi na watu walionifahamu wakati sikuwa na ulemavu kungeniongezea masononeko. Sikutaka kuhurumiwa na kwa hivyo nikaamua kuhamia eneo tofauti. Nilitumia pesa haba zilizobaki kununua kipande cha ardhi eneo la Katuaa, Kola na nikaanza kilimo,” asema.
Anasema hakuna aliyedhani kwamba angeweza kubadilisha kipande hicho cha ardhi kuwa shamba linaloweza kukuzwa mimea.
Kichaka
“Kilikuwa kichaka. Sikuwa na pesa za kuajiri wafanyakazi na kwa hivyo binafsi nilianza kukata miti na kulima. Wengi walinishangaa, baadhi wakasema nilikuwa nikijitesa kutokana na hali yangu na singefaulu. Baada ya miezi michache, nilikuwa nimebadilisha kichaka kuwa shamba,” asema.
Shamba hilo liko eneo la mteremko na Mulei alichimba mitaro kuzuia maji ya mvua kusomba mchanga wenye rotuba. “Kwa mikono yangu mwenyewe nimefanya kazi hii. Lengo langu kuu lilikuwa ni kupata shamba la kukuza chakula cha kutosheleza familia yangu,” asema.
Kwa wakati huu, eneo lililokuwa kichaka, sasa limepambwa kwa mahindi, maharagwe, kunde na aina tofauti za mboga zenye kijanikibichi
“Ninatarajia kuvuna magunia yasiyopungua 25 ya mahindi na 15 ya maharagwe. Haya yamekuwa mavuno yangu kwa miaka miwili iliyopita tangu nihamie hapa na ninashukuru Mungu,” Mulei alieleza Akilimali ilipopata shambani mwake.
“Hii ni hatua ya kwanza. Sitaki kuwa omba omba watu walivyosema nilipohusika kwenye ajali. Ninataka kuwa mfano kwa watu wanaoweza kujipata katika hali sawa na yangu kwamba wanaweza kunufaika kwa jasho lao,” aeleza Bw Mulei ambaye ni baba ya watoto wawili.
Na wanaojipata na ulemavu, Mulei ana ushauri: “ Nina hakika kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kula jasho lao mradi tu wabadilishe mawazo yao. Ninaamini Mungu huwa anabariki kazi ya mikono ya mtu na anaweza kubariki kidogo kilichopatikana kwa jasho kikawa kingi,” anasema.
Na ana imani kuwa siku moja atafufua biashara yake. “ Hii shamba yangu itanipa mtaji wa kurudisha biashara yangu mradi tu niko hai,” asema Bw Mulei anayetembea kwa mikongojo.
Anasema anatarajia kuuza magunia 20 ya mahindi ili apate mtaji wa kuanzisha biashara yake na kusisitiza kuwa hataacha kilimo. Shamba lake linapakana na bwawa la kijamii na anasema akipata jenereta ya kupiga maji ataendeleza kilimo cha mboga na matunda.
Katika sehemu moja ya shamba lake, amepata miparachichi na mipaipai.
“Changamoto ni uhaba wa fedha lakini ninaamini Mungu atafungua njia niweze kupata mtambo wa kupiga maji,” asema.