AKILIMALI: Aliacha mihadarati, sasa mfugaji mbuzi
Na PETER CHANGTOEK
UMBALI wa kilomita takribani 15, kutoka mjini Chuka, ndipo kilipo kitongoji cha Kathatwa, ambapo kuna shamba ambalo linajulikana kwa jina Murang’a Farm.
Shamba hili linamilikiwa na Samuel Muriithi, mkulima ambaye hushughulika na ufugaji wa mbuzi pamoja na ukuzaji wa miche ainati.
Mkulima huyu huwafuga mbuzi aina mbili: German Alpine na Toggenburg. Kwa mujibu wa Muriithi, mbuzi hao wameboresha maisha yake kutokana na riziki anayoipata kwa kuwauza na kuyauza maziwa.
Anaeleza kwamba mbuzi hawa hustahamili hali ngumu katika mazingira tofauti tofauti, na kuwa wana manufaa mengi. “Kuwafuga mbuzi hao kumenipa maisha mema,” aungama mkulima huyu mwenye umri wa miaka 30.
Muriithi ana nyasi aina ya brachiaria, ambazo hutumia kuwalisha mbuzi wake na hivyo kuboresha uzalishaji. Mimea hiyo ya foda, huwa na majani magumu yanayofanya kuwa vigumu kwa magugu kuota shambani. Nyasi hizi pia zina kiwango kikubwa cha protini- asilimia 14 hadi asilimia 20, na hivyo kuwawezesha mbuzi wake kukua upesi mno.
Kwa mujibu wa mkulima huyu, katika ufugaji wa mbuzi ni muhimu kuyazingatia mambo kadha wa kadha, mathalani lishe bora, kuvijenga vibanda vinavyofaa na kuhakikisha kuwa mbuzi wana afya.
“Vibanda vinafaa kuinuliwa juu angalau futi mbili kutoka ardhini, na sehemu ya mbuzi kula kutenganishwa na sehemu inayotumiwa na mbuzi kulala. Vibanda pia viwe na mwangaza wa kutosha na viwe safi na kavu kwa sababu unyevu huwavutia wadudu na magonjwa,” aeleza Muriithi.
Mkulima huyu humuuza mbuzi mmoja aina ya German Alpine na Toggenburg kwa bei ya Sh16,000 hadi Sh25,000. Aidha, humuuza mwanambuzi kwa bei ya Sh8,000.
Yeye huwakama mbuzi wanne, ambapo hupata lita 9 hadi lita 12 za maziwa kila siku. Yeye huyauza maziwa hayo kwa bei ya Sh90 kwa kila lita. Huyauza maziwa yake pamoja na mbuzi wake kupitia mtandaoni.
“Maziwa ya mbuzi huwa yana manufaa mengi kuliko maziwa ya ng’ombe,” afichua Muriithi, akiongeza kuwa maziwa haya huwa hayaathiriwi na mfumuko wa bei. Anaongeza kuwa kwa sababu ya kutoathiriwa kwa bei, maziwa hayo ya mbuzi yana mapato tele.
Muriithi, ambaye hapo awali alikuwa akishughulika na shughuli ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, anadokeza kuwa alikata kauli ya kujitosa katika ufugaji wa mbuzi maadamu mbuzi wana tija kubwa.
Anongeza kuwa ufugaji wa mbuzi huwa hauna gharama kubwa ikilinganishwa na ufugaji wa ng’ombe wa maziwa. Aidha, anasema kuwa mbuzi hufugwa kwa kutumia nafasi ndogo, ilhali ufugaji wa ng’ombe huhitaji sehemu kubwa ya kuwafugia.
“Kuwauza mbuzi pia ni rahisi kuliko kuwauza ng’ombe kwa sababu mnunuzi anatakiwa tu kuwa na Sh16,000, ambazo ni rahisi kupata ikilinganishwa na kiwango cha hadi Sh100,000 zinazohitajika kumnunua ng’ombe,” aeleza mkulima huyu.
Yeye huwalisha mbuzi wake saa kumi na mbili asubuhi kwa kutumia nyasi aina ya brachiaria na mahindi pamoja na lishe nyinginezo.
Ili kuboresha shughuli hiyo ya ufugaji wa mbuzi, Muriithi huhudhuria semina mbalimbali ambazo huandaliwa na Muungano wa Wafugaji wa Mbuzi wa Maziwa, Kenya (Dairy Goats Association of Kenya- DGAK), mjini Nyeri, kupata mafunzo.
Mkulima huyu anasema kwamba kuzalishana kwa mbuzi wake aghalabu huwa changamoto. Hata hivyo, yeye humchukua beberu kutoka kwa muungano wa DGAK mjini Nyeri, ili kuzuia kutokea kwa changamoto hiyo.
Ili kuzidisha mapato yake, yeye aliamua kujitosa katika ukuzaji wa miche miezi sita iliyopita. Aliianzisha shughuli hii kwa kuutumia mtaji kutoka kwa shughuli ya ufugaji wa mbuzi, na kwa wakati huu, ana miche takribani 55,000.
Anasema kuwa ni sharti awe makini kulitumia shamba dogo alilonalo. “Nilianzisha ukuzaji wa miche ili kuongeza mapato yangu,” asema mkulima huyu ambaye aliacha kuitumia mihadarati ili kujishughulisha na shughuli zinazompa riziki.
Ana miche ya mikangazi (mahogany), ambapo yeye huiuza miche hiyo kwa bei ya Sh200 kila mmoja.