AKILIMALI: Aliacha ualimu na sasa maharagwe yanamlipa ajabu!
Na SAMMY WAWERU
KAUNTI ya Nandi ni kati ya maeneo maarufu katika uzalishaji wa majanichai nchini, na taswira inayolaki mgeni katika Kijiji cha Kapsoo, Kaptumo, katika kaunti hiyo ni rangi ya kijani ya majanichai na miti inayochangia kuwepo kwa mvua kila wakati.
Idadi kubwa ya wakazi wakiwa mateka wa zao hilo, katika shamba la Joshua Tiongoi mambo ni tofauti kabisa. Amefanya kinyume na mtazamo wa wengi.
Kwa muda wa miaka miwili mfululizo, kijana huyu amekuwa akikuza maharagwe, zao ambalo ni adimu eneo hilo ila sasa wakulima kadhaa wameanza kufuata nyayo zake.
“Eneo la Nandi wenyeji hutegemea mapato ya majanichai kujiendeleza kimaisha. Mashamba mengi na makubwa ni ya majanichai, ila ninajaribu kuwakwamua kutoka kwa minyororo hiyo, waone umuhimu wa kukuza mimea inayochukua muda mfupi,” Joshua, 34, anasema.
Kabla ya kujitwika jukumu hilo, Joshua alikuwa mwalimu wa shule ya msingi ambapo alifunza Somo la Kiswahili, Historia na Dini.
Mwaka wa 2011, aliacha ualimu, akaanzisha biashara ya uuzaji wa maziwa na mnamo 2013 akajitosa katika shughuli za kilimo. “Nilianza kwa kukuza viazi katika pointi tatu ya ekari,” anadokeza, akiongeza kwamba aliwekeza mtaji wa Sh20,000, kukodi shamba, kununua mbegu, mbolea, gharama ya vibarua, kemikali na mahitaji mengine yaliyoibuka.
Kwa sababu alikuwa amefanya utafiti wa kutosha na mwingi wa ari kufanya kilimo, alipanda mbegu za viazimbatata zilizoimarishwa, na miezi mitatu baadaye anasema mavuno yalimtia tabasamu. “Nilipofanya hesabu, mapato yalikuwa zaidi ya Sh40, 000, mara dufu ya mtaji,” anafichua.
Ni kupitia jitihada zake katika zaraa, mnamo 2018 Joshua aligundua kuna uhaba na wakati mwingine ukosefu wa maharagwe Nandi. Aligeuza gapu hiyo kuwa mwanya wa kilimo-biashara. “Zaidi ya asilimia 80 ya mashamba Kaunti ya Nandi, ni uga wa majanichai. Nilipoona wakazi wanahangaika kupata maharagwe, nilianza kuyalima,” anadokeza, akisema alianza kwa nusu ekari.
Anaendelea kueleza kwamba aligharamika jumla ya Sh25, 000 kuyakuza. Maharagwe ni kati ya mimea inayochukua muda mfupi kuzalisha, na miezi mitatu baada ya upanzi huanza kuvunwa.
Joshua anasema alivuna magunia matano, moja likiwa na uzani wa kilo 90. “Kila gunia niliuza kati ya Sh10, 000 – 12, 000, na chini ya miezi mitatu pekee nilikuwa na mapato yasiyopungua Sh50, 000 kupitia kilimo cha maharagwe,” anafichua.
Huku eneo la Nandi likiwa na gapu ya maharagwe, mkulima huyo anasema alipata oda chungu nzima kutoka kwa shule na taasisi mbalimbali za masomo. Ni hatua iliyomchochea kuyakuza zaidi. Kati ya ekari tano za wazazi wake, barobaro huyo ametunukiwa ekari 1.3, ambazo hulima zao hilo.
“Nina hofu, shule zikifunguliwa wakati wowote kuanzia sasa huenda nikalemewa kukithi kiwango cha oda zitakazoibuka,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano. Alisema, akilinganisha mapato ya majanichai na maharagwe, maharagwe yana faida chungu nzima.
Isitoshe, ni zao lisilo na gharama ya juu. “Shamba hulima mara mbili, na wiki moja au mbili baadaye, huandaa laini za mitaro,” anaelezea. Kulingana na Joshua, nafasi kati ya mtaro hadi mwingine huipa sentimita 50.
Anasema hutumia mbolea ya mifugo, ambayo wakati mwingine huichanganya na fatalaiza. “Katika kila shimo (mashimo huandaliwa kwenye mitaro), hupanda punje za mbegu mbili ya maharagwe,” anasema.
Ekari moja inahitaji kilo 20 za mbegu. Maji si hoja Nandi, kutokana na mvua inayoshuhudiwa mara kwa mara, Joshua akisema eneo hilo ni sawa na Canaan, kwa sababu ya baraka za maji. Anasema wakati bora kuwa na maharagwe shambani ni kati ya mwezi Agosti hadi Oktoba, kwa kile anataja kama miezi inayopokea mvua ya kadri.
“Changamoto kuu katika kilimo cha maharagwe Nandi ni mvua kubwa, ya mawe inayoharibu mazao,” anaeleza mkulima huyo.
Matunzo ya maharagwe, ni pamoja na palizi, fatalaiza ya kuimarisha na kustawisha mazao, dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, hasa msimu wa mvua kubwa.
Ekari moja huzalisha kati ya magunia 8 – 10, ya kilo 90 kila moja. “Gunia halipungui Sh12, 000. Gharama kuzalisha ekari moja ni chini ya Sh40, 000,” akadokeza Joshua, akisema kwa mwaka huwa na misimu mitatu.
Huku maharagwe yakijumuishwa katika familia ya mimea ya legumi, yanasifiwa kwa kudumisha na kuimarisha rutuba kwenye udongo. “Maharagwe huongeza rutuba na Nitrojini (madini muhimu kwa mimea) kwenye udongo. Badala ya kutumia fatalaiza zenye kemikali kuongeza Nitrojini katika udongo, wakulima wawe wakitumia maharagwe kufanya mzunguko wa mimea shambani,” anahimiza Caroline Murage, mtaalamu.
Mbali na kulima maharagwe, Joshua Tiongoi pia hukuza viazi na kabichi. Mkulima huyo anasema ni kwa muda mfupi tu amejipa, aingie kwenye orodha ya mamilionea wachanga nchini kupitia kilimo cha maharagwe ambacho kinaendelea kumtia tabasamu.
Kando na shule na taasisi mbalimbali za masomo, wateja wengine ni wakulima waliopevuka na kuanza kukuza maharagwe ambao humtegemea kupata mbegu.