Makala

AKILIMALI: Alianza ukulima akiwa mwanafunzi na sasa amepiga hatua

January 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

WANAFUNZI wakiwa shuleni aghalabu hujishughulisha na mambo mengi, mbali na harakati za kubukua vitabu ili kuondoa uzuzu.

Aidha, kuna waliojaliwa talanta tofauti kama vile soka, netiboli, riadha, voliboli, masumbwi, raga, michezo ya kuigiza, muziki, kukariri na kughani mashairi, miongoni mwa michezo mingi tu.

Michezo inasifiwa kunyoosha viungo, kupumzisha na kutuliza bongo na mawazo yao, ikizingatiwa kibarua kigumu kinachowakodolea macho cha kusoma.

Katika muktadha uo huo, kuna wanaojishirikisha katika visa vya kupotosha kama unywaji wa pombe kupindukia, utumizi wa dawa za kulevya na mihadarati.

Ni visa ambavyo wengi wamejipata kutekwa nyara navyo, wanaishia kuhangaisha walimu na wazazi, kilele kikiwa ndoto zao kukatizwa ghafla ikiwa hawatanusurika.

Katika taasisi mbalimbali za elimu, kuanzia shule ya msingi, upili, vyuo anuwai na vyuo vikuu, kuna vyama au makundi mbalimbali kupalilia talanta za wanafunzi. Kuna vya michezo ya kuigiza, sarakasi, mashairi na kilimo na ufugaji, hivyo vikiwa vichache tu kuviorodhesha.

Lawrence Mbithi akiwa katika shule ya msingi na upili, kilichoteka na kutawala mawazo yake na ratiba yake ni shughuli za kilimo.

Anasema baada ya kushiriki masomo darasani, muda wake wa ziada aliutumia katika klabu cha kilimo.

“Ilifikia kiwango nikapata jina la lakabu ‘mkulima mdogo’ kwa sababu ya mapenzi yangu katika shughuli za kilimo,” asema Lawrence. Anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba akiwa darasa la nane tayari alikuwa na mgunda wake wa kukodi, eneo la Thika.

Kijana huyo anaendelea kusimulia kuwa alishiriki vibarua vya hapa na pale, hususan kulimia watu mashamba na hata kubeba mizigo, muradi apate mtaji kuafikia lengo lake.

“Nilikusanya Sh5, 000 ambazo nilikodi kipande kidogo cha shamba,” adokeza.

Kulingana na simulizi yake, aling’oa nanga kwa ukuzaji wa mboga za kienyeji. Alipanda mboga kama vile; mchicha maarufu kama terere, mnavu almaarufu managu au sucha, majani ya kunde, spinachi na sukuma wiki.

Kwenye orodha ya alichopanda, pia alijumuisha vitunguu vyekundu vya mviringo, wengi huvitambua kama vitunguu viazi, kwa Kiingereza red bulb onions.

Lawrence anasema yeye ndiye alijifanyia shughuli zote, kuanzia kulima, upanzi, utunzaji kwa njia ya palizi, unyunyiziaji maji, kupulizia dawa dhidi ya wadudu na magonjwa, hivyo basi leba kwake haikuwa balaa.

Hilo anasema lilichochewa na kile anachotaja kama kuzaliwa katika familia iliyoenzi shughuli za kilimo.

“Mama na baba ni wakulima, hivyo basi kilimo nilikijua tangu nikiwa mdogo,” aeleza.

Kwa mujibu wa maelezo yake, pindi tu baada ya shule, majira ya jioni, Lawrence Mbithi alikuwa akijituma hadi shambani, jambo lililowatia moyo na motisha wavyele wake, haswa kuona mwana wao alijiwajibikia. Msimu wa likizo, ratiba yake ilikuwa kujikumbusha aliyosoma na kufanya kilimo.

Ni mkondo aliouendeleza akiwa shule ya upili. Anasema mahitaji binafsi, yeye ndiye alijishughulikia. “La wazazi lilikuwa kulipa karo,” asema.

Lawrence ambaye ana umri wa miaka 21, alifanya mtihani wa kidato cha nne, KCSE mnamo 2018 na sasa amezamia kilimo kikamilifu. “Wito wangu upo kwenye kilimo, kimenifanyia mengi na makuu,” asema, akifichua kwamba mwaka uliopita aliweza kununua pikipiki ambayo humsaidia kusafirisha mazao sokoni na vibarua vya kubebea wakulima wenza mazao yao.

Kwa sasa anafanya zaraa kwenye nusu ekari anayoikodi Sh6, 000 kwa mwaka, ambapo amezamia katika kilimo cha vitunguu viazi. Anasema zao hilo ni mithili ya mahamri moto, mwakani akipania kukodi shamba lingine.

Vitunguu vingi vinavyoliwa nchini vimetoka katika taifa jirani la Tanzania, ambalo ni mkuzaji mkuu Ukanda wa Afrika ya Mashariki. Hii ina maana kuwa zao hilo halijakumbatiwa na wakulima wengi, licha ya hali ya anga na udongo Kenya kutajwa kuwa bora kuzalisha vitunguu viazi.

Aidha, hapa nchini maeneo yanayotambulika katika ukuzaji wa vitunguu hivyo ni Kiawara eneobunge la Kieni, Karatina, Naromoru na Mweiga, yote hayo yakiwa kaunti ya Nyeri. Mengine ni Kajiado, Kakamega, Emali na Naivasha.

Kulingana na wadau wa masuala ya kilimo, ekari moja iliyotunzwa vizuri kwa kuzingatia vigezo muhimu katika ukuzaji wa vitunguu, ina uwezo kuzalisha kati ya tani 20 – 30, sawa na kilo 20,000 hadi 30,000. Kilo moja inauzwa kati ya Sh40 – 80 kijumla, kulingana na misimu.

“Miezi bora kuratibu kuvuna vitunguu ni kati ya Novemba hadi Mei,” anasema Ngugi Mburu, mtaalamu na mkulima hodari wa zao hilo la Nyeri. Hatua ya Lawrence Mbithi kuwa na mazao msimu huu, ni kutokana na mapato yake bora.

Ni kijana ambaye amebobea katika kilimo cha vitunguu, ikikumbukwa kwamba alikianza kitambo.

Ili kujiimarisha, James Macharia mtaalamu na mkulima pia, anasema anachopaswa kufanya kwa sasa ni kusomea taaluma ya masuala ya kilimo.

“Kuna vyuo kadha wa kadha hapa nchini vinavyotoa mafunzo ya kilimo kama vile Chuo Kikuu cha Egerton na cha Jomo Kenyatta, ndicho JKUAT. Anaweza kujisajili anolewe bongo zaidi, atalifaa taifa hili siku za usoni. Sisi tulioanza huduma kitambo tunakaribia kustaafu, vijana wachukue usukani,” ashauri Macharia, akiongeza kusema kwamba shamba lake (Lawrence Mbithi) atakuwa akilitumia kuonesha umahiri wa anachofunzwa.

Mdau huyo anapongeza juhudi za kijana huyo, hasa kuanza kupalilia talanta yake tangu akiwa shuleni. Anasema kuzinduliwa kwa mfumo wa uamilifu, CBC, huenda kukasaidia kutambua na kupalilia vipaji tofauti, katika mdahalo mzima kujaribu kutatua suala la ukosefu wa kazi hasa miongoni mwa vijana.

“Taifa hili limejaaliwa mashamba makubwa yenye rutuba. Tuyatumie kufanya kilimo na ufugaji, kufungua viwanda vya kuongeza thamani kwenye mazao ya kilimo. Utata wa ukazi utasuluhishwa,” ahimiza mtaalamu huyo.