• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
AKILIMALI: Ana uzoefu wa miaka 20 katika ukuzaji wa vitunguu, zao linaloendelea kumtia tabasamu

AKILIMALI: Ana uzoefu wa miaka 20 katika ukuzaji wa vitunguu, zao linaloendelea kumtia tabasamu

Na SAMMY WAWERU

KILIMO cha vitunguu vya mviringo au vitunguu viazi maarufu kama “red bulb onions” kinampa upekee kwa sababu kutokana na mauzo, anapata riziki na kukidhi mahitaji yake ya kila siku.

Gedion Makau, 45, ana uzoefu wa miaka 20 katika uzalishaji wa vitunguu hivyo.

“Sijaanza leo, jana wala juzi kilimo cha vitunguu. Nilianza kuvikuza mwaka wa 2000,” anadokeza.

Makau alifanya kazi za sulubu na za kijungu jiko hapa na pale ambapo aliweka akiba ikafika Sh50,000 mtaji anaosema ulimfungulia milango ya heri katika sekta ya kilimo. Alianza kilimo hiki katika nusu ekari, eneo la Narok.

Anasema jaribio lake la kwanza halikumfisha moyo.

“Baada ya kuondoa gharama ya matumizi, ikiwamo kukodi shamba, mbegu, mbolea na leba ya wafanyakazi, nilipata faida ya Sh125,000 chini ya kipindi cha miezi mitano pekee,” anafichua.

Ni mapato anayosema yalimtia tabasamu na motisha kuendelea kukuza kiungo hicho cha mapishi.

Makau anasema alikodi kipande kikingine cha shamba, akawa na jumla ya ekari moja, ukuzaji vitunguu ukawa afisi yake kujiendeleza kimaisha na kukimu familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Kilichofuata, ni historia, ambapo historia ya wakulima wanaojikakamua kwa hali na mali kuangazia uhaba wa vitunguu vya mviringo nchini ikiandikwa hii leo, jina lake halitakosa kujumuishwa.

“Nimesomesha watoto wangu kupitia kilimo cha vitunguu, watatu kati yao wamehitimu vyuo vikuu na sasa wanafanya kazi,” anasema mkulima huyo ambaye ni baba wa watoto saba.

Mbali na kukuza zao hilo Narok, pia analilima eneo la Mai Mahiu, ambapo wakati wa mahojiano tulimpata akiwa na vitunguu vilivyoko katika ekari nne.

Huku vitunguu vikiwa kati ya viungo vya mapishi vinavyotumika sana, idadi ya wakulima nchini haitoshelezi kiwango cha mahitaji. Ni upungufu ambao huchochea wafanyabiashara wauzaji wa zao hili kuagiza kutoka taifa jirani la Tanzania, ambalo ni mkuzaji tajika wa vitunguu Afrika Mashariki.

Kulingana na Makau, Kenya pia inaweza ikawa mkuzaji mkuu, kwa kile anataja kama “nchi hii kuwa na udongo bora na hali bora ya anga kuzalisha vitunguu”. Anasema muhimu zaidi, ni wakulima wahamasishwe wakumbatie kilimo cha vitunguu kwani kina mapato ya haraka.

“Kinachofisha wengi moyo na kukata tamaa kuendelea kulima vitunguu, ni kukosa kutambua muda unaofaa kuvipanda ili walenge soko bora na lenye mapato ya kuridhisha,” akaambia Akilimali wakati wa mahojiano katika shamba lake eneo la Mai Mahiu.

Alisema vitunguu vinavyovunwa kati ya mwezi Januari na Februari, huwa mithili ya dhahabu sokoni kwa sababu ni kipindi ambacho mashamba Tanzania hayana mavuno.

“Kipindi hicho, vinavyotoka Tanzania huwa vichache mno. Hivyo basi humu nchini bei huwa imenoga, ikizingatiwa kuwa ni wakulima wachache wanaozalisha vitunguu hapa Kenya,” akasema.

Vitunguu vina uwezo kuhifadhika hadi muda wa miezi sita mfululizo, na Makau alisema kwa sasa ana zaidi ya tani 10, sawa na kilo 10,000 kwenye ghala ambazo anasubiri bei iwe bora.

“Kilo kwa sasa ni kati ya Sh70 – 100, ninasubiri itakapogonga Sh150, hasa mapema mwaka 2021,” anasema mkulima huyo stadi, maelezo yake yakiashiria akipata soko bora huenda akaogelea kwenye bahari ya hela.

Hebu tufanye hesabu kwa mujibu wa kiwango cha vitunguu vilivyoko kwenye ghala lake; Makau akiwahi soko la Sh150 kwa kila kilo, ni wazi atatia kibindoni kima cha Sh1.5 milioni pesa taslimu.

Na ikiwa kila kilo itapata soko la Sh100, mkulima huyo bado ataingiza mapato yasiyopungua Sh1 milioni.


Gedion Makau anasema amesomesha wanawe kupitia kilimo cha kiungo hicho cha mapishi. Kwa sasa ana vitunguu kiasi cha kilo 10,000 kwenye ghala, na analenga soko la Sh150 kwa kilo, ishara kuwa akiliwahi ataingiza mapato ya Sh1.5 milioni. Picha/ Sammy Waweru

“Si ajabu kila mwaka kuingiza mamilioni ya pesa kupitia kilimo cha vitunguu,” anaelezea mkulima huyo akionekana kujivunia jitihada zake. Vitunguu huvunwa miezi minne baada ya upanzi.

Kulingana na Ngugi Mburu, mtaalamu, vinafanya vyema katika udongo usiotuamisha maji na wenye rutuba.

Aidha, anasema udongo unapaswa kuwa na asidi, pH, kati ya 5.8 – 6.8

“Mfumo bora, katika upanzi ambao umeibuka, ni matumizi ya besini (udongo unaandaliwa kuunda mfano wa besini ya mstatili),” anadokeza mtaalamu huyo, akisema mfumo huo unasaidia kupunguza uvukizi wa maji.

Muhimu kufanikisha kilimo cha vitunguu ni kuwepo na chanzo cha maji ya kutosha, Ngugi akihimiza wakulima kuzingatia taratibu kitaalamu kukuza zao hilo.

Eneo la Mai Mahiu ni nusu jangwa, na upungufu wa maji ndio kizingiti kikuu kwa wakulima. Makau hutumia mfumo wa kunyunyizia mimea na mashamba maji kwa mifereji.

Hutegemea mito ya muda, maji ya mvua na visima au vidimbwi, ambavyo wakati wa ukame hukauka.

“Wakulima Mai Mahiu wakipata kiini cha maji ya kutosha, yasiyokosekana hata kiangazi kikiingia, tutachangia pakubwa kuwepo kwa vitunguu nchini,” mkulima huyo anasema, akihimiza serikali kuwazindulia miradi ya maji.

You can share this post!

Leicester wapepeta Leeds United na kutua nafasi ya pili...

EPL: Fulham walaza West Brom na kujiondoka kwenye mduara...