• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
AKILIMALI: Ana zaidi ya miti 1,000 ya matunda haya yasifiwayo kuongeza damu

AKILIMALI: Ana zaidi ya miti 1,000 ya matunda haya yasifiwayo kuongeza damu

Na FRANCIS MUREITHI

BARABARA ya mchanga inayotoka kituo kidogo cha biashara cha Wiyumiririe kando ya barabara kuu ya kutoka Nyahururu kwenda Nyeri imekarabatiwa sambamba na hufanya safari ya kwenda msitu wa Aberdares takribani kilomita 12 kuwa fupi.

Na unapokaribia msitu wa Aberdares hali ya hewa ya joto jingi inatokomea na kijibaridi na upepo mwaroro kutoka msitu unazizima.

Hatimaye, safari inakamilika katika shamba dogo la matunda katika kijiji cha Mwangaza kilichoko kando ya msitu wa Aberdares.

Shamba hili la ekari moja na robo linamilikiwa na John Mureithi Nduhiu mwenye umri wa miaka 45 ambaye amejizatiti na kupanda matunda aina ya tree tomato, komamanga, machungwa na mizabibu.

Bw John Mureithi Nduhiu ambaye ni mkulima wa matunda ya mti nyanya ‘tree tomato’ akiwa shambani mwake katika kijiji cha Mwangaza, Ndaragwa, kaunti ya Nyandarua. Picha/ Francis Mureithi

Hali kadhalika mkulima huyu shupavu ameshamiri katika upanzi wa nyanya na hoho ambazo hupanda kwenye hema za greenhouse, mbali na kupanda miche ya mitishamba na maua pia ana kidimbwi cha kufuga samaki.

Kutokana na umahiri wake wa kupanda matunda, shamba hili huwa ni kivutio cha wakulima, watafiti, wanafunzi wa vyuo vikuu ambao husafiri kutoka maeno mbali mbali ya nchi kama vile Uasin Gishu, Nairobi, Nakuru, Busia, Embu na kaunti jirani ya Nyeri kuja kujionea utaalamu wa kisasa wa kupanda matunda hasa matunda ya tree tomato ambayo imemuundia jina.

Historia fupi

Safari yake ya kilimo hiki iling’oa nanga 2008 wakati alipopanda miche 100 ya tree tomato aina ya solid gold ambayo kufikia sasa ni zaidi ya 1,000.

“Nilianza kilimo cha kupanda matunda aina ya tree tomato kwa Sh5,000 ambazo nilitoa kwenye akiba ambayo mimi huweka kila ninapouza matunda,” Mureithi anadokezea Akilimali.

Aidha, mkulima huyu anafichua kuwa kilimo cha tree tomato ni dhahabu ambayo Wakenya wengi bado hawajang’amua.

“Mti mmoja wa tree tomato hutoa kati ya kilo mbili na tatu baada ya kuvunwa wiki mbili kila mwezi na nikiwa na miti 1,000 hiyo inamaanisha mimi huvuna kati ya kilo 2,000 na 3,000,” anafichua mkulima huyu ambaye hafichi mapenzi aliyo nayo kwenye kilimo hiki kwa tabasamu.

Na je yeye hujiwekea kibindoni pesa ngapi?

“Kilo moja ya tree tomato huuzwa kwa kati ya Sh80 – Sh100 na hii inamaanisha kuwa kwa mwezi mimi hupokea kitita safi cha pesa ambazo huniwezesha kusambaza kilimo hiki na kukidhi mahitaji mengine bila hofu,” anasema mkulima Mureithi.

Aliamua kuhamia kilimo cha matunda baada ya kupanda mahindi na viazi na kuhesabu hasara kubwa kutokana na bei duni ya mahindi.

Kwa kawaida mkulima huyu huuza matunda ya tree tomato kwa wafanyabiashara kutoka miji ya Nakuru, Nairobi, Nyahururu na Maralal amabo huvamia shamba lake kama viwavi kununua zao hili.

Ili kupata faida kemkem katika ukulima huu, Mureithi anakiri kuwa ni sharti mkulima azingatie mbinu mwafaka na za kisasa kuanzia upanzi hadi kuvuna.

Aidha anasema kuwa mwanzo kabla ya kupanda tree tomato ni vyema kuchimba shimo upana na urefu wa futi mbili mtawalia.

“Mchanga uliopakuliwa mwanzo wapaswa kuchanganywa na mbolea ya shambani ya kiasi kama kilo 20 na kisha kunyunyuzia kwenye shimo. Shimo hilo halipaswi kuzibwa kabisa na mchanga na ushauri wangu ni kuacha nafasi ya kunyunyizia maji.

“Mchanganyiko huu husalia kwenye shimo kwa wiki moja kabla ya kupanda miche ya tree tomato,” anasema Mureithi.
Ili kuzuia kukauka kwa haraka kwa unyevu ulioko kweye shimo la mmea hu, ni bora kuweka magugu yaliokauka kuzuia jua kali.

Mureithi hatumii madawa kunyunyuzia mimea yake kwani hili laweza kupelekea kutoweka kwa nyuki ambao huchangia uzalishaji wa matunda haya.

“Nimeweka nyuki na nina mizinga kadha kwani bila nyuki ukulima wa mti nyanya hauwezi kufaulu. Pia nimeweka viwavi wekundu ambao huwalisha na mboga na maji wanayotoa kama kinyesi huchanganya na maji kuunda mbolea,” anasema Mureithi.

Aidha anasema kuwa yeye huchanganya lita moja ya kinyesi cha viwavi wekundu na maji lita tano na hutumia mchanganyiko huo kunyunyuzia matunda yake kupigana vita na wadudu waharibifu na magonjwa.

“Mbali na kutumia madawa yasiokuwa na kemikali mimi pia hupanada kitungu saumu na kitungu cha kawaida kwani harufu inayotokana na mimea hii hufukuza wadudu na nzi ambao huvamia matunda haya kutoka na sukari nyingi,” anasema Mureithi.

Anasema mmea wa mti nyanya hulipandwa kulingana na maagizo ya wataalamu wa kilimo na hudumu kwa kipindi cha miaka saba na lazima uwe wa kijani kibichi ishara tosha kuwa una afya kibao.

You can share this post!

AKILIMALI: Maua ni pesa na kwa Mzee Konde yamelisha na...

AKILIMALI: Wateja hufuata mpunga wake wa pishori shambani

adminleo