AKILIMALI: Baada ya kustaafu Mzee Tui sasa anafanya makuu katika ukulima
Na SAMUEL BAYA
UNAPOFIKA katika kijiji cha Endao, eneobunge la Subukia, Kaunti ya Nakuru utaliona shamba lililonawiri kwa mazao mbalimbali.
Kwa ukaribu utagundua wazi kwamba anayemiliki shamba hilo ni mtu ambaye ameitikia mwito wa kulijenga taifa hili kupitia kilimo.
Kuna mahindi, miwa, mihogo, migomba, wimbi, viazi tamu na maharagwe.
Ni hapa ambapo Mzee Edwin arap Tui, mkulima mwenye umri wa miaka 75, na mkazi wa Baringo aliamua kuhamia na kuanza ukulima baada ya kustaafu kama mfanyikazi wa serikali.
Mzee huyu alikuwa akihudumu kama dereva katika hospitali ya kaunti ya Kajiado ila alipostaafu mwaka wa 1999, aliamua kuhamia hapa na kuweka akili yake yote katika ukulima, na hajutii kwa hilo.
Katika mazungumzo aliyofanya na ukumbi wa Akilimali, ilionyesha bayana kwamba yeye ni mkulima ambaye amejitoa mhanga kuhakikisha kwamba sekta hii inakuwa mojawapo ya sekta muhimu za kuimarishwa.
“Nilifika katika kijiji hiki mwaka wa 2006, ingawa nilistaafu kutoka kwa serikali mwaka wa 1999. Baada ya kustaafu nilielekea nyumbani Baringo kuendeleza kilimo cha kahawa. Hata hivyo nilikuwa nimeingia katika chama cha ushirika na ndiposa tuligawanyiwa ardhi hizi, niliamua kuja na kuanza ukulima hapa,” akasema katika mahojiano yetu.
Alisema kuwa baada ya kukita kambi katika shamba hilo mwaka wa 2006 na kuanza ukulima, alipata mafunzo kutoka kwa wataalam kutoka chuo kikuu cha Egerton ambao walifika na kumpa ushauri wa jinsi ambavyo anaweza kufaidika na shamba hilo.
Mwaka huo huo, alipata wataalam pia kutoka kwa shirika la maendeleo la kanisa la Kianglikana ambalo pia lilifika hapa na kumpa maelezo kuhusu jinsi ya kuboresha mazao yake shambani.
“Nilipofika katika eneo hili nilianza kufanya kazi ila muda si muda, nilipata wageni kutoka shirika la ADS la kanisa la Kianglikana pamoja na wataalam kutoka chuo kikuu cha Egerton. Wale wataalam walitufundisha jinsi ya kupanda mahindi na pia aina ya mbegu ambayo nilifaa kutumia. Nashukuru waliporudi wakati wa kuvuna, nilipata gunia 21 ya mahindi katika ekari moja unusu,” akasema Mzee Edwin.
Alisema kuwa hatua yake ya kupanda aina mbalimbali za mimea inatokana na kujaribu kuganga njaa kunapotokea ukame.
“Niliamua kupanda mimea mbalimbali kwa sababu huwezi kukosa chakula wala huwezi kuomba omba. Kwa mfano ninapokosa mahindi, nitauza muhogo na kisha ninunue kile ambacho ninataka,” akasema Mzee Edwin.
Hata hivyo alisema kuwa baadhi ya changamoto zake ni bei duni ya mazao ambayo anauza katika shamba lake. Alitoa mfano kwa zao la muhgo ambalo alisema kuwa bei yake kwa sasa iko chini.
“Mihogo iko na bei duni sana. Kwa mfano kilo moja inanunuliwa kwa Sh15 ulhali muhogo huo unapofika mjini, kilo moja inauzwa kwa kati ya Sh100 na Sh150. Madalali wanatuumiza sana,” akasema mkulima huyu.
Alitaka serikali ianze kusimamia bei za bidhaa za kilimo kwa sababu wafanyibasiahara ambao hawalimi wala kutoa jasho wanawanyasa wao kama wakulima mashambani.
“Kama wakulima, tunadhulumiwa na madalali ambao huja hapa kununua kwa bei ya chini kisha kwenda na kuuza kwa bei ya juu. Serikali inafaa kujiri na mbinu mwafaka ya kuhakikisha kwamba sisi kama wakulima tunafaidika,” akasema Mzee huyo.
Hata hivyo alisema kwamba licha ya bei kuwa chini, hata hivyo kilimo hicho shambani mwake kimeweza kumsukuma kimaisha, kwa viel yuko pekee baada ya watoto wake wote kuwa watu wazima na kuwa na familia zao.
“Ingawa mapato ni machache lakini kwa siku ninaweza kuuza mali yangu ya shamba na kupata Sh1,000. Hiyo ni fedha ambayo inaweza kunisaidia kupambana na maisha,” akasema Mzee Edwin.
Mti mmoja wa muwa huuzwa kwa kati ya Sh40 na Sh50 na wakati imekuwa vizuri, huuza hata miti 100 kwa siku hivyo basi kupata Sh5,000.
“Hii shamba yangu ni ekari moja na nusu ila ningelipata shamba lengine kubwa, mimi ningefanya kilimo kikuu hata zaidi. Ila kwa sasa ninashukuru na mazao haya ambayo ninauza na kupata riziki. Shamba hili ni hisa ambazo tulinunua kama kikundi na ndipo nikapata hapa,” akasema.
Ajira
Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walimshukuru Mzee Edwin kwa kuwapatia ajira shambani mwake.
“Huyu mzee ametusaidia sana kwa sababu anatupatia kazi hapa. Anatuajiri na mara nyingi tuko shambani mwake tukilima. Tunamsaidia kulima na kupanda ndizi, mboga, viazi tamu, wimbi na mimea mingine mingi. Yeye ni mkulima doari sana hapa,” akasema Bi Joyce Lokura. Binti yake mkubwa Bi Lydia Kiprop alimtaja babake kama mkulima hodari sana hasa katika eneo la Baringo.
“Babangu alikuwa dereva katika idara ya afya akifanya kazi katika eneo la Kajiado. Lakini kila mara alikuwa akifanya kilimo cha ukuzaji majani chai katika eneo la nyumbani Kabarnet, Baringo.
Hata sisi tulisoma kwa sababu ya kahawa ambayo alikuwa akiuza na alipostaafu ndipo akaja na kuanza ukulima hapa,” akasema Bi Kiprop.
Kwa mzee Edwin, lengo lake alisema ni kutegemea kilimo kama njia mbadala ya kupambana na maisha.
“Badala ya vijana kujazana mijini na kuhangaika kwa ukosefu wa ajira, wanafaa kurudi mashambani na kuendeleza mambo ya kilimo,” akasema Mzee Edwin.