Makala

AKILIMALI: Baadhi ya mimea inasaidia kuimarisha udongo

November 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

AGHALABU visa vya udongo kuripotiwa kuwa duni si vigeni katika mashamba ya wakulima mbalimbali nchini Kenya.

Hilo hasa linahusishwa na utumiaji wa mbolea na dawa zenye kemikali, na ni jambo linalolemaza jitihada za wengi.

Utawasikia wakilalamikia udongo kuwa duni, usioweza kuafikia matakwa yake. Ni hali inayosababisha mazao kupungua, kwa sababu ya ongezeko la changamoto zinazohusishwa na magonjwa ya udongo na hata mimea.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanahoji asidi huwa imezidi kiwango kinachopaswa.

“Asidi hujiri kupitia matumizi ya pembejeo; mbolea na dawa zenye kemikali,” anasema mtaalamu Bernadinah Magiri,.

Kulingana na mdau huyo, asidi inapozidi udongoni ni vigumu mimea na mazao kunawiri kwa anachotaja kama kusheheni kwa magonjwa ainati. “Ndio maana mkulima anapaswa kupimiwa udongo wa shamba lake katika maabara, ili kujua namna ya kuutibu,” aeleza Bi Bernadinah.

Aghalabu, udongo hutibiwa kwa kutumia laimu, ili kuusawazisha na kuuimarisha.

Wadau wa sekta ya kilimo pia wanahimiza suala la mzunguko wa mimea, katika mdahalo mzima kuimarisha rutuba ya shamba.

Nitrojini ni madini muhimu zaidi katika ustawishaji wa rutuba, na mimea inayoorodheshwa katika familia ya legumi, wakulima wanashauriwa kuikumbatia. Mimea yenyewe ni kama; maharagwe, kunde na mbaazi. Orodha hiyo pia inajumuisha njegere (peas), maharagwe asilia (garden peas) na maharagwe ya soya.

Joshua Tiongoi, ni mkulima wa nyanya, mboga na matunda na anasema anapovuna mazao, hupanda maharagwe ili kuimarisha udongo shambani mwake. “Maharagwe yamesheheni Nitrojini na ni mimea faafu katika uimarishaji wa rutuba,” anasema mkulima huyo.

Awali, alikuwa na mazoea ya kutumia mbolea zenye kemikali kuuimarisha, asijue ilichangia katika kuudunisha.

Kiwango chashuka

Kulingana na mkulima huyo, kilichomuatua moyo ni kuona kiwango cha mazao kikiendelea kushuka.

Asidi ikizidi kwenye udongo, mimea haina budi ila kudhoofika, kwa ajili ya ukosefu wa madini faafu kuistawisha.

Isitoshe, anasema shamba lake liligeuka kuwa uga magonjwa yaliyojificha udongoni.

“Nilipokumbatia ukuzaji wa maharagwe baada ya mavuno, udongo ulianza kurejea hali yake,” anaeleza.

Ili kupata mazao salama, mkulima anashauriwa kutumia mboleahai, ile ya mifugo na kuku. Mfumo huo, kilimohai, unapigiwa upatu kama njia mojawapo kuepuka matumizi ya pembejeo zenye kemikali kwani zinachangia katika usambaaji wa maradhi.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasema mbolea hiyo iwe imeiva (decomposed) sawasawa kabla ya kutumika.

Baada ya kulima shamba, imwagwe na kuchanganywa na udongo.

Ili kuzuia uvukizi wa maji, mashina ya mimea iwekwe nyasi, hasa zilizokauka, maarufu kama boji.