Makala

AKILIMALI: Badala ya kusubiri sana, panda tofaha hili linalokomaa upesi

May 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na SAMMY WAWERU

Anajulikana kama Peter Wambugu, lakini ukitaja Wambugu Apples, anwani yake inatambulika ulimwengu mzima.

Hii ni kutokana na matofaha ya aina yake anayokuza. Aghalabu, moja lina uzito wa karibu gramu 125, tofauti na yale mengine.

Mzee Wambugu hakusomea taaluma yoyote ile ya kilimo wala inayohusiana na shughuli za kulima, lakini ni mtafiti gwiji wa masuala ya kilimo.

Mara ya kwanza kutambulika katika zaraa ilikuwa mwaka wa 2000, baada ya kuibuka Mkenya wa pekee aliyekuza matofaha nchini.

Mzee huyu amekuwa jikoni akipika, si mapishi ya mlo ila kufanya majaribio ya aina mpya ya matofaha aliyovumbua 2014.

Anasema ameibuka na matofaha ambayo yakipandwa leo, miezi tisa baadaye mkulima ataanza kupata mazao.

Matofaha yanayolimwa nchini na mataifa mengine huvunwa baada ya miaka miwili.

Isitoshe, ya mkulima huyu ni aina inayofanya vyema maeneo ya kiangazi, hususan yanayopokea mvua kiduchu. Aidha, hayabagui mchanga, uwe ule mwekundu au udongo kwa mujibu wa maelezo yake.

Matofaha yanaaminika kustawi maeneo ya baridi kwa minajili ya kushinikiza majani yapukutike, ili uchanaji wa maua uanze, hatua muhimu kuruhusu uundaji wa matunda.

Hata hivyo, Bw Wambugu ametegua kitendawili hicho, na anasema haya mapya pia yanakua vyema eneo lolote muradi tu lisiwe la chemichemi.?Idhini ya Kephis na Karlo?Ni ya kupandikiza (grafting) na uvumbuzi wake umeidhinishwa na taasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo) na ya ubora wa mimea (Kephis).

“Karlo ndiyo iliyapa jina la Wambugu Apples, baada ya kuyapiga msasa na kubainika utafiti tuliofanya uliafikia ubora unaohitajika,” anasema meneja wa mauzo na matangazo Catherine Nyokabi Wambugu, ambaye pia ni binti ya mtafiti huyu.

Mara ya kwanza baada ya upanzi, Wambugu Apples huzalisha karibu matunda 20, idadi hii ikiongezeka kila msimu. Kulingana na utafiti wa mkulima huyu ni kwamba, mavuno ya kwanza, mengi ya mitofaha inazalisha ikiwa na urefu wa kuanzia futi mbili hadi nne.

“Kiwango cha mavuno huongezeka kila msimu, cha muhimu ni kuyatunza kwa maji na mboleahai (ya mifugo),” adokeza Bw Wambugu, akiongeza kuwa yana misimu tatu kwa mwaka.

Soko lake kuu la miche limekuwa mataifa ya kigeni, Barani Afrika; Nigeria, Zimbabwe, Botswana, Ghana na Cameroon.

Marekani na Israili pia ni baadhi ya wanaotambua umuhimu wa Wambugu Apples. Agnes Omingo ambaye ni mkulima Ongata Rongai, Kajiado ni mmoja wa wateja wa Wambugu Apples.

Kajiado hukumbwa na kiangazi, na amepanda mitofaha 100 kwenye robo ekari.

“Nilianza ukulima wa matunda haya Julai 2017. Mavuno ya kwanza yalikuwa Aprili mwaka uliopita, hayakuwa mengi. Ninaendelea na ya pili na kufikia sasa nimevuna kilo 500, yanaendelea kuchana maua na kuzalisha,” asimulia Bi Agnes, akisisitiza kuwa huyatunza kwa mbolea ya mifugo na maji.

Mazao na kongole?Mche mmoja wa Wambugu Apples unagharimu Sh1,000 huku tofaha akiuza kwa zaidi ya Sh50.

“Msimu wa kwanza ni tosha kurejesha gharama ya miche. Ni matofaha utakayovuna kwa muda mrefu,” aliambia Akilimali, ilipotaka kuelezwa bayana kuhusu bei yake.

Amepokea kongole kutoka kwa baadhi ya wateja katika nchi za kigeni wakihoji kuwa mtofaha unazalisha hata zaidi ya matunda 1,000 kwa mwaka.

Kenya, Mama Ngina Kenyatta, mke wa Rais mwanzilishi wa taifa hili Hayati Mzee Jomo Kenyatta na mama wa Rais wa sasa Uhuru Kenyatta, ni kati ya viongozi tajika waliomzuru kuthibitisha uhalisia wa matofaha haya.

Laikipia ni miongoni mwa kaunti zinazoorodheshwa kushuhudia kiangazi, na ndiko mkulima huyu ameyapanda.?Eneo la Ngobit, Laikipia Mashariki, ufugaji na kilimo cha mahindi ndio umeshika kasi.

Lakini katika shamba la Bw Wambugu, ekari tatu imesitiri matofaha. Anafichua kuwa ekari moja ina mitofaha 500.

Wakati wa mahojiano, tulipata baadhi ikichana maua na mingine ikizalisha. “Watu hudhani dhahabu ni ile ya kuchimbwa pekee, la hasha. Wambugu Apples ni dhahabu aliyonitunuku Mwenyezi Mungu. Matunda haya ni dhahabu jangwani,” aelezea, akihimiza serikali ipigie upatu kilimo cha matunda haya ili kuangazia upungufu wake.

Bi Nyokabi, meneja wa mauzo na matangazo katika kampuni ya Wambugu Apples, anasema mbali na matunda haya kustahimili juakali, ni nadra kushambuliwa na wadudu na magonjwa ya mimea.

Anaendelea kueleza kwamba miche inayouzwa nje ya nchi sharti ioshwe kuondoa mchanga.

“Mataifa ya kigeni hayaruhusu mchanga kutoka nchi zingine. Kenya pia hairuhusu mchanga wake kuenda nje, ndio maana lazima miche ioshwe na hata kupukutua majani,” asema.

Wambugu alianza kilimo cha matofaha 1985. Awali, alikuwa akipanda kahawa, karakara na matunda ya kuongeza damu mwilini-tree tomato.

“Nililazimika kung’oa mikahawa baada ya kuhangaishwa na bei duni ya mazao. Matunda ya karakara na tree tomato, mavuno yalikuwa haba, kupata soko nayo ilikuwa balaa,” anasema.

Mkulima huyu anasisitiza kuwa kamwe hajutii kupanda matofaha.