Makala

AKILIMALI: Brokoli, mboga yenye faida kiafya na kimapato

December 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

NA SAMMY WAWERU

Brokoli ni mboga ya kipekee inayoorodheshwa katika kundi la familia moja na kabichi na koliflawa.

Ingawa sifa zake zinawiana na za kabichi, kitoweo cha mboga hiyo ni majani ya kijani na matawi yake. Majani yake aidha yanakua kwenye kichwa chake, pia yakizingirwa na mengine yanayofanana na sukuma wiki.

Mahitaji ya brokoli yanaendelea kuongezeka hususan katika mikahawa na maduka ya kijumla yanayofahamu madhumuni yake, wataalamu wa masuala ya afya wakihoji hitaji hilo linaambatana na manufaa yake kisiha, ambayo ni mithili ya changarawe baharini.

Licha ya tija zake kiafya na kimapato, ni wachache mno wanaokuza mboga hiyo nchini, hili hasa likionekana kuchangiwa na kutokuwa na ufahamu wa manufaa yake.

Maeneo yanayoonekana kujikakamua kukidhi kiu cha waraibu walaji wa brokoli ni Murang’a, Laikipia, Kiambu, Nairobi, Makueni na sehemu kadhaa Bonde la Ufa.

Broccoli zinaweza kukuzwa chini ya mfumo wa unyunyiziaji mimea na mashamba maji kwa mifereji, maarufu kama Irrigation na vilevile maeneo yanayopokea mvua ya kutosha.

“Mboga hiyo inahitaji maji ya kutosha, hivyo basi maeneo yasiyopokea kiwango cha mvua ya kuikidhi, mfumo wa kunyunyizia mimea maji kwa mifereji utafanikisha kilimo chake,” asema Margaret Gitau, mtaalamu.

Kulingana na mtaalamu huyo, udongo tifutifu na unaohifadhi maji ndio bora zaidi. “Brokoli zinahitaji maji mfululizo ili kuzinawirisha na kupata mazao bora,” asisitiza mdau huyo kutoka kaunti ya Murang’a. Aidha, uchachu wa udongo, pH, unapaswa kuwa kati ya 5.5 – 6.5.

Bw Eric Mutunga ni mkulima wa mboga hiyo kaunti ya Kiambu, na alianza kuikuza ipatayo miaka miwili iliyopita. Kijana huyo pia hukuza mseto wa mboga kama vile spinachi, sukuma wiki, mnavu – sucha na mchicha – terere.

Hata ingawa analima broccoli kwenye kipande kidogo tu cha shamba, anaiambia Akilimali kwamba soko la mboga hiyo ni mithili ya mahamri moto. “Brokoli moja na ni ile ndogo haipungui Sh30,” asema.

Wakati wa ziara katika shamba analoendeleza shughuli za kilimo tulimkuta akiwa na mboga kadha, moja akiiuza Sh50.

Upanzi

Ikizingatiwa kuwa kuna upungufu wa brokoli nchini, Mutunga anasema ni miongoni mwa mboga rahisi mno kupanda, ikiwa mkulima ana chanzo cha maji ya kutosha. Pembezoni mwa shamba la mkulima huyo, kuna mto na pia amechimba mitaro inayochipuka maji ardhini.

Kuna njia mbili za kupanda mboga hiyo; kupanda mbegu moja kwa moja au kupitia miche. Aidha, miche inachukua karibu muda wa wiki sita kitaluni. Matunzo yake yanawiana na ya kabichi au mboga zingine zinapandwa kupitia miche.

Miche inayopaswa kuhamishiwa shambani ni iliyo na kimo cha sentimita 8 – 10, au iwe na majani matatu ama manne.

“Shamba likiwa tayari, mkulima aandae mashimo au mitaro. Ingawa mfumo wangu ni wa mitaro,” afafanua mkulima Mutunga. Kitaalamu, mitaro inapaswa kuwa kati ya sentimita 40 – 90, nafasi kutoka mtaro mmoja hadi mwingine. Wakati wa upanzi, miche ipewe gapu ya sentimita 30 – 60, kwa sababu ya upana wa majani ya brokoli zinapokua na kukomaa.

Watalaamu wa masuala ya kilimo wanasema brokoli inahitaji madini mengi ya Nitrogen na Potassium. Mkulima anahimizwa kabla ya upanzi, aweke mitaro au mashimo mbolea hai kwani imesheheni Nitrogen, Phosphorous na Potassium. Inapaswa kuwa iliyoiva sawasawa, decomposed.

Palizi ni shughuli muhimu katika kilimo cha brokoli. “Ili kuzuia makwekwe kumea, mkulima aweke nyasi zilizokauka kwenye mashina (nyasi za boji),” ahimiza Bw Mutunga.

Zikiwa na umri wa kati ya wiki nne hadi saba, iweke fatalaiza iliyosheheni Calcium, Ammonium na Nitrogen, hatua hiyo ikifahamika kama top dressing. Muhimu wakati huo ni kuitunza kwa maji.

Huanza kuvunwa kati ya siku 45 – 60, baada ya upanzi.

Sawa na kabichi, brokoli pia hushambuliwa na wadudu kama viwavi na vidukari. Magonjwa yanayoshuhudiwa ni downy mildew, damping-off, leaf spot na black rot.

Manufaa kiafya

Brokoli ni kiini kizuri cha fibre, madini muhimu katika kusaidia usagaji wa chakula mwilini. Inaaminika pia hupunguza kiwango cha mafuta ya cholesterol.

Virutubisho vingine ni Vitamini C, Protini, Potassium na Calcium – madini yanayosaidia kuimarisha mifupa. Wenye shida ya ugonjwa wa Kisukari, wanahimizwa kula brokoli kwa wingi kwani huudhibiti.