Makala

AKILIMALI: Huchonga mifupa na kuigeuza bidhaa za thamani

July 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES ONGADI

NI takriban mita 50 kutoka kituo cha polisi cha Changamwe, Mombasa, ndiko liliko soko la New Magongo ambako kila mmoja anaonekana akiwa akitumia ujuzi aliojaliwa kusaka riziki.

Hapa kuna wachongaji vinyago, kuna wanaounda vyatu aina ya kirikiri (akala) wakitumia magurudumu ya magari na pia wamo wanaouza tumbaku (ugoro) alimradi wamepata mkate wao wa kila siku.

Hata hivyo, Benson Mutavi Mutua, 34, kaamua kutumia mbinu tofauti ya kuhakikisha maisha yamemnyookea.

Anatumia mifupa kuunda mapambo ya shingoni kama mikufu, pete mapambano ya kuvaa mkononi, kisu maalum cha kupakia siagi na mwiko.

“Hivi ndivyo ninavyojichumia riziki kupitia kuchonga bidhaa hizi baada ya kusaka ajira kwa muda mrefu bila kufaulu,” asema Mutua katika mahojiano na Akilimali hivi majuzi.

Mutua asema baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya msingi mwaka wa 2010 eneo la Makindu kaunti ya Makueni, aliamua kufululiza moja kwa moja hadi Mombasa kusaka ajira.

“Tuliishi maisha ya uchochole hivyo wazazi hawangemudu kulipia karo kuendeleza masomo yangu ya upili, njia ya pekee ikawa ni kuja mjini kusaka ajira,” asema.

Hata hivyo, hali haikuwa rahisi kama alivyotarajia kwa sababu hakuwa na ujuzi ambao ungemwezesha kuajiriwa.

Baada ya kuwaza na kuwazua akifanya kazi za mijengo, aliamua njia aula ni kujifunza kazi ambayo angelitegemea kujisaidia na hata wazazi wake mashambani.

Mutua alijipiga moyo konde na kuamua kujifunza kazi ya uchongaji vinyago ambayo kipindi hicho ilikuwa yenye hela si haba.

Kwa kipindi cha miezi mitatu, Mutua alifunzwa na rafiki yake wa tangia utotoni namna ya kuchonga aina mbali mbali ya vinyago.

Baada ya kipindi kifupi alikuwa tayari amejua kuchonga aina tofauti ya vinyago alivyowauzia watalii na wenye hoteli za kitalii waliozuru soko lao la New Magongo.

Lakini baada ya wengi kuingilia kazi ya uchongaji wa vinyago, mapato yake katika kazi hiyo yalianza kudidimia na ndipo akaamua kutumia mbinu mbadala kujipatia mkate wa kila siku.

“Nilianza kuchonga mikufu ya shingoni na mwiko nikitumia mifupa badala ya mbao na kuvutia wateja wengi,” asimulia.

Oda

Kulingana na Mutua, ujuzi huu uliwavutia wateja wengi hasa kutoka maeneo kama Malindi, Kilifi, Watamu, Ukunda na Lamu waliompatia oda ya kuwaundia bidhaa hizi kwa wingi.

Na, je, Mutua anapata wapi mifupa ya kufanyia kazi yake?

“Ninapata mifupa katika vibanda vya kuuza marondo ninayouziwa kwa kiasi kidogo cha hela,” afichua Mutua.

Kisha baada ya kununua mifupa hiyo, Mutua anatumia kemikali maalum kusafisha mifupa kabla ya kuanza kuunda bidhaa anayonuia.

Anasema kemikali hiyo husafisha kwa kuondoa uchafu wote.

Kulingana na Mutua anauza mkufu mmoja kwa kiasi cha kati ya Sh50 hadi 100 wakati mwiko mmoja akiuza kwa Sh100.

Mbali na kuchonga bidhaa hizo, Mutua pia anachonga herufi huku akichonga moja kwa kati ya Sh10 hadi Sh20.

Anafichua kwamba wakati mambo yamemwendea vyema anauza kati ya Sh1,000 hadi Sh2,500 kwa siku jambo ambalo anasema limeweza kubadilisha maisha yake.

Ijapo maisha yanazidi kuwa magumu kila uchao lakini Mutua asema kwamba ubunifu wake umeweza kumtenga na tabia ya ombaomba ambayo imekita miongoni mwa vijana wengi wasio na kazi.

Anawashauri vijana kuwa wabunifu na kuwa tayari kufanya kazi yoyote ile kwa bidii ili kujinasua katika hali ya uchochole inayoletwa na ukosefu wa kazi.