• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 1:22 PM
AKILIMALI: Kampuni ya maembe afua  kwa wakulima wa eneo kame

AKILIMALI: Kampuni ya maembe afua kwa wakulima wa eneo kame

Na PETER CHANGTOEK

Kaunti ya Kitui ni miongoni mwa kaunti ambazo huathiriwa na kiangazi. Hata hivyo, miembe ni aina ya mimea ya matunda ambayo hustahimili kiangazi kinachoshuhudiwa katika maeneo kama hayo.

Wakulima wamekuwa wakipata hasara wakati wanapoyachuma maembe yao na kukosa soko la kuyauzia mazao hayo, hususan yanapoiva kwa wingi.

Hata hivyo, baada ya kuasisiwa kwa kampuni kadha wa kadha za kutengeneza sharubati na bidhaa nyinginezo zinazotokana na matunda hayo, wakulima sasa wana kila sababu ya kutabasamu, maadamu mashirika hayo huwapa fursa aula ya kupata tija kwa kuyauza matunda yao kwayo.

Kampuni ya Kitui Enterprise Promotion Company (KEPC) ni mojawapo ya kampuni zinazowawezesha wazalishaji wa maembe kupata tija kutoka kwa mazao yao kwa kuyanunua na kuyatumia kuitengeneza sharubati kati ya bidhaa nyingine nyingi.

Ilipoasisiwa mwaka 2008, madhumuni ya kampuni hiyo yalikuwa kuwahamasisha akina mama kukabiliana na athari zinazosababishwa na kubadilikabadilika kwa hali ya hewa, na changamoto ya kuharibika kwa maembe baada ya kuchumwa kutoka mashambani.

Kampuni hiyo hutengeneza juisi ya maembe pasi na kuzitumia kemikali.

“KEPC hutengeneza sharubati ya maembe, poda ya maembe na unga ulio na virutubisho ikiwa na lengo la kuongeza riziki kutokana na mazao ya kilimo, kwa wakulima wadogo wadogo zaidi ya 800 katika kaunti hii kwa kutumia teknolojia faafu, ujuzi na rasilimali zilizopo,” asema Bw David Muthoka ambaye ni mwenyekiti wa KEPC.

Poda inayotengenezwa na kampuni hiyo ni salama kwa utengenezaji wa juisi na kwa kuchanganywa na unga wa kutengeneza uji.

Kampuni hiyo imewapa mafunzo zaidi ya wakulima 800 kuhusu jinsi ya kuyahifadhi maembe baada ya kuchumwa, na jinsi ya kukabili mabadiliko ya hali ya hewa kupitia kwa ukuzaji wa miembe.

Aidha, ina wafanyakazi zaidi ya 30; wengi kati yao ni wa kike na vijana.

Muthoka anadokeza kuwa ufanisi wa kampuni hiyo umechangiwa na ubunifu ambao umechangia kwa hali na mali kukua kwa uchumi, na kufaidi aila zaidi ya 20,000 ambazo zilikuwa zikikabiliwa na umaskini.

James Mutio ni mmojawapo wa wakulima ambao wamenufaika kutoka kwa kampuni hiyo.

Alianza kwa kuikuza mimea 50 ya miembe mnamo mwaka 2012. ?“Kwa wakati huu nina miembe 200, na awali nilikuwa nikikumbwa na hasara iliyokuwa ikisababishwa na kuharibika kwa matunda,” afichua.

Kwa wakati huu, kampuni hiyo huzalisha zaidi ya lita 500 za sharubati kwa siku, ambapo lita moja huuzwa Sh100.?KEPC imewahi kupata ufadhili kutoka kwa shirika la NETFUND, ili kuziboresha shughuli zake za kuongeza thamani kwa maembe yanayozalishwa na wakulima katika kaunti hiyo.

Serikali ya kaunti ya Kitui imeisaidia kampuni hiyo kwa kutangaza kuhusu bidhaa zinazotengenezwa nayo katika hafla zinazoandaliwa katika kaunti hiyo na nje ya kaunti yenyewe.

Kampuni nyingine ya kuongeza thamani kwa mazao ya maembe ni Mwingi Value Addition Enterprises Limited (MVAEL), ambayo ilisajiliwa mnamo mwaka 2017. ?Kampuni iyo hiyo, hushirikiana na makundi ya kijamii kwa kuyanunua maembe na kuyaongezea thamani kwa kuzitengeneza bidhaa za kila nui kutoka kwa matunda hayo.

Mradi uo huo, pia, unanuiwa kuongeza riziki na hivyo kupunguza umaskini kwa wakulima walioko katika kaunti ya Kitui.

Kampuni hiyo hushirikiana na makundi 36 ya wakulima, yenye jumla ya wakulima 900 na ina zaidi ya wafanyakazi wanane, na huwaajiri vibarua kadha wa kadha, wakati wa misimu ya kuchumwa kwa maembe.

Aidha, kampuni huyo imepokea ufadhili wa fedha zaidi ya milioni tatu na laki tano kutoka kwa shirika la NETFUND, ili kuziboresha huduma zake.

You can share this post!

Mazingira safi yatasaidia kudhibiti maradhi ya kansa

MBURU: Ni wazi, viongozi wa wafanyakazi hawana haja nao

adminleo